Na. WAF – Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa rai kwa wananchi kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuifanya miili yao kuwa imara na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Waziri Ummy ametoa wito huo leo Januari 13, 2024 alipokuwa katika moja ya maduka ya vifaa vya michezo la ‘Just fit’ lililopo Jijini Dar es Salaam.
“Kumekuwa na ongezeko la kasi magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari na Shinikizo la Juu la Damu (Presha) Watanzania tunatakiwa kuzingatia mtindo wetu wa maisha kwa kupunguza mafuta na chumvi katika vyakula pamoja na ufanyaji wa mazoezi.” Amesema Waziri Ummy.
Amesema, Mwaka 2022 ugonjwa wa Kisukari ulichangia asilimia 1.6 ya magonjwa yanayowasumbua Watanzania ambapo kwa Mwaka 2023 imepanda mara Mbili zaidi kutoka asilimia 1.6 mpaka 2.5.
“Ugonjwa wa Shinikizo la Juu la Damu Mwaka 2022 ilichangia kwa asilimia 2.7 ya magonjwa yanayowasumbua Watanzania huku Mwaka 2023 ikipanda mara Mbili yake na kufikia asilimia 5.6 na kufanya kuwa ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayotokana na mitindo mibaya ya maisha tunayoishi ikiwemo ya kutofanya mazoezi.” Amefafanua Waziri Ummy.