Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Angola zimesaini Hati tatu za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) katika sekta ya mafuta na gesi, kuondoleana visa kwa wenye hati/pasi za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Angola uliomalizika leo Zanzibar.
Waziri Makamba amesaini hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi. Aidha, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesaini hati ya ushirikiano katika sekta ya afya
Mara baada ya kusaini kwa Hati hizo, Waziri Makamba alisema Tanzania na Angola zina uhusiano wa kihistoria ulioanzishwa na viongozi wakuu wa Kitaifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Agostinho Neto walianzisha uhusiano huo kwa matarajio yao kuwa uhusiano huo utoe manufaa kwa nchi zote mbili.
“Leo kupitia mkutano wetu tumesaini Hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola. Hati hizo ni pamoja na hati ya makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, Hati ya makubaliano ya kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya afya,” alisema Waziri Makamba.
Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa kisiasa, ulinzi, elimu, afya, mafuta na gesi, uchumi wa buluu, usafiri wa anga, kubadilishana visa, kusafiri bila visa kati ya nchi zetu mbili na hatimaye tumeingia makubaliano ya ushirikiano.
Kuadhalika, viongozi hao pia wamekubaliana kuyafanyia kazi masuala mbalimbali husasan uwepo wa ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya Kongamano la bishara na uwekezaji na kuziwezesha sekta binafsi kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano zaidi.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja walizokubaliana kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupitia makubaliano tuliyosaini leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tuahidi kuyatekeleza yale yote tuliyokubaliana katika mkutano wetu ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu,” alisema Balozi António.
Aidha, kuhusu kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya kongamano la biashara na uwekezaji ili kuwawezesha wananchi wetu kubadilisha uzoefu na kuendelea kukuza sekta binafsi kwa mataifa yote mawili.