Katibu wa Halmshauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndugu. Paul Makonda amebainisha kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ilifika kipindi alichukiwa na wana CCM wenzake kutokana na kuonekana kuweka ukaribu na watu wa upinzani, lakini alisimama imara katika dhamira yake na kwakuwa ni mwenye uthubutu aliamua kuridhia na kukutana na Wanawake wa CHADEMA kwa maridhiano.
Hata hivyo, Mwenezi Makonda amesema CCM na Taifa kwa ujumla limesikitika kuona pamoja na dhamira ya dhati ya Mwenyekiti wa CCM na Rais Dkt. Samia aliyonayo bado Viongozi wa CHADEMA wameonesha hali ya kumdhihaki na kumsema vibaya.
Makonda amebainisha kuwa hali hiyo kwa Viongozi hao wa CHADEMA akiwemo Mbowe, Lissu na Mnyika inaonesha wazi ni watu wenye kupambania maslahi yao binafsi na si kwa Taifa letu.
” Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa na Rais Dkt. Samia alikuja haoa kukutana na kukaa mkutano wa maridhiano na Wanawake wa CHADEMA lakini bado Mwenyekiti wao wa CHADEMA pamoja na Viongozi wenzake Lissu na Mnyika wamekuwa wakiendelea kumtukana…lakini tuna imani na Samia na tunaamini Mwenyezi Mungu atamlipia kwa wema wake kwa watu hao,” Alisema Mwenezi Makonda.
Aidha, Mwenezi Makonda amebainisha kuwa uwepo wa Ofisi ya CHADEMA iliyopo Mikocheni ni zao la maridhiano katika falsafa ya 4R za Dkt. Samia na kusema kuwa pamoja na hilo bado hawajawahi kutoa hata shukrani.
Ameyasema hayo leo tarehe 22 Januari, 2024 akizungumza na Wananchi wa Himo Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro akiwa katika muendelezo wa ziara yake.