Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Na: Dk. Reubeni Michael Lumbagala, Kongwa.
Wanafunzi kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vikuu hupata maarifa, ujuzi na stadi mbalimbali kwenye taasisi mbalimbali za elimu wanazosoma.
Katika kufanikisha shughuli muhimu ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni au vyuoni, walimu wanao wajibu wa kufundisha wanafunzi huku wanafunzi wakiwa na wajibu wa kusikiliza na kuzingatia yale wanayofundishwa na walimu wao ili kuweza kupata yale wanayotarajiwa kujifunza.
Shughuli za ujifunzaji hutamatishwa na kupimwa kwa wanafunzi katika yale waliyojifunza. Upimaji huu huwa katika mfumo wa utoaji wa mazoezi, majaribio na mitihani ya kishule na kitaifa. Upimaji katika mitihani hii hutoa taswira ya uelewa wa wanafunzi katika kipindi husika cha ujifunzaji wao.
Mathalani; upimaji kitaifa darasa la nne, hutoa taswira ya uelewa wa wanafunzi katika yale waliyojifunza miaka minne yaani darasa la kwanza hadi la nne.
Kwa wanafunzi wa darasa la saba, hupimwa katika yale waliyojifunza katika kipindi chote cha miaka saba. Pia, upimaji kitaifa kidato cha pili hupima wanafunzi katika yale waliyojifunza katika kipindi cha miaka miwili, hali kadhalika kidato cha nne na sita.
Ili wanafunzi wafanye vyema katika mitihani hiyo, walimu wanao wajibu wa kuwaandaa vyema wanafunzi hao kwa kuwafundisha kikamilifu. Wana dhima pia ya kuhakikisha nidhamu kwa wanafunzi inasimama vyema.
Kwa upande mwingine wa shilingi, wanafunzi wanawajibika kufanya kinachowaweka darasani, kusikiliza kwa umakini, kuuliza maswali pale ambapo somo halijaeleweka, kufanya mazoezi ya darasani na kujisomea vya kutosha ili kujiandaa vyema na mitihani hiyo na hatimaye kuweza kufanya vizuri ili kuendelea na ngazi nyingine ya masomo.
Wazazi pia kwa upande wao wana jukumu la kusimamia nidhamu ya watoto wao, kufuatilia nyendo zao ili kubaini kama kuna vitu vinaweza kuwafanya wasijifunze ipasavyo au kuwa na marafiki wa hovyo, kuwanunulia mahitaji muhimu ya kishule ikiwemo vitabu na mengine.
UDANGANYIFU KWENYE MITIHANI
Udanganyifu unaofanywa na wazazi/walezi, walimu na wanafunzi umekuwa na madhara makubwa kwa watahiniwa wenyewe, kwa shule wanazosoma, kwa jamii nzima na hata kwa taifa.
Mtu anapofaulu kwa udanganyifu, kuna uwezekano kwamba anakwenda kuziba nafasi ya mwingine kwa sababu nafasi huwa ni chache.
Halikadhalika hatumtazamii afanye vizuri katika ngazi nyingine ya masomo anayoiendea. Hebu fikiria mwanafunzi aliyefaulu kwa udanganyifu darasa la saba, kweli aatafanya vizuri kwa masomo ya sekondari? Na kama ndio anatoka chuo, na kubahatika kuajiriwa, unadhani weledi na ufanisi utakuwa mzuri kazini kwake?
Uliwahi kusikia habari ya daktari aliyetakiwa kumfanyia operesheni ya mguu mgonjwa yeye akamfanyia ya kichwa? Kama hujasikia, kwaheri! Lakini baya zaidi udanganyifu husababisha wanafunzi kufutiwa matokeo yao.
UANDISHI WA MATUSI KWENYE MITIHANI YA KITAIFA
Zipo taarifa za baadhi ya watahiniwa wachache huandika lugha za matusi kwenye mitihani ya kitaifa. Jambo hili si ishara njema katika ujenzi wa taifa letu kwani watahiniwa hawa ni sehemu ya raia katika nchi yetu. Lakini wazazi siku hizi tunapokuwa ‘bize’ na kutafuta na kusahau majukumu tunachangia hali hii.
Kwanza, lugha ya matusi ni miongoni mwa tabia mbaya, ni jambo lisilokubalika kuanzia kwenye imani za dini hadi kwenye tamaduni zetu kijamii. Hata katika uga wa kisheria, matusi ni kosa la jinai, hivyo lugha ya matusi haikubaliki abadan asilani.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Said Mohamed.
MATOKEO YA DARASA LA NNE NA KIDATO CHA PILI KWA MWAKA 2023.
Akitangaza matokeo ya kitaifa ya upimaji wa darasa la nne na kidato cha pili, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk. Said Mohamed amesema baraza limefuta matokeo kwa wanafunzi 178 wa darasa la nne na 28 wa kidato cha pili waliofanya udanganifu (jumla watahiniwa 206). Vilevile, baraza limewafutia matokeo wanafunzi watatu wa darasa la nne na 14 wa kidato cha pili (jumla watahiniwa 17) walioandika matusi kwenye karatasi za kujibia mitihani yao.
TUHIMIZE UJENZI WA MAADILI MEMA KATIKA JAMII.
Pamoja na sababu kadhaa ambazo wataalamu wanaweza kuja nazo kama sababu zinazopelekea udanganyifu na uandishi wa matusi kwenye mitihani, lakini kubwa ninaloliona hapa ni mmomonyoko wa maadili.
Katika suala la udanganyifu kwenye mitihani, ni muhimu kwa wazazi au walezi, walimu na wanafunzi wenyewe kuzingatia maadili. Udanganyifu kwenye mitihani ni zao la mmomonyoko wa maadili kwani kwa wazazi, walimu na wanafunzi wenye maadili mema katu hawatakuwa sehemu ya kufanikisha njama za kufanya udanganyifu kutokana na kujua athari zake.
Uandishi wa matusi kwenye mitihani unaofanywa na baadhi ya watahiniwa wawapo kwenye vyumba vya mitihani, ni matokeo ya maadili mabaya waliyonayo baadhi ya wanafunzi. Mwanafunzi mwenye tabia njema, hawezi kuandika matusi kwenye mitihani. Ni muhimu kwa wazazi na walezi kuwajenga watoto wao kwenye maadili mazuri ili waepukane na tabia mbaya ikiwemo hii ya kundika matusi kwenye mitihani ya kitaifa.
Walimu kwa upande wao, wanayo fursa ya kuzuia uandishi wa matusi kwa kuwakumbusha mara kwa mara wanafunzi kuepukana na tabia hii mbaya. Wawakumbushe umuhimu wa kuzingatia maelekezo ya kwenye mitihani badala ya kufanya vitu visivyokubalika. Kimsingi, mwanafunzi aliyejiandaa vyema kwenye mitihani kamwe hawezi kuandika matusi kwani malengo yake ni kufanya vizuri ili avuke ngazi nyingine.
Ni muhimu wanafunzi wakakumbushwa kuwa hata kama wamekosa majibu ya kujaza kwenye karatasi zao za kujibia, waepuke kuandika matusi kwa sababu ni afadhali kufeli mtihani kuliko kufutiwa matokeo kwa kuandika matusi.
Tuzingatie hili kwamba kuanzia ngazi ya familia, ukoo, jamii, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa tunalo jukumu kubwa la ujenzi wa maadili mema katika jamii.
Tukiwa na jamii yenye maadili mema, tukawalea vyema watoto, udanganyifu na matusi kwenye mitihani pamoja na tabia nyingine nyingi mbaya na zenye ukakasi zitatoweka.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.