akizungumza jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha
taarifa kuhusu mwenendo wa biashara ya mafuta nchini kwa kipindi cha
mwezi Septemba hadi Disemba 2023, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini. Kikao kimefanyika tarehe 19 Januari 2023 na
kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu
Mkuu, Mhandisi, Felchesmi Mramba, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo
chini ya Wizara na Watendaji wa Wizara ya Nishati.
Asema kampuni ya mafuta TANOIL inaboreshwa ili kuleta ufanisi
Asisitiza PBPA ni nguzo ya Serikali katika uhakika wa upatikanaji mafuta
PBPA yazidi kudhibiti upotevu wa mafuta
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema
kuwa, juhudi zinazofanywa na Wizara ya Nishati, Wakala wa Uagizaji wa
Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati
na Maji (EWURA) zimepelekea gharama za uletaji wa mafuta nchini
(premium) kuendelea kushuka na hivyo kuchangia katika unafuu wa
gharama za mafuta ikiwemo ya dizeli na petroli.
Amesema hayo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma wakati Wizara ya
Nishati ilipowasilisha taarifa kuhusu mwenendo wa biashara ya mafuta
nchini kwa kipindi cha mwezi Septemba hadi Disemba 2023, kwa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Kikao ambacho kilihudhuriwa
na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, Katibu Mkuu,
Mhandisi, Felchesmi Mramba, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya
Wizara na Watendaji wa Wizara ya Nishati.
“ Wizara ya Nishati, EWURA na PBPA, kwa kweli wamefanya kazi kubwa mno
ya kushusha gharama za uagizaji mafuta kutoka nje ya nchi, hapo awali
gharama hizi zilikuwa zikiongezeka kila mwezi lakini wamesimamia
vizuri suala hili na gharama hizi zimeanza kushuka na hivi karibuni
mlisikia Waziri wa Kenya akisema bei za mafuta nchini humo zipo juu na
za Tanzania zipo chini sababu ya premium, na wengine pia walio nje
wanatoa ushuhuda kwamba walau sisi gharama zetu zina unafuu.” Amesema
Dkt. Biteko
Dkt. Biteko ameeleza kuwa PBPA ambayo inasimamia uagizaji wa mafuta
kwa pamoja, ina umuhimu mkubwa nchini kwani ndiyo inayopelekea nchi
kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji ya
nchi na yenye viwango vya ubora unaohitajika, Serikali kufahamu
kiwango cha mafuta kinachoingia nchini, kupanga ukusanyaji wa mapato
kwa kutumia takwimu sahihi na kupanga bei elekezi ya mafuta.
Amesema kuwa, Serikali itaendelea kuisimamia kwa ukamilifu Taasisi
hiyo ili iendelee kufanya kazi kwa ufanisi kwani tayari imekuwa ni
mfano wa kuigwa kwa nchi zinazotuzunguka na kuwataka watendaji wa
Taasisi hiyo kufanya kazi kwa maadili na bila kumuonea mtu yeyote.
Vilevile ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuiboresha kampuni ya
Mafuta ya TANOIL ambayo ni kampuni tanzu ya TPDC kutokana na umuhimu
wake katika biashara ya mafuta nchini na kwamba, TANOIL imekuwa ni
kimbilio hasa katika nyakati ambapo zinatokea changamoto za
upatikanaji mafuta kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio
waaminifu.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi alieleza kuwa, ili
kuboresha mfumo wa upakuaji mafuta melini na kuhakikisha kuwa meli
hazikai muda mrefu bandarini, Serikali iliagiza matenki ya TIPER nayo
yatumike kupokea na kuhifadhi mafuta na hatua hiyo imewezesha meli za
mafuta ya dizeli kutumia siku nne kushusha mafuta badala ya siku tisa
na hivyo kuleta unafuu kwa mlaji na kupunguza gharama ambazo Serikali
inalipa kutokana na muda wa meli kukaa bandarini.
Amesema kuwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ipo
katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa sehemu maalum ya kupokea
na kuhifadhi mafuta ijulikanayo kama single receiving terminal ambapo
meli itakuwa na uwezo wa kupakua mafuta kati ya masaa 48 na 36 na
hivyo kumaliza kabisa changamoto ya gharama za meli kukaa bandarini.
Amesema kuwa, kabla ya kuwepo taasisi ya PBPA upotevu wa mafuta kutoka
bandarini ulikuwa ni asilimia 0.5 lakini hali ya upotevu kwa sasa
imedhibitiwa na upotevu umepungua hadi asilimia 0.1 na kwamba Serikali
inaendelea na jitihada za kuondoa upotevu kabisa kwa kufunga mita za
kupimia mafuta (flow meter) pamoja na mfumo wa uangalizi wa flow meter
(SCADA) ambao utakuwa chini ya PBPA na kwamba mfumo huu utakuwa
unafanya kazi muda wote meli ikiwa inashusha mafuta na hivyo kuondoa
uwezekano wa upotevu wa mafuta kabisa wakati wa ushushaji wa mafuata.
Ameongeza kuwa, mfumo huo wa SCADA utaweza kuona shughuli ya ushushaji
wa mafuta kwa bandari za mikoa inayopokea mafuta ambayo Tanga, Mtwara
na Dar es Salaam.