Mkurugenzi wa matengenezo na huduma za ufundi wa wakala wa ufundi na umeme nchini(Temesa)Mhandisi Hassan Koronda akiangalia baadhi ya vifaa vinavyotumika katika matengenezo ya magari ya serikali wakati wa kikao kazi cha Temesa na wadau wa Temesa katika viwanja vya Chandamali Resort mjini Songea.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,akiangalia sanduku la kuhifadhi vifaa vya matengenezo ya magari wakati wa kikao kazi cha Temesa na wadau kilichofanyika katika viwanja vya Chandamali Resort mjini Songea.
Fundi wa magari kutoka wakala wa ufundi na umeme (Temesa) Mkoa wa Ruvuma David Haule kushoto, akimuonyesha mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas kulia,mashine inayotumika kuonyesha waya unaopita chini ya ardhi wakati wa kikao cha Temesa na wadau kilichofanyika mjini Songea.
Viongozi wa Dini waliohudhuria mkutano huo wakimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas(hayupo pichani).
………
Na Mwandishi wetu, Ruvuma.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas,amezitaka taasisi na idara za serikali zinazodaiwa na wakala wa ufundi na umeme(Temesa) kulipa madeni yao haraka ili Temesa iweze kuendesha shughuli zake kwa ufanisi na kufikia malengo iliyojiwekea.
Kanal Laban,ametoa agizo hilo jana,wakati akifungua mkutano wa mpango kazi kati ya Temesa na wadau uliofanyika katika ukumbi wa Jeshi la Wananchi Chandamali Resort mjini Songea.
Aidha,ameziagiza taasisi za serikali mkoani humo, kuhakikisha zinapeleka magari yake Temesa kwa ajili ya matengenezo badala ya kupeleka kwa mafundi binafsi ambao baadhi yao siyo waaminifu.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa,amewataka mafundi wa Temesa kuwa na lugha nzuri kwa wateja wao,kuwa waaminifu na kujiendeleza kitaaluma ili waweze kwenda sambamba na aina ya magari yanayopelekwa kwenye karakana yao.
Laban,amewakumbusha wakuu wa idara na taasisi za umma mkoani humo,umuhimu wa kufanya matengenezo ya magari mara kwa mara ili kuepusha madhara ikiwemo ajali zinazotokana na ubovu wa magari.
Kwa upande wake meneja wa Temesa mkoani Ruvuma Mhandisi Frank Jackson alisema,Temesa)inadai zaidi ya Sh.bilioni 1.2 taasisi na idara za serikali kutokana na kupata huduma ya matengenezo ya magari.
“hadi kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita tunadai zaidi ya Sh.bilioni 1.2 ambazo tunawadai wateja wetu mbalimbali ambao ni taasisi na idara za serikali,lakini tayari tumeshafanya makubaliano na taasisi hizo juu ya kulipa madeni yao haraka ili tuweze kujiendesha na kutoa huduma bora ”alisema.
Alisema,wamejipanga kutoa huduma bora na tayari wamepokea gari moja linalotumika kama karakana(Temesa Mobile Works)ambalo litafika kila wilaya ili kutoa huduma kwa wateja wake.
Jackson,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh.bilioni 1.6 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa karakana mpya na ya kisasa ambayo ujenzi wake utakamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Naye Mkurugenzi wa matengenezo na huduma za ufundi wa Temesa Mhandisi Hassan Kavonda alisema,lengo la mkutano huo ni kupata ushauri kutoka kwa wadau na kufahamu mapungufu yao na kuyafanyia kazi ili Temesa iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mhandisi Hassan,alitumia nafasi hiyo kutaja majukumu yaTemesa ni pamoja na kutoa huduma za ushauri,ufundi na kusimamia matengenezo ya vivuko vyote hapa nchini vilivyomilikiwa na Serikali.
Hata hivyo alitaja changamoto inayowakabili ni ukosefu wa vifaa vya kisasa,mafundi wake kukosa ujuzi na weledi na gharama kubwa inayotolewa kwa wateja ikilinganisha na gharama zinazotozwa na watu binafsi.
Alieleza kuwa,katika kukabiliana na changamoto hizo Temesa imelazimika kuingia mkataba na baadhi ya makampuni hapa nchini kama vile Nissan,Isuzu,Toyota na makampuni mengine ili kupata vifaa kwa ajili ya matengenezo ya magari ya wateja wao.
Mkuu wa utawala na fedha wa Temesa Josephine Matiro,amewaomba wateja ambao ni taasisi na idara za serikali kuwaamini na kuendelea kupeleka magari Temesa kwa ajili ya ushauri wakiufundi na matengenezo.