TAREHE: 11 JANUARI, 2024
Assalamu Aleikum
Ndugu Wananchi,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutupa uhai na afya njema na kutuwezesha kufikia siku ya leo, tukiwa katika mkesha wa Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi, tuna wajibu pia wa kuwakumbuka Waasisi wetu chini ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, viongozi na wananchi wenzetu waliotangulia mbele ya haki, ambao waliitumikia nchi yetu kwa moyo, ujasiri na uzalendo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze pema peponi. Na wale walio hai, Mola awape afya njema na umri mrefu tuendelee kushirikiana nao katika kujiletea maendeleo.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa kujitokeza kwa wingi katika matukio mbali mbali yaliyoandaliwa katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi. Ni matarajio yangu kuwa na kesho siku ya kilele, mtajitokeza tena kwa wingi katika uwanja wa Amani ili kufanikisha sherehe zetu.
Tofauti na mara nyengine zote safari hii sherehe yetu itafanyika mchana ili kutoa fursa kwa waumini wa Dini ya Kiislamu kupata nafasi ya kutekeleza ibada ya sala ya Ijumaa.
Mara hii tulikuwa na miradi iliyozinduliwa 65 na miradi 45 imeekewa mawe ya msingi. Hii ni idadi kubwa sana ya miradi ambayo hatujawahi kuifikia katika kipindi cha sherehe kama hizi. Vile vile, tumeandaa matukio makuu maalum na sherehe za aina yake ambazo kilele chake kitafanyika katika uwanja wa Amani. Kadhalika, tuna ujio wa baadhi ya wageni mashuhuri tutakao kuwa nao katika maadhimisho yetu haya.
Ndugu Wananchi,
Mafanikio tuliyoyapata miaka 60 tokea Mapinduzi ya mwaka 1964, yametokana na uongozi thabiti wa Waasisi wa Taifa letu na viongozi wote wa awamu zilizotangulia kwa ushirikiano na uzalendo kati yao na nyinyi wananchi. Serikali ya Awamu ya Nane tokea ilipoingia madarakani miaka mitatu iliopita, inayaendeleza mafanikio hayo na kufanya juhudi za kuhakikisha Zanzibar inazidi kupiga hatua za maendeleo katika sekta zote na kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
Nilipoingia madarakani mwaka 2020, nilieleza dhamira yangu ya kuunganisha Malengo ya Mapinduzi na uchumi, nikilenga kuimarisha jitihada za kukuza uchumi ili kustawisha maisha ya wananchi wa Zanzibar. Lengo la Serikali ninayoiongoza ni kuendeleza umoja, mshikamano na maridhiano ili kila Mzanzibari apate fursa ya kuchangia maendeleo na kunufaika na matunda ya Mapinduzi kwa misingi ya usawa. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika kuifikia dhamira hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane.
Ndugu Wananchi,
Katika kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, tunafurahia mafanikio tuliyo nayo katika kudumisha na kuendeleza Amani, Umoja na Mshikamano. Misingi hii muhimu imetuwezesha kupiga hatua katika maendeleo ya uchumi, ujenzi wa miundombinu, kuimarisha huduma za jamii, biashara na kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Natoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM kwa ushirikiano mkubwa anaonipa. Vile vile, nawashukuru viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na asasi za kijamii, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote kwa kunipa ushirikiano na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini kwa faida ya kizazi cha sasa cha baadae. Nawahakikishia wananchi na wageni wote wanaotutembelea kwamba nchi yetu ipo salama na kwamba Serikali zetu zote mbili zitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria katika kulinda amani, utulivu na usalama wa mali zao.
Ndugu Wananchi.
Katika hotuba yangu hii ya kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na miaka mitatu Serikali ya Awamu ya Nane, nitaelezea kwa muhtasari mafanikio, changamoto na mipango yetu ya utekelezaji wa majukumu ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. Serikali iliwapa jukumu mawaziri wote kuelezea kwa kina kupitia vyombo vya habari, mafanikio, changamoto na mipango ya kila wizara ili wananchi wafahamu utendaji wa Serikali yao. Nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kutekeleza kwa mafanikio agizo hilo.
Ndugu Wananchi
Juhudi zinazochukuliwa na Serikali zimewezesha uchumi wetu kuzidi kuimarika. Thamani ya Pato halisi la Taifa (GDP at constant Price) imeongezeka kutoka TZS. Trilioni 3.116 kwa mwaka 2020 na kufikia thamani ya TZS. Trilioni 3.499 mwaka 2022. Vile vile ukusanyaji wa mapato umeongezeka kufikia TZS. Trilioni 1.4 mwaka 2022/2023 kutoka TZS. Bilioni 790.48 mwaka 2020/2021, sawa na ongezeko la asimilia 56.4. Aidha, kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2022 imefikia wastani wa asilimi 6.8 ikilinganishwa na asilimia 1.3 ya mwaka 2020. Kiwango cha ukuaji wa uchumi wetu ni kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea.
Kukuwa kwa uchumi wetu kumetokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwa kutekelezwa miradi ya Maendeleo ya kipaumbele ikiwemo miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, huduma za maji safi na salama, uimarishaji wa huduma za nishati ya umeme, masoko na kuimarika kwa sekta ya huduma kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii. Pato la mtu binafsi nalo limeongezeka kutoka USD 1,099 sawa na TZS. Milioni 2.5 mwaka 2020 na kufikia USD 1,230 sawa na TZS. Milioni 2.8 mwaka 2022. Aidha, jitihada zilizochukuliwa na Serikali zimeweza kudhibiti kasi ya mfumko wa bei na kuendelea kuwa katika tarakimu moja. Kwa mwaka 2023 mfumko wa bei ulikuwa ni wa wastani wa asilimia 6.8 hali inayomuhakikishia mwananchi kupata mahitaji ya lazima.
Ndugu Wananchi
Serikali za awamu zote zilizopita baada ya Mapinduzi zilichukuwa juhudi za uwekezaji kwa ujenzi wa miundombinu, majengo ya Ofisi, huduma na maakazi, viwanda na kuwakaribisha wawekezaji kuzitumia fursa na rasilimali zilizopo nchini katika kuchangia ukuaji wa uchumi. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na Miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane tumeshuhudia mafanikio makubwa katika jitihada zetu za kuvutia wawekezaji. Kasi ya uwekezaji nchini imeongezeka ambapo jumla ya miradi 296 yenye thamani ya USD. Bilioni 4.5 imeidhinishwa. Miradi hiyo inakadiriwa kutoa ajira zipatazo 17,479 ikihusisha uwekezaji katika visiwa vidogo 16 wenye thamani ya USD. Milioni 377.5, ujenzi wa hoteli za kitalii 112, viwanda 36, biashara ya majengo 56 na miradi mingine ya kiuchumi.
Mafanikio haya yametokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ikiwemo uimarishaji wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambapo sasa wawekezaji wanaweza kupata huduma zote za uwekezaji katika kituo kimoja (One Stop Center) ndani ya masaa 24. Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa zilizopo katika maeneo ya bandari jumuishi ya Mangapwani na ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, maji na umeme katika maeneo ya uwekezaji.
Ndugu Wananchi
Kwa kuzingatia umuhimu wa biashara kwa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbali mbali kuimarisha mazingira ya ufanyaji wa biashara. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, sekta ya biashara ya usafirishaji na uingizaji bidhaa kwa ujumla inaendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022 Zanzibar imefanya biashara yenye thamani ya TZS. Trilioni 1.4 ukilinganisha na TZS. Bilioni 913.1 kwa mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 57.6.
Zanzibar imesafirisha nje bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 180.4 kwa mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 174.7 ikilinganishwa na usafirishaji wa bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 65.7 kwa mwaka 2020. Kwa mwaka 2022, Zanzibar imesafirisha tani 6,452.8 za karafuu yenye thamani ya TZS. Bilioni 118.3 ikilinganishwa na tani 3,506.8 zilizosafirishwa mwaka 2020, zenye thamani ya TZS. Bilioni 38.37 sawa na ongezeka la fedha la asilimia 208.1. Kwa upande wa mwani Zanzibar imesafirisha Tani 13,972.5 zenye thamani ya TZS. Bilioni 16.0 kwa mwaka 2022 ukilinganisha na tani 11,382.6 wenye thamani ya TZS. Bilioni 11.7 kwa mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 36.8.
Kuhusu biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, mwaka 2022, Zanzibar imesafirisha bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 37.64 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 15.03 zilizosafirishwa mwaka 2020. Kwa upande wa uagiziaji katika kipindi cha mwaka 2022, Zanzibar imeagizia bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 375.80 kutoka Tanzania Bara ikilinganishwa na uagiziaji wa bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 243.81 kwa mwaka 2020.
Ndugu Wananchi
Kwa madhumuni ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi, Serikali imechukua hatua za kuimarisha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kupambana na umaskini. Serikali imepata mafanikio katika uimarishaji wa vikundi vya ushirika ambapo jumla ya vikundi 1,546 vya ushirika vimesajiliwa. Idadi hiyo imewezesha kufikia vikundi 3,662 vya ushirika vilivyosajiliwa nchini. Kupitia fedha za Ahuweni ya UVIKO – 19, Serikali imetoa jumla ya TZS Bilioni 60. Fedha hizi zinajumuisha TZS. Bilioni 29 zilizotolewa kwa ajili ya sekta za Uchumi wa Buluu, TZS Bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi wa Masoko na TZS. Bilioni 15 kwa ajili ya Programu ya Inuka yenye lengo la kutoa mikopo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara.
Programu ya Inuka ilianza na mtaji wa TZS. Bilioni 15.0. Hadi sasa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 22.4 imeshatolewa kupitia programu hii. Ongezeko la thamani la mikopo hiyo limetokana na fedha za marejesho ambazo zinaendelea kutolewa mikopo mipya (Revolving Fund). Mikopo hiyo imewezesha kuzalisha ajira za moja kwa moja (direct employment) kwa Wananchi 43,360. Aidha, programu ya Khalifa Fund imetoa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 2.10 kwa miradi 18 ya wananchi. Kadhalika, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi jumla ya TZS Milioni 852.17 zimetolewa kwa wananchi.
Kupitia Programu ya Mikopo kwa Makundi Maalum, hadi sasa Serikali imefanikiwa kukusanya jumla ya TZS. Bilioni 1.9 kutoka Halmashauri za Wilaya. Fedha hizi zimelengwa kutumika kwa ajili ya kutoa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.
Ndugu Wananchi
Katika kuhakikisha suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi linapata mafanikio, Ujenzi wa miundombinu umezingatiwa ambapo vituo viwili vya kusarifu asali vinavyogharimu TZS. Milioni 529.29 vimejengwa Unguja na Pemba. Aidha, ujenzi wa kituo cha mafunzo ya usarifu mazao utakaogharimu USD. Milioni 1.29 umeanza kwa matayarisho ya awali.
Kadhalika, wajasiriamali wamepatiwa vifaa vya uzalishaji wa asali ikiwemo Mizinga yenye thamani ya TZS. Milioni 459.98, vifaa vya nyuki vyenye thamani ya TZS Milioni 194.34, Vifaa vya maabara vyenye thamani ya TZS Milioni 34.40 na Pikipiki 9 zenye thamani ya TZS Milioni 35.91.
Serikali pia, imeanzisha Wakala ili kuimarisha usimamizi wa utoaji wa Mikopo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB. Vile vile, mafunzo yanaendelea kutolewa kwa wajasiriamali ili kuwajengea uwezo zaidi ambapo wajasiriamali 2,225 wameshapatiwa mafunzo hayo kwa kipindi hiki.
Jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi cha miaka mitatu, zimewezesha kupatikana kwa jumla ya ajira 187,651. Idadi hiyo imevuka malengo ya ajira 180,000 kwa miaka mitatu, sawa na ongezeko la asilimia 104.3
Ndugu Wananchi,
Serikali imezingatia haja ya kuwapatia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo mazingira bora ya kufanyia kazi zao. Ujenzi wa vituo 14 vya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo vilivyogharimu TZS Bilioni 16.03 vimejengwa Unguja na Pemba ambapo baadhi yake vimeanza kutumika. Vile vile, jumla ya masoko 10 yamejengwa kwenye Wilaya 6 yenye thamani ya TZS. Bilioni 4.93. Aidha, ujenzi wa masoko makubwa ya kisasa unaogharimu TZS. Bilioni 102.41 unaendelea katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini. Ni matumaini yetu kuwa masoko haya yatakamilika mwaka huu 2024 na kuanza kutumika.
Hadi kufikia tarehe 20 Disemba, 2023 jumla ya wajasiriamali 7,227 wamesajiliwa na kupatiwa vitambulisho katika Serikali za Mitaa Unguja na Pemba. Vile vile, mafanikio yamepatikana katika ukusanyaji wa mapato kwa Serikali za Mitaa, ambapo ukusanyaji wa mapato umeongezeka kwa asilimia 26 kutoka TZS Bilioni 15.24 zilizokusanywa mwaka 2020 hadi kufikia TZS Bilioni 20.71 mwaka 2023.
Ndugu Wananchi
Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Nane imekuja na dhana ya Uchumi wa Buluu unaotilia mkazo matumizi ya rasilimali za bahari na shughuli nyengine za kiuchumi zinazohusiana na bahari. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio yamepatikana katika sekta kuu za uchumi wa buluu ambazo ni utalii, uvuvi na kilimo cha mwani, bandari, mafuta na gesi asilia na biashara inayohusiana na usafiri wa majini.
Kuhusu utalii, ni sekta iliyopewa mazingatio katika kuleta fedha za kigeni na ajira katika awamu zote za Serikali baada ya Mapinduzi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi. Juhudi mbali mbali zimefanywa na viongozi wa awamu zilizopita ili kuongeza michango ya sekta hii katika Pato la Taifa pamoja na upatikanaji wa ajira. Sekta ya utalii imeendelea kupata mafanikio makubwa. Idadi ya watalii imeongezeka kwa asilimia 143.6, kutoka watalii 260,644 mwaka 2020 hadi 638,498 mwaka 2023. baada ya UVIKO – 19.
Miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa idadi ya watalii ni ongezeko la idadi ya ndege za kimataifa zilizotua nchini kutoka 4,253 mwaka 2020 hadi 10,548 mwaka 2022 kulikochochewa na uimarishaji wa huduma ya kiwanja chetu cha ndege cha AAKIA. Aidha, ongezeko la hoteli za daraja la juu nchini kumechangia kuimarisha sekta ya utalii kwani kumevutia kutembelewa na wageni wengi. Katika kipindi hiki, idadi ya miradi ya utalii imeongezeka kutoka 620 mwaka 2020 hadi miradi 709 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 15.
Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi, Zanzibar haikuwa na mipango madhubuti ya kuimarisha uvuvi na mazao mengine ya bahari licha ya nchi hii kubarikiwa rasilimali hiyo kila upande. Katika kipindi chote baada ya Mapinduzi, jitihada zimefanywa na Serikali kuimarisha sekta hii hasa kwa kuwashajiisha wavuvi wadogo wadogo wanaoishi pembezoni mwa mwambao wa bahari. Serikali ya Awamu ya Nane katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu, imeongeza juhudi za kuimarisha sekta ya uvuvi na kilimo cha mwani. Mafanikio yameanza kupatikana katika dhamira hiyo baada ya Serikali kuwapatia wananchi vifaa, fedha za mitaji, mafunzo na miundombinu ikiwemo ujenzi wa soko la kisasa la samaki Malindi na kiwanda cha kusarifu bidhaa za mwani Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba. Serikali pia imeanza kuvutia uwekezaji katika Mpango mkakati wa Uchumi wa Buluu ili kuwezesha kuongezeka kwa miradi ya maendeleo.
Kiwango cha uzalishaji wa samaki kwa mwaka kimeongezeka kutoka Tani 38,107 mwaka 2020 zilizokuwa na thamani ya TZS. Bilioni 205.4 hadi kufikia Tani 80,085 kwa mwaka 2023 zenye thamani ya TZS. Bilioni 569.08. Aidha, usafirishaji wa dagaa umeongezeka kufikia Tani 10,695 zenye thamani ya TZS. Bilioni 39.1 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka 2020 ambao ulikuwa Tani 3,500 zenye thamani ya TZS. Bilioni 12.3. Mafanikio hayo yamewezesha kuongezeka kwa pato la Taifa katika sekta ya uvuvi kutoka asilimia 4.5 na kufikia asilimia 6.32 mwaka 2023.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu zao la mwani, Selikali ilitoa jumla ya boti 500 pamoja na kamba na taitai kwa wakulima wa mwani 5,000. Jitihada hizi zimechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mwani kutoka tani 8,785 zenye thamani ya TZS. Bilioni 5.38 mwaka 2020 na kufikia tani 16,653 zenye thamani ya TZS. Bilioni 16.35 kwa mwaka 2023. Pia, katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la mwani, tumekamilisha ujenzi wa Kiwanda cha kusarifu mwani cha Chamanangwe Pemba kwa awamu ya kwanza. Kwa ushirikiano na wadau wetu wa maendeleo kutoka Korea, Kiwanda chengine cha pili kikubwa cha kutengeneza bidhaa za mwani kitajengwa Pemba. Vilevile, viwanda vitatu vidogo vidogo vya ujasiriamali wa wakulima wa mwani vitajengwa kwa Mikoa ya Unguja.
Kuanzishwa kwa Kampuni ya Mwani ya Serikali, kumeongeza ushindani katika ununuzi wa mwani kutoka kwa wananchi. Hali hii imesababisha kuongezeka kwa bei ya mwani. Bei ya mwani wa Spinosum imepanda kutoka TZS 600 kwa kilo hadi TZS. 1,000 kwa kilo. Mwani wa Cottonii unauzwa kwa TZS. 2,200 kwa kilo kutoka TZS. 1,000. Ahadi ya Serikali ni kufanya kila linalowezekana katika kuhakikisha bei hiyo inazidi kuongezeka ili kumpa faida zaidi mkulima.
Ndugu Wananchi,
Serikali baada ya Mapinduzi ilianza kuchukua hatua za kuimarisha huduma za bandari na usafiri wa majini kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa visiwa kama ilivyo Zanzibar na kurahisisha huduma za usafiri. Serikali, ilifanya upanuzi wa bandari zetu, ujenzi wa gati, ununuzi wa vifaa na mashine mbali mbali pamoja na ujenzi wa majengo ya Ofisi na kuhudumia abiria. Pia, Selikali ilinunua meli mpya na kuruhusu sekta binafsi kuanzisha usafiri wa boti za mwendo wa kasi kwa madhumuni ya kuimarisha usafiri wa majini.
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi jitihada za kuimarisha bandari zetu na usafiri wa majini nazo zimepata mafanikio. Kwa upande wa bandari, Serikali ilifunga mkataba na Africa Global Logistic (AGL) inayomilikiwa na kampuni ya MSC, shirika lenye kumiliki meli za usafirishaji. Kampuni hii inahusika na uendeshaji wa bandari ya Malindi kwa kipindi cha miaka mitano na imesajiliwa kwa jina la Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT). Tayari Kampuni hii imeanza kazi ya kushughulikia meli za makontena pamoja na mizigo ili kuongeza ufanisi wa huduma za bandari ya Malindi.
Mafanikio ya hatua hiyo yameanza kupatikana ikiwemo kupunguza muda wa meli kukaa ukutani, wafanyabiashara kupata makontena yao ndani ya muda mfupi, kujengewa uwezo wafanyakazi na stahiki zao kuongezeka. Pia gharama za usafirishaji zimepungua, ulinzi na usalama bandarini umeimarika na mapato yameanza kuongezeka.
Aidha, utoaji wa huduma kwa wateja kupitia mifumo ya kidijitali umeimarishwa kwa kuweka mifumo na taratibu zilizo wazi zenye malengo ya kurahisisha kupata huduma bora kwa wadau (customer-oriented service). Utaratibu wa kuwa na bandari kavu umeanza ili kupunguza mrundikano wa makontena katika bandari ya Malindi. Serikali tayari imetoa eneo la Maruhubi kutumika kuhifadhia kontena. Vile vile kwa kushirikiana na wawekezaji Serikali imeanzisha bandari ya mizigo katika eneo la Fumba. Sambamba na hilo Serikali ipo mwishoni kukamilisha hatua zote muhimu za kuanza ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mwangapwani. Hatua za uwekaji wa miundombinu muhimu katika bandari ya Mangapwani zinaendelea ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko (Ring Road).
Mipango ya Serikali ni kuifanya bandari hiyo kuwa ndio lango kuu la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutoa huduma bora zenye ufanisi katika kuhifadhi na kusafirisha mizigo, matengenezo ya vyombo vya majini na kuwa kituo kikuu cha kutoa huduma ya mwanzo katika ukanda wa bahari ya hindi. Pamoja na hatua hiyo Serikali inadhamira ya kuzifanyia matengenezo makubwa bandari zote nchini ili zitowe huduma zilizo bora. Aidha, Serikali imetiliana saini na kampuni ya ZF DEVCO ya Uholanzi juu ya mradi wa ujenzi wa Bandari kubwa ya kisasa ya abiria katika eneo la Mpigaduri. Tumedhamiria kuikarabati bandari ya Malindi iwe kubwa zaidi ndani ya Afrika Mashariki ya kutoa huduma za abiria na kuruhusu meli kubwa za kitalii kuweza kufunga nanga Zanzibar.
Katika kuimarisha usafiri wa baharini, Serikali imeamua kuifanyia matengenezo meli ya Mapinduzi 2 chini ya wataalam kutoka Jamhuri ya Korea ya Kusini (South Korea) wakisaidiana na wahandisi wetu wa ndani ili kukabiliana na changamoto ya usafiri iliyopo hasa baina ya Unguja na Pemba. Nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati wenzetu wa sekta binafsi Kampuni Azam Marine na Zan Fast farries kwa mchango wao katika kusaidia kukabiliana na changamoto hii kwa kuimarisha usafiri kati ya bandari ya Unguja, Pemba, Dar es Salaam na Tanga.
Ndugu Wananchi,
Sekta ya mafuta na gesi asilia haikupewa mazingatio kabla ya Mapinduzi. Kufuatia taarifa za kuwepo kwa rasimali hizo hapa nchini, Serikali baada ya Mapinduzi katika awamu mbalimbali za uongozi ilianza kuchukua hatua za kufanya tafiti zitakazowezesha kupatikana kwa mafuta na gesi asilia hapa Zanzibar. Serikali ya Awamu ya Nane nayo inaendelea na jitihada hizo. Serikali imekamilisha kazi ya ugawaji wa vitalu katika eneo la baharini kupitia taarifa zilizokabidhiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Agosti 2022. Kazi hiyo imefanywa kwa kushirikiana na Kampuni ya Kimataifa ya Schlumbeger ambapo vitalu 12 vimegaiwa katika eneo la baharini. Aidha, katika mwezi Julai 2023, Serikali ilitangaza rasmi kufungua maeneo ya uwekezaji kupitia vitalu vilivyogaiwa. Hatua hiyo ina lengo la kukuza sekta hii kwa kuwakaribisha wawekezaji wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
Ndugu Wananchi
Ujenzi wa miundombinu ni muhimu katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya ustawi wa jamii. Katika miaka 60 ya Mapinduzi jitihada mbali mbali zimefanywa na Serikali katika ujenzi wa barabara na uimarishaji wa viwanja vya ndege.
Serikali ilianza ujenzi wa barabara za lami na madaraja, shamba na mjini na kufanyiwa matengenezo kwa vipindi tafauti pamoja na kujengwa mpya katika awamu mbali mbali za serikali kwa lengo la kurahisisha usafiri. Serikali ya Awamu ya Nane nayo imeanza kwa mafanikio kazi ya ujenzi wa barabara kuu KM 103.5, barabara za ndani mjini na vijijini KM 275 pamoja na ujenzi wa barabara za mjini KM 100 na madaraja ya juu mawili katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar. Miradi hii inatekelezwa na Makampuni mbali mbali toka nje ya nchi.
Ndugu Wananchi
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio makubwa yamepatikana katika kuimarisha huduma za viwanja vya ndege na usafiri wa anga. Mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali kwenye viwanja vya ndege na usafiri wa anga, yamewezesha Mapato ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuongezeka kutoka TZS. Bilioni 11.6 mwaka 2019/2020 hadi kufikia TZS. Bilioni 29.3 mwaka 2022/2023. Aidha, kuna ongezeko kubwa la abiria wanaoingia na kutoka Zanzibar kwa kutumia Viwanja vya Ndege kutoka abiria 1,609,235 mwaka 2019 (Kabla ya UVIKO – 19) na 840,599 mwaka 2020 (wakati wa UVIKO – 19) hadi kufikia abiria 1,904,459 mwaka 2023.
Ndugu Wananchi,
Mafanikio mengine ni kuanza kazi kwa kampuni ya Emirate leisure inayoendesha biashara katika jengo jipya la TB3 pamoja na kampuni ya Dnata inayohusika na uhudumiaji wa ndege. Kupitia Kampuni hizi uwanja wa ndege wa AAKIA umeweza kupata tuzo ya Kimataifa kuhusu mabadiliko ya huduma bora za chakula na vinywaji kutoka “Airport Food & Bevarage (FAB) + Hospitality Conference & Awards’’ Bangkok nchini Thailand.
Kadhalika, Serikali imeingia Makubaliano na Kampuni ya SEGAP ya Ufaransa kuisaidia Menejimenti katika huduma za uendeshaji viwanja kwa lengo la kuimarisha utoaji huduma za usafiri wa Anga hapa nchini. Vile vile, kazi ya upembuzi yakinifu (feasibility study) imekwishanza kwa ajili ya ujenzi wa jengo la nne la abiria – TB4 katika kiwanja cha AAKIA. Ripoti ya awali tayari imeshakamilika na Serikali ipo katika hatua za kukamilisha utaratibu wa upatikanaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.
Kwa upande wa ujenzi wa Uwanja wa Pemba, Serikali imeshakamilisha hatua za tathmini na kuanza kulipa fidia. Sambamba na hilo, Serikali imekamilisha kazi ya uwekaji wa taa za kuongozea ndege katika njia ya kurukia ndege (Portable AGL lights system) ili kuziwezesha ndege kutua na kuruka kwa usalama zaidi wakati wa usiku na wakati wa mvua na mawingu.
Ndugu Wananchi
Katika awamu zote baada ya Mapinduzi, Serikali ilifanya jitihada za kuwezesha upatikanaji wa huduma za umeme kwa wananchi pamoja na miradi ya kiuchumi. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio yamepatikana katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za umeme nchini.
Kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za umeme kwa urahisi, Serikali imepunguza bei ya kuunganisha umeme kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 50. Punguzo hilo ni kutoka TZS. 464,000 kufikia 200,000 kwa gharama za uungaji usiozidi mita 30. Vile vile, kutoka TZS. 1,700,000 kufikia 690,000 kwa gharama za uungaji wa nguzo moja na kutoka TZS. 2,600,000 kufikia 1,040,000 kwa gharama za uungaji wa nguzo mbili.
Hatua hiyo imesababisha idadi ya wateja wanaoomba kuunganishiwa umeme kuongezeka hadi kufikia wastani wa wateja mia mbili (200) kwa siku katika kipindi hiki kutoka wastani ya wa wateja 50 kwa siku hapo awali. Wananchi wengi wameweza kufikiwa na huduma ya umeme ambapo Shirika la ZECO limeweza kuwaungia umeme wananchi 93,124; (Unguja 78,122 na Pemba 15,002) sawa na ongezeko la wateja kwa asilimia 45 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kufuatia kuimarika kwa huduma za usambazji umeme vijijini katika kipindi cha miaka mitatu (3), Serikali imeweza kuviungia umeme jumla ya Vijiji 190 ambapo Unguja ni 116 na Pemba 74, sawa na asilimia 62 ya Vijiji 305 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025.
Katika kuhakikisha Zanzibar inapata vyanzo vyake vya ndani vya uzalishaji umeme, Serikali imesaini mkataba wa mauziano ya umeme (PPA) na Kampuni ya Generation Capital Ltd kwa lengo la kuwekeza katika nishati ya umeme wa jua kwa kujenga mtambo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 130. Aidha, Serikali imetiliana saini na Kampuni ya ESR ya Ujerumani ambayo itazalisha megawati 15 za umeme wa jua kwa ajili ya kisiwa cha Pemba. Sambamba na hatua hiyo, Serikali inashirikiana na mshauri elelezi kutoka Kampuni ya NOVAVIS INTERNATIONAL ya Marekani kufanya upembuzi yakinifu wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya umeme mdogo katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Vile vile, mshauri elekezi wa Kampuni ya WSP ya Canada amepatikana kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi wa laini kubwa ya kilowati 132 ya Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba kwa ufadhili wa AfDB, KOICA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Ndugu Wananchi
Kabla ya Mapinduzi watoto wengi wa Zanzibar hawakupata elimu kwa kukosa uwezo wa kuilipia, ubaguzi na uchache wa skuli. Baada ya Mapinduzi, fursa za upatikanaji wa elimu zimeimarika katika ngazi zote. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi, mafanikio makubwa yamepatikana katika uimarishaji wa miundombinu ya elimu na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi cha miaka mitatu ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya elimu kwa ujenzi wa skuli mpya zikiwemo za ghorofa, ujenzi wa maabara, ujenzi wa vyoo pamoja na ukarabati wa skuli mbali mbali. Jumla ya madarasa 2,273 yamejengwa ambapo madarasa 1,131 yamekamilika na tayari yanatumika. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la madarasa 773 katika lengo la kujenga madarasa 1500 kwa mujibu wa ilani ya CCM 2020 – 2025. Vile vile ujenzi wa maabara 10, vyoo 1,693 na ukarabati wa Skuli 24 umekamilika.
Juhudi hizi za Serikali zimeanza kuzaa matunda kwa kuimarisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa ya darasa la 7, kidato cha 4 na 6. Kwa upande wa matokeo ya darasa la 7 ufaulu umeongezeka kutoka wanafunzi 2,167 waliofaulu madarasa ya michepuo na vipawa mwaka 2021 na kufikia wanafunzi 6,666 mwaka 2023. Aidha Takwimu zinaonesha kuwa, ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 55.4 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 74 mwaka 2022. Pia, matokeo ya kidato cha sita ya mwaka 2023 yametupa taswira bora zaidi, ambapo asilimia 99.3 ya wanafunzi wamefaulu kuendelea na masomo ya chuo kikuu. Kati yao, asilimia 65.9 wamefaulu katika masomo ya Sayansi. Aidha, wanafunzi wawili tu kati ya wanafunzi 2,587 waliofanya mtihani walipata divisheni zero ikilinganishwa na wanafunzi 99 waliopata divisheni 0 mwaka 2021.
Kwa kuwazingatia wenye mahitaji maalum, Serikali imewajengea Skuli maalum mbili pamoja na kujenga ngazi mteremko (ramps) kwa ajili ya kuwasaidia wenye mahitaji maalum katika Skuli 43 Unguja na Pemba. Pia Serikali inakamilisha matayarisho ya ujenzi wa vyuo vitano vya mafunzo ya Amali na kuvifanya kuwa kumi kwa madhumuni ya kuzidi kupanua fursa za elimu ya ujuzi. Serikali pia imeimarisha mafunzo ya juu ya fani za ufundi katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia hadi ngazi ya shahada ya kwanza. Aidha, katika kuimarisha elimu jumla ya madawati 4,012 yaliyogharimu TZS Bilioni 1.98 kwa ajili ya Skuli za msingi yamenunuliwa na ajira 2,050 za walimu zimetolewa ili kupunguza tatizo la upungufu wa walimu.
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi, mafunzo ya walimu yameendelea kuimarishwa katika vyuo viwili vya ualimu vya Serikali na katika vyuo vikuu vilivyopo Zanzibar ambapo kabla ya Mapinduzi kulikuwa na Chuo kimoja tu cha ualimu cha Beit Raas. Fursa ya Elimu ya juu nayo imeimarika ambapo mwaka 2023, Vyuo vikuu vimedahili wanafunzi 11,272 katika fani mbalimbali kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ya uzamivu.
Ndugu Wananchi,
Bajeti ya Serikali katika Sekta ya elimu imeongezeka kutoka TZS Bilioni 265.5 mwaka 2021/2022 na kufikia TZS Bilioni 457.2 mwaka 2023/2024, sawa na ongezeko la asilimia 72.2. Aidha, Serikali inaendelea kuwapatia mikopo na udhamini vijana wanaojiunga na elimu ya juu ndani na nje ya nchi. Bajeti ya Serikali kwa Bodi ya Mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka TZS Bilioni 19 kwa mwaka 2022/2023 na kufikia TZS Bilioni 29.4 kwa mwaka 2023/2024. Ongezeko hili limenufaisha wanafunzi wa elimu ya juu 6,060 wanaosoma vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi. Hatua hii imewezesha kuzalisha wataalamu kwa wingi katika fani mbali mbali na kupunguza tatizo la kutegemea wataalam kutoka nje ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi,
Juhudi kubwa imefanywa na Serikali katika kipindi cha miaka 60 iliyopita kwa madhumuni ya kuimarisha huduma za afya ambazo kabla ya Mapinduzi zilitolewa kwa ubaguzi na hazikutosheleza mahitaji. Katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, mafanikio yamezidi kupatikana kutokana na mabadiliko makubwa ya muundo na uendeshaji wa huduma za afya nchini. Serikali imejenga Hospitali kumi (10) za Wilaya ambazo zimeshaanza kazi. Aidha, Serikali imedhamiria kujenga hospitali za Mikoa, ambapo kwa sasa ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Mjini magharibi iliopo Lumumba umeshakamilika na imeshaanza kazi.
Kuwepo hospitali hizi kumeboresha mfumo wa rufaa nchini kwa wagonjwa kuanza kupata huduma katika vituo vya Afya ya Msingi, Hospitali za Wilaya badala ya wagonjwa wote kukimbilia Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja. Hospitali za Wilaya hivi sasa zinatoa huduma bora za uzazi, upasuaji, maabara, rediolojia na ICU katika Wilaya zote Unguja na Pemba. Hatua hii imefungua ukurasa mpya wa upatikanaji wa huduma za afya hapa nchini.
Mafanikio mengine ni kuimarika kwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya kutokana na kuongeza bajeti ya dawa kutoka TZS. Bilioni 17 mwaka 2020 hadi TZS Bilioni 37.3 mwaka 2023/2024. Hivi sasa vituo vya afya vinapelekewa dawa kila mwezi. Dawa za Pemba zinapelekwa moja kwa moja na msambazaji bila ya kupitia Bohari kuu ya Dawa ya Unguja – Maruhubi.
Ndugu Wananchi,
Kwa kipindi cha miaka mitatu, Serikali imetoa ajira mpya 1,050 katika sekta ya Afya kati ya hizo 738 Unguja na 312 Pemba. Madaktari bingwa wameongezeka kutoka 50 mwaka 2020 hadi kufikia 90 mwaka 2023. Maslahi ya wafanyakazi yameboreshwa, mishahara imeongezwa kutokana kiwango cha elimu, muda wa ajira na kada muhimu. Mafanikio mengine ni kuanza kwa Mfuko wa Huduma za Afya (ZHSF) kuanzia Oktoba 2023. Huduma zake zinapatikana katika Hospitali za Umma na Binafsi. Hadi kufikia tarehe 31 Oktoba 2023, jumla ya Watumishi wa Sekta za Umma 53,490 wameingizwa katika mfumo.
Ndugu Wananchi,
Uimarishaji wa huduma za Afya nchini umepelekea kupunguza tatizo la mama wajawazito kujifungulia majumbani na vifo vya watoto wachanga. Vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka vifo 120 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi vifo 99 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022. Hali hii kwa kiasi kikubwa imechangiwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, wataalam na kuimarika kwa elimu ya Afya kwa jamii.
Vile vile, ufanisi umepatikana baada ya kuanza kwa utaratibu wa kutoa huduma za afya kwa ushirikiano na Sekta Binafsi. Utaratibu huu umeondosha usumbufu kwa wananchi wanaofika kupata huduma na vipimo vyote wanavyohitaji bila ya kulazimika kwenda hospitali binafsi. Aidha, usimamizi wa Hospitali za Wilaya unaofanywa na Taasisi binafsi umeimarisha hali ya usafi, upatikanaji wa chakula cha wagonjwa na mazingira ya nje kwa kupanda bustani. Utaratibu huu unahakikisha dawa zote muhimu zinapatikana katika hospitali zote za Wilaya.
Ndugu Wananchi,
Sekta ya maji ni miongoni mwa sekta muhimu kwa maisha ya watu na maendeleo yao. Baada ya Mapinduzi, Serikali ilianza jitihada ya kuwapatia huduma ya maji safi na salama wananchi wa Zanzibar wanaoishi mijini na vijijini. Jitihada hizo zimeendelezwa katika awamu zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, huduma ya maji safi na salama zimeimarika kwa kuongeza uzalishaji, uhifadhi na usambazaji. Katika awamu hii ya Nane tumeweza kutekeleza miradi miwili mikubwa. Miradi hiyo ni Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar wenye thamani ya Dola za Kimarekani TZS Milioni 92.18 na Mradi wa Ahueni ya UVIKO – 19 wenye thamani ya TZS Bilioni 40.2.
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu, jumla ya visima 102 vimechimbwa vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 201,552,000 kwa siku. Hatua hiyo itawezesha uzalishaji wa maji kuongezeka kufikia lita 345,388,735 tutakapomaliza kufungua miradi yote ya maji ambapo mahitaji kwa sasa ni lita 264,568,220. Jumla ya Skimu 9 mpya za maji tumeshazifungua rasmi katika kipindi hiki cha maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi, kati ya Skimu 17 mpya.
Ndugu Wananchi,
Jumla ya matangi 15 ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 134,000,000 yamejengwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi kupitia Mradi wa Uhuishaji na Uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji Zanzibar. Aidha, Matangi 10 yamejengwa Unguja na Pemba yenye ujazo wa lita milioni 1 kila moja kupitia Mradi wa Ahueni ya UVIKO – 19 yenye jumla ya ujazo wa lita 10,000,000 kuwezesha uhifadhi mpya wa lita 144,000,000 katika matangi mapya 25 ya miradi yote miwili.
Kabla ya ujenzi huo kulikuwa na matangi 64 kwa Unguja na Pemba yenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 46,915,000. Kukamilika kwa Miradi miwili mikubwa tutaweza kuwa na uhifadhi wa maji lita 190,915,000. Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 144 ya uhifadhi.
Ndugu Wananchi,
Kazi ya ulazaji mabomba ya kusambazia Maji kwa miradi yote miwili itafikia jumla ya KM 785.9, kwa mradi wa Exim Bank KM 466.0 na mradi wa Ahuweni ya UVIKO – 19 KM 319.0 katika kipindi cha miaka mitatu. Aidha, Serikali kupitia ZAWA imeanzisha Mfumo shirikishi (Intergrated Water Management System) unaosaidia kusimamia utekelezaji wa huduma ya maji, zikiwemo kuwafahamu wateja wa Mamlaka ya maji, kupeleka bili, kupokea malipo, kupata taarifa za uvujaji na ujazo wa maji katika matangi.
Jitihada hizi za Serikali hadi sasa, zimewezesha kupeleka huduma za maji safi na salama katika shehia 342 kati ya shehia 388 kwa kusambaza mtandao wa maji Unguja na Pemba. Lengo la Serikali ni kuwafikishia huduma endelevu za maji safi na salama wananchi wote wa Zanzibar kwa saa 24.
Miradi mingine mipya ya maji safi na salama iko njiani kutekelezwa ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa huduma hii ikiwemo Mradi wa KfW wa Ujerumani wenye thamani ya € Milioni 25 (Grant), Mradi wa JICA Yen Milioni 100, Mradi wa Mkopo wa Exim Bank USD Milioni 35 na Mradi wa NEC wenye thamani ya USD Milioni 26.
Ndugu Wananchi,
Ujenzi wa majengo kwa ajili ya makaazi, Ofisi na biashara umepewa umuhimu katika awamu zote za Serikali baada ya Mapinduzi. Kwa kuzingatia haja ya wananchi kupata makaazi bora, Serikali ilianzisha ujenzi wa nyumba za maendeleo mijini na vijijini na kuwapatia wananchi. Aidha, majengo ya huduma za kiofisi, hospitali na Skuli yalijengwa baada ya Mapinduzi ili kupata mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kuongeza ufanisi. Vile vile, ujenzi wa majengo ya Umma na Binafsi ya biashara unaendelezwa.
Katika kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, jitihada ya ujenzi wa majengo ya makaazi, biashara na Ofisi za Serikali umeshamiri. Ujenzi wa nyumba za makaazi kwa Mchina na Tomondo unaendelea. Vile vile Serikali imejenga maduka ya kisasa Darajani. Maandalizi ya ujenzi wa mji wa Serikali Kisakasaka yameanza pia ujenzi wa eneo la maonesho ya biashara Nyamanzi umikamilika na limeanza kutumika. Kwa lengo la kuimarisha haiba ya mji na kuondoa changamoto ya maegesho, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) inaendelea na mradi wa kituo cha mabasi Kijangwani na ujenzi wa maegesho ya kisasa katika eneo la Malindi. Serikali inaendelea kuwakaribisha Wawekezaji katika Sekta ya ujenzi zikiwemo nyumba za gharama nafuu, kumbi za mikutano na majengo ya biashara.
Ndugu Wananchi,
Nchi yetu ina historia ndefu ya maendeleo ya sekta ya habari na michezo kabla na baada ya Mapinduzi. Kuhusu sekta ya habari, juhudi kubwa zimechukuliwa na Serikali katika awamu zote za uongozi baada ya Mapinduzi kwa madhumuni ya kuimarisha utoaji na upatikanaji wa habari nchini. Serikali ya Awamu ya Nane imeziendeleza juhudi hizo kwa kuliimarisha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kwa kulipatia vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi na mafunzo kwa wafanyakazi ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma zake. Pia, Serikali imepanga kuimarisha Kampuni ya Uunganishaji Maudhui Zanzibar (ZMUX) kwa kuweka miundombinu ya urushaji wa matangazo na vifaa vya kisasa, gari la kurushia matangazo (OB VAN) pamoja na wataalamu ili kufanya kazi kwa ufanisi. Aidha, Shirika la Magazeti ya Serikali limeimarishwa kwa kupatiwa jengo jipya la Ofisi na mtambo wa kuchapia magazeti. Hatua hii imeliongezea Shirika ufanisi kwa kuhimili gharama na kuongeza uzalishaji na usambazaji wa magazeti kwa asilimia 80 ya Wilaya zote za Tanzania bara.
Kwa upande wa sekta ya michezo, Serikali ya Awamu ya Nane, imekamilisha matengenezo makubwa ya viwanja vya Amani na Gombani kuwa na kiwango cha kimataifa. Vile vile, katika uwanja wa Amani, ujenzi wa viwanja viwili vya mpira wa miguu vya nje, ukumbi wa judo na viwanja vya ndani vya michezo midogo umekamilika. Kadhalika, ukarabati mkubwa wa hoteli ya uwanja wa Amani unaendelea na kutarajiwa kukamilika hivi karibuni. Aidha, kupitia mradi wa michezo kwa ushirikiano na Serikali ya Ujerumani, tunakamilisha zabuni ya ujenzi wa viwanja vitatu vya michezo katika maeneo ya Mkokotoni, Kangani na Mchanga mdogo. Kwa lengo la kuimarisha sekta ya michezo, Serikali imeruhusu mchezo wa ngumi hapa Zanzibar ili kuwapatia nafasi wapenzi wa mchezo huo.
Ndugu Wananchi,
Utumishi bora wa Umma ni miongoni mwa vigezo vya Utawala Bora unaotekelezwa na kusimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kipindi chote cha miaka sitini 60 iliyopita. Katika miaka mitatu 3 hii, Serikali imechukua hatua mbali mbali za kuimarisha mazingira ya Utumishi wa Umma ili kuongeza ufanisi. Serikali imeongeza maslahi ya Watumishi kwa kupandisha mishahara na maposho kwa kuzingatia viwango vya Elimu, Kada na Uzoefu. Hatua hii, imeweza kuondoa malalamiko yaliyokuwepo ya kutozingatiwa suala la Elimu, Kada na Uzoefu katika Miundo ya Awali.
Katika marekebisho hayo, Serikali ilitumia jumla ya TZS. Bilioni 58.1 kwa mwezi kutoka TZS. Bilioni 35.5. Kiwango hicho ni ongezeko la TZS. Bilioni 22.6, sawa na asilimia 38.85. Vilevile, Serikali ilifanya marekebisho ya kima cha chini cha Pencheni kwa Wastaafu kutoka TZS. 90,000 kwa mwezi kwenda TZS. 180,000 sawa na asilimia 100. Kwa upande wa Pencheni jamii, Serikali imepandisha Pencheni hiyo kutoka TZS. 20,000 kwenda TZS. 50,000 kwa mwezi sawa na asilimia 150. Mbali na Pencheni, Serikali imefanya mabadiliko katika mifumo ya ulipaji wa Kiinua Mgongo kwa Wastaafu ambapo awali walikuwa wako