Na Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa.
HARAKATI za kila siku anazofanya binadamu zina lengo la kuboresha maisha yake na kujiletea maendeleo kwa ujumla. Mkulima shambani, mvuvi baharini, daktari wodini, bodaboda barabarani, mwanafunzi shuleni na wengine wengi, wanafanya juhudi kubwa za kutekeleza majukumu yao ili maisha yaende na hivyo kuchangia maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla.
Maendeleo yenye tija ni yale yanayogusa maisha ya watu. Maendeleo yasiyogusa maisha ya watu hayana umuhimu kwa watu. Maendeleo ya watu yanapaswa kutangulia kabla ya kuelekea kwenye maendeleo ya vitu. Maisha ya watu yakiwa bora, hata maendeleo ya vitu yakifuata yatakuwa na maana kubwa.
Ajenda ya wananchi popote pale iwe ni nchi zilizoendelea au nchi zinazoendelea kama Tanzania ni kupata maendeleo yanayogusa nyanja zote za maisha yao, iwe kisiasa, kijamii na kiuchumi. Kiufupi, wananchi wanataka maendeleo tena maendeleo yanayogusa maisha yao moja kwa moja.
Baadhi ya vitabu vya dini vinaonesha kwamba mtu anayependeza sana mbele za Mungu ni yule ambaye jamii kubwa inanufaika naye. Kwa muktadha huo, viongozi wa ngazi mbalimbali, wana nafasi kubwa ya kupendwa na Mungu kwa sababu wana kila sababu ya kuwanufaisha watu wengi.
Mwalimu Nyerere alipata kusema kwamba ukiwa kiongozi mahala, basi ujue madhila ya watu unaowaongoza ni mzigo wako. Ni viongozi wangapi wanatilia maanani hilo?
Viongozi na wananchi kwa pamoja ni wadau muhimu wa kufanikisha azma ya kupata maendeleo. Pande hizi mbili zinapaswa kushirikiana kikamilifu ili kufanikisha na kurahisisha mzunguko wa kasi wa gurudumu la maendeleo. Mipango ya maendeleo inapaswa kuratibiwa kwa karibu kupitia ushirikiano baina ya viongozi na wananchi.
Viongozi hasa wa kuchaguliwa huwa wanaomba ridhaa kutoka kwa wananchi kupitia utaratibu uliopo wa uchaguzi, uwe uchaguzi wa serikali za mitaa au uchaguzi mkuu. Katika kipindi cha uchaguzi, wagombea, hujinadi kupitia majukwaa wakiomba ridhaa ya kuongoza (kwa maana ya kuwawakilisha) kwa kipindi cha miaka mitano na kuahidi mambo mbalimbali ambayo kama wakipata ridhaa watayatekeleza ili kuleta ustawi wa maisha ya wananchi. Ni wawakilishi kwa sababu haiwezekani wananchi wote tukaenda Bungeni ili kuisimamia serikali na kutunga sheria. Tunatuma wawakilishi.
Hata viongozi wa kuteuliwa, wana dhima ileile ya kumwakilisha rais tuliyemchagua ama kiongozi aliyewateua kwetu na hivyo bado matatizo ya wananchi ni mzigo wao.
Deni kubwa walilonalo viongozi baada ya kupata dhamana ya kuongoza ni kutekeleza ahadi zao ambazo huwa zina lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo utakuwa na tija kwa wananchi endapo wananchi hao watashirikishwa kikamilifu na viongozi hawa kwa kutoa maoni yao kuhusu nini wangependa kitangulie kutekelezwa katika maeneo yao. Hivyo basi, ni muhimu sana wananchi wakashirikishwa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ili miradi hiyo ya maendeleo iwe na tija kubwa katika maisha ya kila siku ya wananchi.
Akizungumza na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wananchi wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi baada ya kuzindua Shina la Chama, Majengo Sokoni, Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametoa rai kwamba mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ya wananchi, ni vyema wananchi washirikishwe kwanza na yatokane na wananchi wenyewe.
Kinana alitoa mfano hai juu ya hoja yake ya kuwashirikisha wananchi kwenye ajenda ya maendeleo. Alieleza kuwa alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM akiwa na Nape Nnauye (aliyekuwa Katibu Mwenezi wakati huo) walikwenda wilayani Ngorongoro ambako walifanya mkutano mkubwa.
“Tulipokuwa pale, ukitazama pale kwa mimi ungeniuliza ningesema wale wananchi wanahitaji maji, lakini tulipowauliza wenyeji, wakasema tatizo lao si maji bali ni mtandao wa simu. Unaweza ukaona wewe unakwenda mahali ukifikiri shida ya watu ni shule, ni maji kumbe shida yao ni jambo lingine kabisa ndiyo maana ni lazima tuwashirikishe wananchi,” alisema Kinana.
Hii pia imenikumbusha kwamba kuliwahi kuwepo matukio ya baadhi ya halmshauri kujenga masoko na kisha yakabaki kama magofu kwa sababu wananchi waliyatekeleza, wakawa wanaendelea kutumia ‘masoko mjinga’. Hii yote ilitokana na wakubwa wa halmashauri ‘kufikiri kwa niaba ya wananchi’ badala ya kuwashirikisha ni wapi mahala sahihi pa kujenga soko.
Mfano hai ni pale Musoma Mjini ambapo Halmashauri ya Mji (wakati huo, miaka ya 1980) ilijifunga kibwebwe kuwaamlia wananchi kujenga soko la kisasa na kubwa katika eneo la Kamunyonge lakini wananchi walilitelekeza na kufanya manunuzi yao kwenye soko mithili ya genge wakati huo la Nyasho ambalo lilikuja kuendelezwa baadaye!
Kutokana na viongozi kuwa na jukumu la kuboresha maisha ya wananchi wao, juhudi zao zitaleta matunda na hata kuwa na uhakika wa kuchaguliwa tena endapo viongozi wataibua na kutekeleza miradi inayogusa maisha ya watu. Vivyo hivyo kwa viongozi wa kuteuliwa, mamlaka za uteuzi kila mara zitawafikria pale watakapokuwa wanafanyia kazi kwanza matakwa na maslahi ya wananchi.
Hata kama viongozi ni wakazi wa maeneo hayo, ni muhimu wawashirikishe wananchi wao juu ya miradi gani itangulie kutekelezwa na iwekwe wapi ili miradi hiyo iwe na tija kwa wananchi kwa wakati huo.
Si jambo lenye afya kwa kiongozi kudhani kuwa anajua kila kitu, hivyo kuchukua jukumu la kupigia debe utekelezwaji wa miradi ya maendeleo kadri anavyofikiria yeye bila kupata ushauri na pengine ridhaa kutoka kwa wananchi wake. Changamoto zinaweza kuwa nyingi katika eneo fulani la utawala; mathalani, kijiji hakina zahanati, shule, maji, umeme, stendi na kadhalika.
Ikiwa hakuna fedha za kutosha za kumaliza changamoto hizi kwa wakati mmoja, ni muhmu kwa viongozi kuwashirikisha wananchi juu ya mradi gani uanze kutekelezwa kutokana na uzito wake kwao.
“Katika kuamua mambo yanayohusu maisha yao, tusichukue amana ya kuwafikiria, tusichukue mamlaka ya kuwaamulia. Ni vizuri tukae na wananchi tuzungumze nao ili watuambie kitu gani wanakihitaji kwa wakati gani na kwa sababu gani,” amesema Kinana.
Mwangwi wa hili alilolisema Kinana ni vyema ufike hadi bungeni kwa maana ya wawakilishi hao wa wananchi kufanya mikutano kwa wingi majimboni ili wawe wakipeleka mawazo ya wapiga kura na si ‘kujiwakilisha’ wenyewe kwa kusema wanayofikiri!
Vivyo hivyo madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi wa kata zao wanapaswa pia kufanya mikutano mingi na wananchi na kupeleka mawazo yao kwenye vikao vya kupanga maendeleo ya halmashauri. Kwenye mikutano hii, madiwani na hata wabunge wasijitishwe jukumu la kuhutubia wananchi bali wawaache wananchi kuwa wazungumzaji wakubwa ili kusikia sauti zao, kero zao, hoja zao na hata makemeo yao.
Muda umebaki mfupi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu. Unaweza kufanya uchunguzi na kugundua kwamba ni wabunge wachache ambao wamefanya mikutano ya kutosha na wananchi na kusikia kero na mawazo yao. Wapo wabunge ambao wanaonekana tu wakati wa uchaguzi baada ya hapo wanapotea. La kujiuliza, wabunge kama hawa wanamwakilisha nani?
Ni muhimu kwa viongozi wote kuzingatia hili alilosisitiza Kinana juu ya maendeleo ya wananchi. Hata tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, ni muhimu kwa wagombea kujua kile wananchi wanataka. Kwa kufanya yale wananchi wanataka, hayo ndiyo maendeleo halisi na ndipo kwenye utatuzi wa kero za wananchi na hatimaye kufikia maendeleo ya kweli ya nchi yetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Wapiga kura pia tusichague viongozi ‘wanaojiwakilisha’ wenyewe, wabinafsi na wasiokaribu na wananchi. Kama ni hundi, basi tunaenda kupewa hundi nyeupe tuandike fedha tunazotaka. Tuwe makini tutakapokuwa tunajaza hiyo hundi. Binafsi nimemuelewa sana Kinana, wewe je?
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa- Dodoma. Mawasiliano yake ni 0620 800 462.