Timu ya Taifa ya Senegal wameanza kwa kishindo baada ya kuichapa timu ya taifa ya Gambia mabao 3 – 0 katika mchezo wao wa kwanza kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 uliofanyika Januari 15, 2024 kwenye Uwanja wa Yamoussoukro.
Timu ya taifa ya Senegal ambao wapo kundi C ilianza harakati zake za kuwania taji la AFCON kwa ushindi wa mabao 3 katika mchezo ambao ulikuwa na upinzani mkubwa.
Senegal walipata bao la kwanza mapema, huku kiungo wa Olympique de Marseille Pape Gueye akifunga dakika ya 4 kwa pasi nzuri ya Sadio Mané.
Katika dakika ya 45+5’, mambo yalizidi kuwa magumu kwa Gambia huku Ebou Adams alitolewa kwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu katika mchezo huo, na kuiacha timu yake katika hali mbaya.
Katika kipindi cha pili cha mchezo huo, mchezaji wa Metz mwenye umri wa miaka 20 Lamine Camara aliendeleza uongozi kwa 2-0 dakika ya 51 kwa mwendo wa ajabu katika eneo la hatari baada ya kupiga shuti kali lililomwacha kipa Baboucarr Gaye bila majibu.
Katika dakika za mwisho za mchezo huo, Lamine Camara kwa mara nyingine alifanya vyema baada ya kuipatia Senegal bao la 3 dakika ya 86.
Mchezaji huyo chipukizi alifunga mara mbili katika mechi yake ya kwanza katika Kombe la Mataifa ya Afrika, kuifanya timu yake kuwa na mwanzo mzuri wa kuwania ubingwa huo.
Mchezo mwengine timu ya taifa ya Cameroon ilishuka dimbami kuminyana na Guinea mchezo ambao ulimalizika kwa sare bao moja kwa moja.
Senegal ambao wataendelea na safari yao ya kuwania kombe la AFCON 2023 Januari 19, 2024 watakapominyana na Cameroon, mechi ambayo bila shaka itakuwa ya kusisimua zaidi katika hatua hii ya makundi, huku Gambia itajaribu kubadilisha mambo itakapomenyana na Guinea.
Pia katika kundi D timu ya taifa Algeria ilishuka dimbani kuminyana na Angola mchezo ambao walitoshana nguvu baada ya kutoka na sare ya bao moja kwa moja.