Na Sophia Kingimali.
Mamlaka ya udhibiti usafiri Ardhini(LATRA) Imeyafungulia mabasi 35 ya kampuni ya Kilimanjaro kuendelea na safari zake baada ya kukidhi vigezo walivyowekewa ikiwemo kuunganisha mfumo wake wa tiketi mtandao na mfumo wa mamlaka ya mapato Tanzania.
Akizungumza leo januari 14, 2024 Jijini Dar es Salaam baada ya kutoa tamko hilo Mkurugenzi Mkuu wa LATRA Habibu Suluo amesema hatua hiyo ya kuyafungulia imekuja baada ya kampuni kukamilisha maelekezo na kuwasilisha maombi ya kurejesha huduma.
“LATRA kwa kushirikiana na jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani pamoja na kituo cha kuhifadhi kumbukumbu(NIDC) imehakiki mfumo wa tiketi mtandao wa Kilimanjaro Truck Company Limited nauli zilizoingizwa kwenye mfumo na ubora wa mabasi na madaraja vinaendana”amesema Suluo.
Sambamba na hayo Suluo amewataka watoa huduma wote wa mabasi yaendayo mkoani kuhakikisha wanabandika stika za madaraja kwenye mabasi yao kwani ni lazima kufanya hivyo na stika zote zinatolewa na serikali bure.
Kwa upande wake mwanasheria wa kampuni hiyo Dickson Ngowi ameishukuru LATRA kwa kusimamia sheria huku akiwataka kuendelea kufanya hivyo kwa kila kampuni ambayo inaenda kinyume na sheria za usafirishaji ili kuendelea kuboresha sekta hiyo.
Nae Mratibu Mwandamizi wa polisi Salumu Morimori akimuwakilisha kamanda mkuu wa kikosi cha usalama barabarani amewataka kampuni za usafirishaji kuzingatia sheria ili kuweza kuwasafirisha abiria salama.
“Watoa huduma wote wanapaswa kutii sheria ni imani yangu kupitia kikao hiki maelekezo ya mamlaka yatasimamiwa na mabadiliko makubwa yatakuwepo”amesema kamanda Morimori.
LATRA ilisitisha leseni na ratiba za mabasi 35 ya kilimanjaro kuanzia januari 8,2024 ambapo hatua hiyo ilikuja baada ya ukiukwaji wa masharti ya leseni uliofanywa na mtoa huduma bila kutumia mfumo wa tiketi mtandao lakini pia kutoza nauli zaidi ya viwango vilivyoidhinishwa ma LATRA.