Nishati jadidifu imetajwa kuwa chanzo kikubwa cha kupunguza matatizo na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana kwa sababu inazalisha umeme wa uhakika na kutoa nafasi ya ajira kupitia nishati hiyo.
“Nishati mbadala inaweza kunufaisha matabaka yote ya jamii kwa usawa zaidi, hasa wajasiriamali wadogo kutokana na upatikanaji wa nishati kwa bei nafuu na kutoa mafunzo.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Januari 11, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Kampuni ya CSI Energy Group, Bi. Natacha Emilien akitoa shukurani zake baada ya uteuzi huo ambapo pia ameeleza dira ya kampuni hiyo inayojihusisha na nishati.
“Kampuni hiyo pia inasaidia katika kushirikiana na wajasiriamali wanawake kama wakandarasi wadogo katika mnyororo wa thamani,”amesema Natacha.
Wakati Tanzania na dunia kwa ujumla ikipambana na mabadiliko ya Tabia nchi, matumizi ya nishati jadidifu yanatajwa kuwa suluhu ya changamoto hizo ambayo italeta faida kubwa kwa jamii lakini pia kwa mazingira .
Akizungumza katika kongamano la mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia uliofanyika jijini hapa Novemba 2022, Mkurugenzi wa Taasisi ya Climate Action Network Tanzania, Dk Sixbert Mwanga alisema tafiti nyingi zinaonyesha Tanzania ina kiwango kikubwa cha nishati safi inayotosheleza mahitaji ya wananchi wake.
Alisema nishati jadidifu ni chanzo kingine muhimu kitakachowezesha uzalishaji umeme bora kwa bei rahisi na kutosheleza mahitaji ya nchi.
“Nishati mbadala zilizopo ukifuatilia zinatosha na uzuri wa hizi hazihitaji kufuatwa na gridi ya Taifa, badala yake zenyewe ndiyo zinaifuata gridi ili ziende kufidia wengine wenye upungufu.”
Jitihada za Tanzania katika nishati jadidifu
Wakati bosi wa CSI akitaja faida za matumizi ya nishati jadidifu kwa wananchi, Tanzania miezi michache iliyopita imetoka kusaini mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (Irena) ambao utasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji wa nishati isiyo rafiki.
Oktoba 31, 2023 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alitaja faida za mkataba wa Irene alipokuwa akiwasilisha azimio la mkataba huo bungeni jijini Dodoma.
Dk Biteko alisema mkataba huo utasaidia kuimarika kwa mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa nishati ya umeme na kuliwezesha Taifa kuwa na vyanzo mchanganyiko vya umeme unaoendana na mahitaji ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii, pia kutatua changamoto ya vyanzo vya umeme visivyo endelevu na uhakika.
Faida nyingine ni nchi kupata taarifa na takwimu sahihi kuhusu masuala ya nishati jadidifu, fursa za uwekezaji katika nishati hiyo zilizopo, kuimarika kwa utaalamu, teknolojia, utafiti na uelewa kuhusu nishati jadidifu kwa watoa maamuzi na wadau mbalimbali wa nishati.