Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani akizungumza na madaktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) waliofika katika Mkoa wa Tabora kwaajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa mkoa huo. Kambi hiyo maalumu ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Program ya siku tano imeanza leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE Dkt. Mark Waziri akitoa neno la shukrani kwa madaktari bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwafikia wananchi wa Tabora wakati wa kuwapokea madaktari hao leo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora kabla ya kuanza kambi maalumu ya matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Program ya siku tano inayofanywa na madaktari hao.
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na mratibu wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Program Loveness Mfanga akielezea huduma zitakazotolewa katika kambi maalumu ya siku tano iliyoanza leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE leo mkoani Tabora.
Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE wakisikiliza wakati wa kikao cha namna ya kutoa huduma kwa wananchi wa mkoa wa Tabora wakati wa kambi maalumu ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Program iliyoanza leo mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE mara baada ya kukutana na wataalamu hao kabla ya kuanza kwa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Program iliyoanza leo mkoani Tabora.Picha na: JKCI.
……..
Na: Mwandishi Maalumu – Tabora.
Wananchi wa mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani wametakiwa kutumia fursa ya uwepo ya wataalamu wa afya mabingwa wa moyo vizuri kuchunguza afya za mioyo yao na kupata ushauri wa namna ya kujikinga na magonjwa moyo.
Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akiwakaribisha wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika ofisi yake kabla ya kuanza kwa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Program inayofanyika kwa siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETEMhe.
Batilda alisema huduma hiyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan outreach program itasaidia kubadilisha fikra za watu kwani imehusisha wataalamu wa lishe wanaotoa elimu kuhusu lishe bora na namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo.
“Nimefurahi kuona mmekuja na wataalamu wa lishe kwani katika mkoa wetu wa Tabora kumekuwa na makundi mawili yanayokinzana katika masuala ya lishe kwani watu wazima wamekuwa wakila vyakula vya asili na kupunguza kwa asilimia kubwa vyakula vyenye mafuta mengi lakini upande wa vijana maisha hayako hivo wao hupendelea kula vyakula vya kisasa na vilivyopikwa na mafuta mengi”, alisema Mhe. BatildaAidha Mhe.
Batilda ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE kufikisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Tabora na mikoa ya jirani.
“Kupitia kambi maalumu za matibabu ya moyo wanazofanya JKCI zinatoa ishara ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kuhakikisha kuwa afya za watanzania zinaboreshwa”, alisema Mhe. Batilda.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE Dkt. Mark Waziri alisema huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo imekuwa adimu kwa mkoa wa Tabora kwani kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa madaktari bingwa na wabobezi wanaotibu magonjwa ya moyo.
Dkt. Waziri alisema huduma ya tiba mkoba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan outreach program imesogeza huduma za tiba ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Tabora ambao wamukuwa wakifuata huduma hizo mkoani Dar es Salaam.
“Kupitia kambi hii wataalamu wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE wataenda kujengewa uwezo ili pale watakapokutana na wagonjwa wa moyo waweze kuwahudumia kwa wakati”, alisema Dkt. Waziri.
Aidha Dkt. Waziri amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza vifaa tiba vya kutosha na kuruhusu tiba mkoba ya uchunguzi wa matibabu ya moyo kuwafikia wananchi wa Tabora.
Naye mtafiti wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Loveness Mfanga alisema wataalamu wa afya kutoka JKCI wamefika mkoani Tabora kwaajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani.
Loveness ambaye pia ni mratibu wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan outreach program alisema huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na kuangalia mfumo wa umeme wa moyo.
“Huduma nyingine tutakayotoa ni ile ya kupima magonjwa ya shinikizo la damu na magonjwa ya sukari mwilini pamoja na kutoa elimu ya lishe kuwalinda wananchi wasipate magonjwa yasiyoambukiza”, alisemaLoveness.