Na. Koplo Issa Mwadangala wa Jeshi la Polisi Songwe
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Theopista Mallya amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto vimepungua mkoani Songwe kutokana na elimu na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Jeshi la Polisi na wadau wwngine katika kuifikia jamii.
Kamanda Mallya aliyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa Ibada ya Jumapili na kutoa elimu ya madhara ya ukatili kwa waumini wa kanisa la Kisima cha Uponyaji mjini Tunduma 14 Januari 2024.
Kamanda Mallya aliongeza kwa kusema kuwa, dalili za kuonyesha kupungua kwa vitendo hivyo Inatokana na kupungua kuripotiwa kwa kesi za vitendo vya ukatili ambazo zina ripotiwa Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na Jamii kutoa taarifa katika vituo vya Polisi Mkoa wa Songwe pindi tu ukatili unapotokea au kutaka kutokea jambo ambalo linaonesha kuwa, elimu imefika kwa jamii.
“Nasema hali ni nzuri kwasababu matukio ya ukatili ikiwemo ya ulawiti yamepungua kwa kiasi kikubwa lakini pia tunapokutana na watu hivi tunaacha namba za simu kwa wachungaji na waumini kwa lengo la kutoa taarifa kwa tukio lolote linapotokea kwenye mtaa wowote tunapata taarifa” Alisema Kamanda Mallya.
Aliendelea kusema kuwa, “imeonekana elimu ni muhimu kwasababu tumekuwa na mialiko mingi ya kwenda kukutana na waamini wa dini zote kwa ajili ya kwenda kutoa elimu na kuwapa ufahamu namna ya kupambana na wahalifu na uhalifu”.
Matukio ya ukatili yamepungua kwasababu unaweza ukakaa kwenye Dawati la Jinsia na Watoto wiki nzima usione mtu amekuja kuripoti na unaweza kukaa mwezi mzima ukapata tukio moja kwa hiyo inaonesha watu wameshajitambua wameelewa ukifanyiwa kitu gani ni ukatili kwa hiyo wanatoa taarifa ambazo zinapelekea tunachukua hatua na matukio yanaendelea kupungua, alisema.
Aidha, Kamanda Mallya aliwaasa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuendelea kuchukua hatua kutokomeza matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ya Ulawiti na Ubakaji ambayo bado yapo kwa uchache wake kwenye Jamii.