Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Ukiriguru Mkoani Mwanza imetakiwa kufanya utafiti unaoendana na hali halisi ya matokeo ya upatikanaji wa mazao kwa wakulima hatua itakayosaidia kuwa na kilimo chenye tija nchini.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Januari 10, 2024 na Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde, alipokuwa akizungumza na watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru Jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi.
Amesema utafiti unaonesha kuwa mbegu ya UK 08 inaweza kuzalisha kati ya kilo 1000 hadi 1200 kwenye heka moja lakini ikienda kwa mkulima wa kawaida anapata kilo 500 kwa heka moja hivyo kupelekea matokeo ya utafiti na uhalisia kukinzana.
Silinde ameeleza kuwa Wizara iko tayari kuwasaidia katika kila jitihada wanazozifanya ikiwemo kuwapa vitendea kazi, kuwawekea mradi wa umwagiliaji ili waweze kuzalisha mbegu kwa mwaka mzima.
“Utafiti unafayika kwa miaka sita na mkulima anahitaji mbegu kwaajili ya kuanza kilimo hivyo tutakapofanya kilimo cha umwagiliaji itasaidia sana kuwa na kilimo endelevu”, amesema Silinde.
Amesema Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ujenzi wamekubaliana kwenye maeneo yote ya changamoto za barabara ambapo kunakuwa na upitishaji wa maji watajenga mabwawa ili maji hayo yasipotee na yatatumika katika shughuli za kilimo sanjari na kutengeneza mipango endelevu itakayosaidia barabara zisiharibike.
Aidha, Silinde aliongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anaunga mkono kwa asilimia 100 kwenye kilimo na adhima yake ni kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla ili kuweza kudhibiti mfumuko wa bei na usalama wa chakula nchini.
Kwaupande wake mtafiti mgunduzi wa mbegu za Pamba kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru Seperatus Kamuntu, amesema mbegu ya UK08 ndio iko kwenye soko na inazaa vizuri pia inauvumilivu mdogo wa vishambulizi visumbufu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Ukiriguru Dkt.Paul Saidia, amesema hadi sasa wana mbegu takribani 10 lakini pamoja na mbegu zote hizo wanachangamoto mpya iliyoibuka ya wadudu wasumbufu (chawajani) ambao wanafanya uharibifu kwenye mazao.
“Kutokana na changamoto hiyo tumeanza nguvu mpya ya kushirikiana na bodi ya Pamba na wadau wengine katika kuhakikisha mbeleni tunapata mbegu bora ambayo inaukinzani kwenye tatizo la wadudu hao”, amesema Dkt.Saidia.