Afisa Mipango na Uratibu Halmashauri ya Msalala bw.Elkana Zabron akiwa na mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii, wanawake,vijana na walemavu Bw.Judica Sumari wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi Mtendaji NDG.Khamis Katimba akielezea dhumuni la kuitishwa kwa kikao Cha wadau kupitia mpango mkakati wa Halmashauri
Mwenyekiti wa halmashauri ya Msalala Mhe. Mibako Mabubu akifungua kikao Cha wadau wa halmashauri kupitia mpango mkakati wa halmashauri.
Baadhi ya wadau wa maendeleo wa halmashauri ya Msalala wakifuatilia mada zinazowasilishwa
………………………..
WADAU wa maendeleo katika Halmashauri ya Msalala, Kahama mkoani Shinyanga wamekutana na kupitia mkakati wa maendeleo wa miaka mitano ulioasisiwa 2021/2022.
Kwenye kikao hicho, mkurugenzi wa halmashauri hiyo Khamis Katimba, aliwataka wadau hao kupitia na kurekebisha kasoro zilizopo kwenye mpango huo tangu ulipoanza kutekelezwa miaka mitatu iliyopita.
“Mpango huu ulianza kutumika miaka mitatu iliyopita na sasa tunauishi, hivyo wadau tunayo nafasi nzuri ya kuchangia ili tufike mwaka 2025/2026 tukiwa pamoja na serikali yetu.
“Leongo letu ni kuhakikisha tunajua halmashauri inafanya nini kwa sasa na inalenga kufanya nini baadaye, ninaamini mtindo huu unitasaidia mimi kama mkurugenzi na watendaji wenzangu kuona kasoro wakati wa utekelezaji na kuchukua hatua,” alisema Katimba.
Miongoni mwa malengo yaliyomo kwenye mpango mkakati huyo ni pamoja na kuwezesha wananchi wa Msalala kufanya kilimo cha kibiashara, uchimbaji wenye faida, kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali, halmashauri kutangaza fursa za uwekezaji pia utnzaji wa mazingira na afya za wananchi.
Katika kikao hicho, Mbunge wa Msalala, Alhaj Idd Kassimu Idd ameeleza kufurahishwa nah atua ya Rais Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha zote za maendeleo zilizoahidiwa kwenye halmashauri hiyo.
“Halmashauri ya Msalala ni miongoni mwa halmashauri zilizopokea fedha zote za kutekeleza miradi ya maendeleo, ni halmashauri ya kwanza kupata fedha nyingi mkoani Shinyanga,” alisema.
Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kupitia fedha hizo kuwa ni ujenzi wa vituo vya afya katika Kata za Isaka, Mwalugulu, Segese, Bulige, Mwanase ambapo zaidi ya Tsh. bilioni 2.5 zilitumika kukamilisha vituo hivyo.
“Halmashauri ya Msalala imekamilisha zahanati 24 ambazo sasa zinatoa huduma, hii yote ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano,” alimema mbunge huyo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Msalala, OCD Masome ameitaka halmashauri hiyo kuboresha ulinzi na usalama kwa kuwa, ni kubwa na ina vyanzo vingi vya mapato.
“Maendeleo hayawezi kufikiwa pasipo kuwa na amani, hivyo katika mpango mkakati huu wekeni kipaumbele cha kwanza ulinzi. Halmashauri ya Msalala ina vyanzo vingi vya mapato hivyo tukiimarisha ulinzi na usalama tutavutia wawekezaji,” alisema.
Akiwasilisha mada ya mpango na bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Afisa Mipango wa halmashauri hiyo Elkana Zabron alisema, halmashauri imepanga kukusanya Tsh. 5.5 Bilioni ikiwa na ongezeko la Tsh. milioni 500 kutoka bajeti ya mwaka 2023/2024.
“Ongezeko hili litatokana na kufunguliwa kwa stendi ya mabasi ya Isaka, kuboreshwa kwa mazingira ya kukusanyia ushuru wa mazao, tozo za minada na maboresho ya ukusanyaji mapato kutoka kampuni zinazofanya kazi na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu,” alisema.
Baadhi ya wadau wa maendeleo kwenye kikao hicho wameitaka halmashauri hiyo kuboresha zaidi mazingira ya wawekezaji ili kuinua wananchi kwa kuwa, ina mazingira mazuri.
Kizito Mtendaji kutoka Kata ya Isaka ameiomba halmashauri kukaribisha wawekezaji kujenga maghala ya kuhifadhia mpunga na mashine za kukoboreshea mpunga.
Hakimu Dismas, Hakimu kutoka Mahakama ya Mwanzo ya Lunguya ameshauri halmashauri kupima maeneo yote yanayomilikiwa na serikali na hasa maeneo ya mahakama kutokana na kuwepo kwa mradi wa wa kimataifa wa kujenga mahakama.
“Hapa kigezo kikubwa ni ardhi iwe imepimwa, hivyo halmashauri iwezeshe suala hili sambamba na kuwezesha vitendea kazi kwa ofisi za watendaji wa kata/vijiji na kuyajengea uwezo mabaraza ya ardhi ya kata, kwani mabaraza haya yamekuwa yakiingilia shughuli zisizowahusu,” alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mibako Mabubu aliwashukuru wadau wa maendeleo ya halmashauri kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao kuhusu shughuli za halmashauri jiyo.
“Michango mliyoitoa nitahakikisha Mkurugenzi Mtendaji anafanyia kazi yeye na watumishi wote wa halmashauri sambamba na mimi kufanya kazi niliyoagizwa na madiwani,” alisema.
.