Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso leo Januari 15, 2024 jijini Dodoma amefanya kikao maalumu cha tathimini ya utendaji wa Wizara ya Maji kwa mwaka 2024 ambapo pamoja na mambo mengine msisitizo mkubwa umeuweka kwenye eneo la uchimbaji visima na Ujenzi wa Mabwawa ambapo pia Naibu Waziri wa Maji Mhe Maryprisca Mahundi amehudhuria kikao hicho.
Aidha ameeleza matamanio na malengo yake wazi na kumuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof.Jamali Katundu kuweka uangalizi maalum katika eneo hili ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya Utendaji wa Magari ya Uchimbaji visima hususani eneo la ufanisi na Gharama za uchumbaji visima hivyo.
Akizungumza kwa msisitizo ameeleza kuwa tathmini ya kina ifanyike na mchakato wa kutengeneza mfumo ambao utakua na misingi bora ya utendaji uanze mara moja.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameyasema hayo alipofanya kikao na Menejimenti ya Wizara na kuwataka kuhakikisha mwaka 2024 unakuwa na matokeo chanya kwa Watanzania wote katika Kuhakikisha huduma ya Maji inafika kila kona ya nchi na kwa kasi.
Katika hatua nyingine Aweso amesema mafanikio yaliyopatikana mwaka 2023 yako wazi kwa kila mwananchi lakini yako maeneo ambayo Wizara haikufanya vizuri sana hivyo ni wajibu watendaji kuhakikisha wanarekebisha pale ambapo mambo hayakwenda vizuri.