Kisima kinachozalishaji maji kwa ajili ya eneo la viwanda kata ya Lilambo manispaa ya Songea.
Tenki la kuhifadhi maji kwa ajili ya eneo la viwanda Lilambo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira manispaa ya Songea(Souwasa)Mhandisi Patrick Kibasa akielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na mamlaka hiyo.
……..
Na Mwandishi wetu, Ruvuma
MKURUGENZI wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira manispaa ya Songea (Souwasa)Patrick Kibasa,ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipa fedha mamlaka hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Alisema kwa muda wa miaka miwili , Souwasa imetekeleza jumla ya miradi minne ambapo miradi miwili ya Lilambo wenye thamani ya Sh.milioni 416 na mradi wa Mwengemshindo uliogharimu Sh.milioni 547 imekamilika na imeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Kibasa,mradi wa maji Mwengemshindo unahudumia takribani wakazi 3,000 na mradi wa Lilambo umejengwa maalum kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa viwanda 200.
Amesema,kukamilika kwa miradi hiyo kumewezesha Mamlaka kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 85 mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 87 mwaka 2023.
Kibasa ameyasema hayo jana,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi na utoaji wa huduma ya maji kwa Waandishi wa Habari ofisini kwake mtaa wa Mahenge mjini Songea.
Ametaja miradi miwili inayoendelea kutekelezwa ni mradi wa maji Subira uliotengewa Sh.bilioni 1.2 ambao utakapokamilika utawanufaisha wakazi 13,000 wa kata ya Subira na mradi wa miji 28 uliotengewa Sh.bilioni 145.77.
Alisema,mradi wa miji 28 mkandarasi wake ameshapewa Sh.bilioni 21 ikiwa ni malipo ya awali na wanategemea ataanza ujenzi muda wowote kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa Kibasa,mradi huo na mradi wa Subira itakapokamilika itaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 87 ya sasa hadi kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2025.
“tunategemea baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa miji 28 tutafikia asilimia 100 ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi kama Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inavyoelekeza”alisema Kibasa.
Mkazi wa mtaa Bombambili Salum Athuman,ameipongeza serikali kupitia wizara ya maji kwa kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika manispaa ya Songea.
Oswald Kapinga alisema,kwa sasa wanapata maji ya uhakika ikilinganisha na miaka ya nyuma ambapo walikaa kati ya siku 2 hadi 3 bila kupata huduma hiyo na hivyo kuathiri sana shughuli zao za kiuchumi kwa sababu walitumia muda mwingi kwenda kutafuta maji.