Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma akizungumzia wiki ya sheria ambayo kitaifa itafanyika mkoani Dodoma mgeni rasmi katika kilele chake atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan sherehe hizo za kilele cha wiki ya sheria zitafanyika kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma
Jaji Profesa Juma amezungumza hayo katika mkutano na waandishi wa habari Leo Januari 17, 2024 kwenye kituo jumuishi cha utoaji haki masuala ya familia Temeke jijini Dar es Salaam
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Elisante Ole Gabriel akizungumza kabla ya Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma kuzungumza na waandishi wa habari.
Wananchi wameombwa kuhudhuria wiki ya Sheria itakayoanza Januari 24 hadi 30, 2024 ili waweze kuona teknolojia inavyotumika kurahisisha upatikanaji wa haki.
Ombi hilo limetolewa leo Januari 17, 2024 na Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma wakati alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kwenye kituo jumuishi cha utoaji haki masuala ya familia kilichopo Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam.
Amesema katika wiki hiyo Mahakama itaonesha hatua mbalimbali iliyopiga katika matumizi ya tehama huku akieleza kuwa teknolojia inamsaada mkubwa katika kuboresha haki pamoja na upatikanaji wake kuwa rahisi.
Profesa Juma amesema moja kati ya mifumo inayosaidia upatikanaji wa haki ni mfumo mpya wa kielektroniki wa kuratibu uendeshaji na Usimamizi wa mashauri ulioanza kufanya kazi Novemba 2023 na inatumia Akili bandia katika kuratibu uendeshaji na usimamizi wa mashauri.
“Mfumo huu unasiadia usajili wa mashauri kupokea nyaraka za mashauri za taarifa zote za migogoro kwa njia ya mtandao hivyo wananchi ni vyema wakajitokeza kwa wingi ili waweze kuona namna inavyofanya kazi”, amesema Profesa Juma
Amesema mfumo huo unafaida nyingi ikiwemo kutunza kumbukumbu ukilinganisha na utumiaji wa mifumo ya makaratasi ambao umekuwa ukipoteza taarifa muhimu.
Aidha, amesema kuwa kauli mbiu itakayoongoza wiki ya sheria ni “Tutaendelea kusisitiza umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa” na wataangali nafasi ya mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai.
Amesema Taasisi zote na wadau katika haki jinai wanawajibu wa kutafakari na kuendeleza suala la haki ambalo ni la msingi katika ustawi wa Taifa.
“Kauli mbiu hii inatoa nafasi nyingine kwa taasisi za haki jinai kutafakari maoni na mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande ilitopewa jukumu la kuboresha taasisi za haki jinai”
Ameeleza kuwa mchakato wa haki hupitia hatua mbalimbali zinazohusisha mahakama na wadau na hatua hizo ni uchunguzi, Upelelezi na Mahakama ambapo kunawaendesha mashitaka hivyo kauli mbiu ya mwaka huu inatupa tahadhari kuwa haki ni muhimu katika shughuli za wadau wote ambao wako kwenye mnyororo wa utoaji haki.
Uzinduzi wa rasmi uatafanyika Januari 27,2024 na utaanza kwa matembezi kuanzia saa 12 asubuhi kuanzia kwenye jengo la Kituo jumuishi Dodoma na kuhitimisha kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoani humo.
Profesa Juma amesema Mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Aksoni huku kilele cha wiki hiyo kikiwa ni Feburuari 1, 2024 kwenye viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma