Na Rashid Nchimbi -Arusha
Wafanyabishara wa kijiji cha Moita Bwawani kilichopo kata ya Moita wilayani Monduli mkoani Arusha, wametatakiwa kutohifadhi mafuta ya Petroli kwenye maduka ya vyakula.
Tahadhari hiyo imetolewa leo asubuhi na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi wa kata hiyo, Mathew Michael wakati akiongea na baadhi ya wafanyabiashara wa kijiji hicho.
Mkaguzi huyo wa Polisi amesema kwamba, pamoja na jambo hilo kuwa ni kinyume cha sheria lakini pia linaweza kusababisha ajali ya moto na kuleta madhara.
“Kutokuwa na vituo vya kuuzia mafuta ya Petroli au Dizeli kijijini hapa, isiwe tiketi ya nyinyi kuhifadhi mafuta ya aina hii kwenye makazi yenu kwa nia ya kufanya biashara.
Kila kitu kina utaratibu uliowekwa na serikali kupitia mamlaka zake na ndio unasababisha tuwe katika mazingira salama”. Alisema Mkaguzi huyo wa Polisi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabishara wenzake waliopo kijijini hapo, ndugu Piniel Lukumay maarufu kama Lemali alisema kwamba wameshukuru kwa elimu hiyo na wameipokea kwa mikono miwili na kuahidi kuifanyia kazi mara moja.