Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Busokelo, David Kittivo akiwa ameshika kitabu cha Mwongozo wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria Kikao cha Uzinduzi wa Programu hiyo katika ngazi ya Halmashauri ya Busokelo iliyopo wilayani Rungwe (Picha na Joachim Nyambo).
Wadau mbalimbali waliohudhuria Kikao cha Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) katika ngazi ya Halmashauri ya Busokelo iliyopo wilayani Rungwe wakiendelea kufuatilia mada kutoka kwa wataalamu wa programu hiyo kutoka ngazi ya Mkoa wa Mbeya(Picha na Joachim Nyambo).
Afisa Maendeleo ya Jamiii Mkoa wa Mbeya, Elukaga Mwalukasa (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Busokelo, David Kittivo kitabu cha Mwongozo wa utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) baada ya uzinduzi wa Programu hiyo kwenye ngazi ya halmashauri.(Picha na Joachim Nyambo)
…………………
Kwa mtoto isiishie Lishe Bora ni Lishe Bora kwa Ratiba sahihi
Na Joachim Nyambo.
WATAALAMU wa masuala ya Afya wana kauli isemayo ujionavyo ni kutokana na vile unavyokula. Hii ina maana anachokula binadamu au kiumbe hai chochote ndicho huufanya mwili wake uonekane vile ulivyo.
Ni kutokana na hali hiyo wataalamu wa masuala ya lishe wanasisitiza pia umuhimu wa lishe bora kwa watoto kuanzia wakiwa kwenye matumbo ya mama zao, baada ya kuzaliwa na kadiri wanavyoendelea kukua hadi kufikia utu uzima na hadi uzeeni.
Wataalamu wa Afya wanaeleza kuwa Lishe bora kwa mtoto ni sehemu ya mambo muhimu matano yanayowezesha ukuaji stahiki wake. Yaani Lishe inaungana na mambo mengine manne ambayo ni pamoja na Malezi yenye muitikio, Afya bora, Ulinzi na Usalama na Ujifunzaji wa awali.
Lakini Lishe isiyo ya Mlo Kamili pia si bora hivyo lazima izingatie vyakula vyenye kuwezesha mlo kamili.Mlo kamili ni mkusanyiko wa vyakula mbalimbali ambavyo kwa pamoja huimarisha na kuujenga mwili wa binadamu na wanyama kwa sababu vinaleta virutubishi vyote vinavyohitajika.
Josephine Swai ni Afisa Lishe wa Mkoa wa Mbeya, yeye anasema kwa watoto wadogo suala la lishe sahihi haliishii tu kwa uandaaji wa vyakula vya mlo kamili bali ratiba iliyo sahihi pia ni muhimu. Ratiba ya ulaji wa mtoto mdogo ni tofauti na ya mtu mzima.
Ni kwa kulipa uzito jambo hilo Swai anasema kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha maeneo yaliyotengwa maalumu kwaajili ya utoaji huduma kwa watoto wadogo yanazingatia muda wa kuwalisha watoto. Iwe ni majumbani au kwenye vituo vituo maalumu, na mashuleni kwa madarasa ya awali, la kwanza na darasa la pili yaliyo na wanafunzi wenye umri mdogo.
Anasema vituo vinavyotoa huduma ya malezi kwa watoto wadogo wakati wa mchana vinatakiwa kuzingatia utoaji wa milo sahihi kwa watoto badala ya kuwalisha kwa kufuata ratiba ya watu wazima hatua inayoweza kuathiri ukuaji wao.
Ili kuwezesha ufuatiliaji wa hilo ianashauri kuwepo kwa mawasiliano ya karibu baina ya wazazi na walezi wanaowapokea watoto hao asubuhi ili kujua iwapo watoto walipata kifungua kinywa nyumbani kabla ya kupelekwa kwenye kituo husika.
Alitoa rai hiyo alipowasilisha Mada ya Lishe Bora kwa Watoto kwenye Kikao cha Uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(PJT-MMMAM) katika ngazi ya Halmashauri ya Busokelo iliyopo wilayani Rungwe.
PJT-MMMAM ni programu maalumu iliyoanishwa nchini kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau mbalimbali wakiwemo Children in Crossfire (CiC), Mtandao wa Maendeleo ya awali ya mtoto nchini(Tecden) na Muungano wa Klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC).
Programu hii inalenga kuyaangazia maisha ya watoto walio na umri wa kuanzia miaka sifuri hadi miaka nane katika nyanja za Afya bora, Lishe bora, Ujifunzaji wa awali, Ulinzi na usalama na Malezi yenye mwitikio. Hizi ni nyanja kuu tano zinazomwezesha mtoto kukua kwa utimilifu zikiwa zinategemeana kwa umoja wake.
Swai anasema kumekuwepo na vituo ambavyo hutoa milo miwili kwa muda ambao watoto wako chini yake ratiba aliyosema huenda ikawa inakwenda sawa na ya mtu mzima iwapo mtoto husika hakupata mlo wa kwanza akiwa nyumbani. Yaani kwa muda wanaokuwepo kituoni hapo watoto walipaswa kupata milo mitatu au zaidi.
Anasema iwapo mtoto anafikishwa kituoni saa mbili inabidi apewe chakula mara tu baada ya kufikishwa kama hakulishwa nyumbani kisha milo mingine miwili ifuatie baadaye. Hii ni kwa sababu pia ulaji wa mtoto kwa mlo mmoja waweza usiwe kwa kula chakula kingi na cha kukaa kwa muda mrefu tumboni.
“Mzazi unaweza ukajua mtoto anapata chakula kituoni hivyo ukaacha kumpatia nyumbani kabla ya kumpeleka matokeo yake utakuta anakula kwa ratiba sawa na yako wewe uliyepo kazini. Kama unampeleka saa mbili akaanzishiwa mlo wa kwanza saa nnee unaofuata akala saa nane hana tofauti na wewe jambo ambalo si sawa.” Anasisitiza Swai.
“Ni muhimu kama mtoto atafikishwa kituoni muda huo basi mzazi na mlezi wawasiliane ili kama hakula chochote nyumbani ale mara tu baada ya kufika na ndipo hiyo milo mingine ya saa nne na kuendelea ifuatie.”
Afisa huyo pia anasema utaratibu huo wa lishe pia unawahusu wanafunzi wa madarasa ya kwanza na la pili kwakuwa na wao bado wako katika umri mdogo usiopaswa kula kwa ratiba ya watu wazima. Hivyo ni muhimu pia walimu wa madarasa hayo na wazazi kuwasiliana kwa karibu.
Kwa upande wa watoto waliofikisha umri wa miezi sita wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza baada ya kumalizika kwa kipindi cha kunyonya maziwa ya mama pekee kabla ya kulishwa vyakula vingine wanatakiwa kunyonyeshwa kwanza ndipo walishwe.
“Mtoto anayepewa chakula cha ziada aanze kunyonya kwanza ndipo alishwe chakula kingine. Isiwe unaanza kumlisha vyakula kisha ndipo umnyonyeshe iwe kama vile unampa maji ili ashushie hapana! Aanze kwa kunyonya maziwa ya mama kwanza.” Anasisitiza.
Swai anasisitiza pia umuhimu wa mtoto mdogo kupewa mlo kamili. Yaani ulio na mchanganyiko wa vyakula vya makundi yote muhimu kama ilivyo kwa mtu mzima japo uaandaaji wake ndiyo utatofautiana ili kumrahisishia ulaji wake.
Makundi ya vyakula yanayotakiwa kuzingatiwa ni vyakula vinavyojenga mwili, vinvyoupa mwili nguvu na vinavyoupa mwili joto ambapo kwenye makundi hayo kuna vyakula vilivyo na protini, mafuta, wanga au kabohidrati, vitamini na nyinginezo.
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Itika Mlagila anasema kutokana na wanaume kukosa elimu ya lishe bora kwa wajawazito, wanaonyonyesha na pia watoto wachanga familia hazitengi bajeti za baadhi ya makundi ya vyakula ambavyo ni muhimu kwenye ukuaji wa watoto.
Mlagila alitolea mfano kwa kundi ambalo halipewi kipaumbele na familia nyingi kuwa ni la Protini yaani la vyakula vya mazao ya jamii ya wanyama pamoja na wadudu wote wanaoliwa kulingana na taratibu na imani za watu mbalimbali kama maziwa, nyama, mayai, kumbikumbi na senene.
“Kundi hili linaitwa Protini au Utomwili na kazi yake kubwa ni kuujenga mwili. Hivyo kundi hili ni kama matofali yanayowezesha kuujenga mwili yaani itasababisha mtoto akue kiurefu, aongezeke ukubwa wa ubongo wake na aweze kuzalisha tishu mbalimbali zenye muonekano wa afya bora kama ngozi, kucha na nyinginezo.”
“Na kundi hili asilimia kubwa ya watoto wetu hawapatiwi na wazazi wengi hawaamini kama mtoto akishafikisha umri wa miezi sita kama anaweza akala nyama au akala samaki, wanaamini anaweza kula uji tu. Na takwimu zinaonesha hata hapa kwetu Mbeya wazazi wengi hawalipi umuhimu kundi hili.” Aliongeza.
Elukaga Mwalukasa ni Afisa Maendeleo ya Jamiii Mkoa wa Mbeya anasema kuna changamoto pia la uandaaji usio sahihi wa vyakula vya watoto wadogo. Upo uchanganyaji holela wa aina ya vyakula ambavyo wakati mwingine unasababisha ugomvi baina ya mtoto na mtu anayemlisha. Mtoto anakataa kula kwakuwa hajaridhishwa na ladha ya chakula au kinamletea matatizo.
David Kittivo ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Busokelo, Akifunga Kikao cha uzinduzi wa PJT-MMMAM kwenye halmashauri hiyo aliwataka wajumbe waliohudhuria kuwa mabalozi kwa kufikisha Elimu ya programu husika ili utekelezaji wake uwe shirikishi kwa kila mmoja kutimiza wajibu kwenye eneo lake.
Kittivo aliwataja viongozi wa dini pamoja na wazee maarufu kuwa wadau muhimu watakaowezesha elimu ya programu hiyo kuenea kwa kasi na kutekelezwa na watu wengi kutokana na kusikilizwa na kuaminiwa na jamii wanazoziongoza.
Sera ya Chakula na Lishe ya Tanzania ya Mwaka 1992 pamoja na Sheria namba 24 Chakula na Lishe Tanzania ya Mwaka 1973 iliyorekebishwa na sheria namba 3 ya Mwaka 1995 pamoja na Mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa wanafunzi wa elimu ya Msingi vinaweza kutumika kama miongozo ya kuokoa maisha ya watoto nchini kupitia Lishe bora.