Na Sophia Kingimali
Kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika bandari ya Dar es Salaam imepelelekea kupokea meli kubwa yenye urefu wa mita 294 iliyobeba watalii zaidi ya 2, 000.
Akizungumza leo januari 16,2024 baada ya kuwasili meli hiyo kwenye Bandari ya Dar es salaam Mkurugenzi wa bandari hiyo Mrisho Mrisho amesema ujio wa meli hiyo umedhihirisha maboresho makubwa yaliyofanywa hasa katika uchimbaji wa kina kirefu na upanuzi wa lango la kuingilia meli.
“Kwa bandari ya Dar es Salaam hii ndio meli ndefu ya kwanza kwa ukubwa wake kuweza kuingia tangu uhuru hii imetoka na maboresho yaliyofanyika katika kuchimba kina kirefu lakini pia upanuzi kwa hili tunajivunia sana na kuishukuru serikali”amesema Mrisho.
Amesema meli hiyo umechukua nafasi ya meli tatu ambazo wanazihudumia kila siku yaani gati namba 1,2 na nusu ya gati namba 3.
Aidha ameongeza kuwa matarajio ya bandari hiyo ni kuhudumia meli zenye urefu wa mita 305.
Kwa upande wake nahodha mkuu wa mamlaka ya bandari(TPA) Abdula Mwingamno amesema meli yenye ukubwa huo haijawahi kuingia kwenye bandari yeyote za TPA.
Amesema kuboresha mlango wa kuingilia meli utasaidia kuingiza bandari ya Dar es salaam,Tanga na Mtwara kwenye ushindani wa kibiashara.
Aidha ametoa rai kwa wafanyabiashara kuendelea kuingiza meli zenye ukubwa wa mpaka mita 305 muda wowote na si kama ilivyokuwa awali ambapo meli zenye ukubwa huo zilikua zikiingia mchana.