Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo Januari 24, 2024 inatarajia kushuka katika dimba la Amadou Gon Coulibaly nchini Ivory Coast kuminyana na timu ya Taifa ya Jamhuri ya Demokrasia Congo katika mchezo wa Fainali za Mataifa ya Afrika AFCON 2023 utakaopigwa majira ya saa 5 usiku.
Tanzania ambayo ipo kundi F ili isonge mbele katika mashindano hayo makubwa Barani Afrika inapaswa kupata ushindi wa aina yoyote dhidi Congo kwa ajili ya kujitengenezea nafasi nzuri katika kundi.
Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars Hemed Morocco ameahidi timu itapambana kwa jasho na damu ili kuhakikisha inapata ushindi.
Matokeo ya mchezo huo na mengine itakayocheza muda mmoja kati ya Zambia na Morocco katika dimba la Laurent Pokou San Pedro ndiyo itaamua nani asonge mbele na nani abaki.
Timu mbili zitakazomaliza zikiwa nafasi za juu katika msimamo wa kundi F zitatinga hatua ya 16 bora. Ingawa pia kuna timu nne zitakazokuwa na uwiano mzuri wa matokeo na kushika nafasi ya tatu zitakwenda katika hatua hiyo kwa mtindo wa mshindwa bora (Best Looser).