Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akikabidhi vifaa tiba kwa wabunge wa majimbo 10 ya mkoa wa Dar es Salaam leo katika hgala la Bohari ya Dawa MSD Mabibo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akizungumza wakati alipokabidhi vifaa tiba kwa wabunge wa majimbo 10 ya mkoa wa Dar es Salaam leo katika hgala la Bohari ya Dawa MSD Mabibo jijini Dar es Salaam.
…………………………….
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hususani huduma ya mama na mtoto lengo ni kupunguza vifo vitonavyo na uzazi pingamizi.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alipokuwa akiwakabidhi wabunge wa majimbo 10 ya mkoa wa Dar es Salaam, vifaa tiba vyenye thamani ya sh. Milioni 691 vilovyotolewa na serikali kwa majimbo hayo.
Amesema vifaa hivyo ni miongoni mwa vifaa vilivyozinduliwa wiki iliyopita na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa nchi nzima vikiwa na gharima ya sh. bilioni 14.9 kwa majimbo na halmashauri 214 nchi nzima.
Chalamila amesema Rais Dk. Samia amedhamiria kumaliza vifo vinavyosababishwa na uzazi, hivyo uwekezaji mkubwa unaendelea kufanyika katika sekta hiyo.
Alisema mkoa huo umepewa zaidi ya sh. bilioni 52 kuimarisha sekta ya afya na kwamba wanaboresha kujenga vituo vipya vya afya na kuiwezesha MSD kusambaza vifaa tiba vya kisasa katika vituo vya umma vilivyo tayari kutoa huduma kwa wananchi.
“Mbali na kupokea vifaa hivi jiji hili limenufaika na uwekezaji huo mkubwa unaohusisha uboreshoji wa miundombinu, vifaa, utoaji huduma huku utekelezaji wa miradi mingine mipya ukiendelea,” alisema.
Chalamila ameeleza kuwa uwekezaji huo unaofanywa na serikali katika sekta ya afya umeleta mapinduzi makubwa ya utoaji huduma hivyo anatoa wito kwa jamii kuchangamkia fursa ya bima ya afya kwa wote ili kupunguza gharama za matibabu.
“Hatua hiyo ya bima ya afya kwa wote hususani kwa wananchi wa hali ya chini itawaondolea mzigo wa kutelekeza maiti kutokana na kukimbia gharama.
“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi tuhakikishe tunawatia moyo watoa huduma wetu, wanafanya kazi kubwa zipo changamoto lakini na mazuri yapo kazi zao ni ngumu sisi hatuwezi, kila mmoja na kazi yake kuokoa maisha ya mtu au kufanya kazi pale chumba cha kuhifadhia maiti si jambo dogo,”alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai amesema serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 14.9 kununua vifaa hivi kwa ajili ya nchi nzima na MSD ndiyo imenunua na itavisambaza kwa majimbo hayo 214 nchi nzima.
Naye Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu, Akizungumza katika hafla hiyo alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa wabunge wote 528, lengo likiwa kuboresha sekta ya afya nchini.
“Rais Dk. Samia mpaka Novemba mwaka 2023 peke yake amewekeza zaidi ya trilion sita katika afya.Mwezi uliopita kila Mbunge amekabidhiwa gari moja na wabunge wako 528 wamepatiwa gari la kubeba wagonjwa.
” Rais Samia ametoa magari hayo kwa wabunge kwa lengo likiwa kuhakikisha vifo vya mama na watoto vinapungua, “amesema Naibu Spika Zungu huku akiwatumia nafasi hiyo kuwapongeza watoa huduma za afya.
” Niwapongeze wauguzi na madaktari kwa kuendelea kutoa huduma.Kwa kipekee nimpongeze Mganga wa wa Jiji la Dar es Salaam Dk.Mohamed Mang’unya ambaye amefanya maboresho makubwa katika huduma za afya katika Jiji la Dar es Salaam katika kipindi kifupi.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai, ameisema vifaa hivyo ni sehemu ya mkakatibwa serikali kukabiliana na changamoto ya vifo vya mama na mtoto.
Amesema mkakati wa kugawa vifaa hivyo ulizinduliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambapo serikali imetumia sh bilioni 14 kununua vifaa hivyo ambavuo vitasambazwa katika halmashauri za wilaya zote nchini.
Kwa mujibu wa Tukai, kwa Dar es Salaam vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 700 vitagawiwa katika zahanati na vituko vya afya vyote mkoani humo.
Akitoa salamu za shukran kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, alieleza kwamba vifaa hivyo vitaleta ahueni kubwa kwa wananchi hususan kuepuka vifo vya mama na mtoto.
“Tunashukuru serikali kupitia MSD kwa kutuletea vifaa hivi. Haya ni mageuzi makubwa ambayo yatasaidia kuimarisha afya ya wananchi wa Mkoa huo,” alisema.