Na Dk. Reubeni Lumbagala.
Mmomonyoko wa maadili ni moja ya tatizo linaloisumbua dunia na Tanzania ikiwemo. Mmomonyoko huu umeonekana dhahiri kuanzia kwa watoto, vijana, watu wazima hadi kwa wazee. Kutokana na umuhimu wa kujenga jamii yenye maadili na mienendo mizuri, ni lazima kama nchi kuweka mikakati ili kujenga jamii na taifa lenye maadili kama ilivyokuwa zamani.
Serikali kama mdau muhimu katika ujenzi wa maadili katika jamii, inashirikisha wadau wengine ili kuunganisha nguvu ya pamoja kufanikisha azma ya kujenga maadili bora katika jamii.
Moja ya eneo ambalo kama taifa tunapaswa kuwa na sauti moja kuanzia kwa mwananchi mmoja mmoja, familia, jamii na taifa kwa ujumla ni kupinga ndoa za jinsia moja (homosexual marriage).
Ndoa za jinsia moja kuanzia kwenye imani za dini, mila, desturi na tamaduni zetu ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo na wala halihitaji mjadala mrefu, ila kutokana na ushawishi na msukumo toka mataifa ya kimagharibi, hatuna budi kama taifa kuendelea kupaza sauti na kueleza bayana msimamo wetu kama taifa.
Hivi karibuni, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Geita, Flavian Kassala alisema hayuko tayari kubarki ndoa ya jinsia moja kwa sababu ni kinyume na maagano ya Mungu ya kutaka binadamu wakazaliane na kuendeleza vizazi ulimwenguni. Akihubiri katika misa ya kitaifa ya Krisimasi iliyofanyika katika kanisa la Bikira Maria Malkia wa Amani, Askofu Kassala alisisitiza kuwa ni bora abariki jiwe likajengee nyumba lakini si kubariki watu wa jinsia moja wanaotaka kufunga ndoa ndani ya kanisa hilo. _“Binadamu amemuacha Mungu na kufanya mambo yaliyokatazwa. Binadamu ameukataa uumbaji na kuendeleza uumbaji na sasa wanafanya mambo machafu yanayomchukiza Mungu, wamekuwa wakiharibu vizazi kwa kutoa mimba na sasa wanataka kubariki na mapenzi ya jinsia moja. Kwangu bora nibariki jiwe lakini sio uchafu huo.”_ amesema Askofu Kassala.
Nimpongeze Askofu Kassala ambaye ameamua kuusema msimamo wake waziwazi kwani viongozi wa dini wanao ushawishi mkubwa katika jamii katika kufanikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kijamii na ya kiserikali. Kutokana na umuhimu wa viongozi wa dini, ndiyo maana mara kwa mara serikali imekuwa ikiwashirikisha kwenye mipango na mikakati ya nchi ili kurahisisha utekelezaji wake.
Msimamo wa Askofu Kassala unaunga mkono juhudi za wadau zenye lengo la kujenga maadili mazuri katika nchi yetu. Hatuwezi kufanikiwa kujenga maadili huku tukiwa tunaruhusu na kukumbatia ndoa za jinsia moja.
Namkumbuka mwalimu wangu wa somo la Uraia (Civics) kidato cha kwanza katika mada ya Maisha ya Ndoa (Marriage Life) alitufundisha tafsiri (definition) ya neno “ndoa” kuwa ni muunganiko wa mwanaume na mwanamke kama mume na mke. Hivyo, ndoa inahusisha jinsia mbili tofauti yaani mwanamme na mwanamke, watu hawa huungana na kuwa familia moja; mwanaume anakuwa mume (husband) na mwanamke anakuwa mke (wife).
Hata katika vitabu vya dini vinaeleza Mwenyezi Mungu ndiye muasisi wa taasisi ya ndoa. Katika kuweka msingi mzuri wa ndoa, Mungu aliwaumba Adamu (mwanamme) na Hawa (mwanamke), akawabariki, akawaagiza waende wakaitawale dunia na kuzaliana.
Maandiko Matakatifu katika Biblia, kitabu cha Mwanzo 1:28, Biblia inasema _“Mungu akawabariki, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”_
Kwahiyo, msingi wa Mungu katika suala la ndoa ni lazima ndoa ihusishe mwanamme na mwanamke, na katika jinsia hizi mbili tofauti, ndipo kwenye kuzaliana (reproduction). Kama taifa, tuna kila sababu ya kulaani na kupaza sauti kukemea ndoa za jinsia moja ili kuendeleza mipango mizuri ya ujenzi wa maadili kwa mustakabali mwema wa nchi yetu.
Viongozi wa dini zote, wanaharakati, asasi za kiraia na kila mpenda maendeleo na maadili wanayo nafasi ya kukemea ndoa za jinsia moja kwa mdomo mpana kabisa ili msimamo huu ueleweke vyema kuanzia ndani ya nchi hadi nje ya nchi yetu.
Mwaka 2011, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alisema nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja. Katika kutoa msimamo wa serikali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa wakati huo, Benard Membe ambaye kwa sasa ni marehemu alisema _“Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa.”_
Nitoe rai kwa serikali yetu kuendeleza msimamo huu mzuri. Zaidi sana, kama nchi tuendelee kutumia raslimali zetu vizuri ili kupitia raslimali hizo tuweze kupata fedha za kutosha za kuendesha nchi yetu kwa kufanikisha miradi ya maendeleo na matumizi mengine ili kuepukana na kadhia ya kuomba misaada ambayo wakati mwingine inakuja na masharti ya ndoa ya jinsia moja.
*Dk. Reubeni Lumbagala*
*Mwalimu Shule ya Sekondari Mlali,*
*Wilaya ya Kongwa- Dodoma.*
*Mawasiliano yake ni (+255) 620 800 462.*