Na Sophia Kingimali
Taasisi ya Mtetezi wa Mama imepinga vikali maandamano yaliyoandaliwa na chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) yenye lengo la kuitaka serikali kuondoa miswada mitatu Bungeni ambapo maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika januari 24,2024.
Akizungumza na waandishi wa habari januari 20,2024 jijini Dar es salaam mwenyekiti wa hamasa mkoa wa Dar es salaam Mwinyi Ludete amesema hoja walizozitoa CHADEMA hazina mantiki za kutaka kuitisha maandamano bali wamehitisha maandamano ili kuharibu taswira ya nchi.
“Watanzania wanahitaji huduma zote za kijamii zikiwemo maji,Afya na Elimu ambavyo vyote vimepatikana kupitia katiba hii iliyopo ambapo Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan anayatekeleza tena kwa vitendo”Amesema.
Ameongeza kuwa hoja ambazo wamezitoa CHADEMA ikiwemo ya katiba mpya ni hoja inayotaka majadiliano na ni mchakato unaozingatia vipaumbele ambapo kipaumbele cha serikali ni ridhaa ya wananchi katika kuleta maendeleo.
Amesema maandamano hayo ni kichaka cha kuficha uovu unaofanywa na kiongozi wa chama hiko ikiwa ni pamoja na ubinafsi alionao kwa kukaa madarakani muda mrefu bila kupisha wengine.
“Maandamano yamekuwa kichaka cha kuwajibika ili kuonesha kana kwamba Mwenyekiti wa chama hicho anawajibika ili kuficha madhaifu yake ya kiuongozi,huwezi kutaka maandamano kwa kushinikiza mnavyotaka nyinyi”amesema Ludete.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtetezi wa Wamama mkoa wa Dar es Salaam Mohammed Chande amesema uhamasishaji wa maandamano unaofanywa na CHADEMA ni kuishiwa kwa hoja.
Amesema wao kama mtetezi wamekitaka chama hicho kutoa hoja zao na kuziweka kwenye majadiliano lakini si kukimbilia barabani kwani huko kunaonyesha anguko lao.
“Sisi kama Taasisi ya Mtetezi wa Mama tunaiunga mkono serikali na tumejipanga kumsemea Rais wetu kwa hoja za msingi na kama ilivyo kauli yetu Ukimvaa Mama tunakuvaa kwa hoja,hivyo ni wakati wa wao kuleta hija zao lakini si kusababisha fujo na kuiondoa amani ya nchi yetu” Amesema Chande.
Amesema kukosekana kwa hoja ya msingi kumewafanya kuja na hoja za kulazimisha na kuhamasisha maandamano.
Amesema siasa haihitaji hasira bali inahitaji mapinduzi ya mawazo na akili ili kujenga demokrasia ya kweli nchini.
Aidha Chande ametoa wito kwa wananchi kutojitokeza kwenye maandamano hayo badala yake viongozi wa CHADEMA wanapaswa kuchukua familia zao na kuanza kuandamana na si kutumia vijana.
“Nyinyi mnazo nchi za kukimbilia tunaomba mtuachie nchi yetu salama sisi tunataka amani maana Tanzania ndio mama yetu na ndio baba yetu hatuna nchi nyingine zaidi ya hii”ameongeza Chande.
Taasisi ya mtetezi wa wamama wamejipanga vyema kuhakikisha wanaelezea mazuri yote yanayofanywa na serikali hivyo wametoa rai kwa wananchi wote wazalendo kuepuka kutumika katika kuiondoa amani iloyopo nchini.