Mkurugenzi mkuu wa bodi ya utalii (TTB) Damus Mfugale amesema zao la kimkakati la utalii wa meli nchini limeendelea kukua katika sekta hiyo kufuatia ongezeko la watalii linaloendelea kukua siku hadi siku.
Hayo ameyasema leo Januari 16,2024 jijini Dar es salaam wakati akipokea watalii zaidi ya 2000 waliowasili na meli kubwa ya utalii yenye urefu wa mita 294 iitwayo Norwegian Cruise Line Down(NCL).
Amesema watalii hao ambao ni watalii wa meli ni mkakati wa serikali kuendeleza na kukuza utalii huo kwani utasaidia kuongeza pato la taifa na ongezeko la fedha za kigeni nchini.
Amesema baadhi ya watalii hao waliowasili watatembelea vivutio mbalimbali ikiwemo mbuga ya selous na maeneo ya historia bagamoyo na wengine kwenye vivutio mbalimbali jijini Dar es salaam.
“Ujio wa meli hii kubwa ni mkakati wa kukuza sekta ya utalii lakini pia muendelezo wa utalii wa meli ambao ni moja ya mkakati wa serikali kuhakikisha utalii huo unakua kwa kasi hapa nchini”amesema Mfugale
Amesema ujio wa meli hiyo ni mwanzo wa kuingia meli nyingine za utalii ambapo wanatarajia mwezi mwezi wa Februari kupokea meli nyingine kubwa ya watalii nchini ikiwa ni muendelezo wa kuhakikisha zao la utalii wa meli linakua.
Meli hiyo iliyotia nanga leo ikitokea Mombasa ikiwa inaendelea na safari zake za utalii Duniani itaondoka nchini jioni ya leo januari 16,2024.