OR-TAMISEMI
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kuhakikisha anamsimamia Mhandisi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Iringa inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kuongeza idadi ya mafundi kama ilivyoelekezwa kwenye mkataba na ujenzi ufanyike usiku na mchana.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo, Mhe. Ndejembi ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo kutokana na idadi ndogo ya mafundi huku akiagiza kufungwa kwa taa ili ujenzi wa shule hiyo ufanyike usiku na mchana ili kukamilika haraka na wanafunzi wa Mkoa wa Iringa waweze kunufaika na shule hiyo kama ilivyo dhamira ya Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“ Mkurugenzi na timu yako ya afisa manunuzi na mhandisi hakikisheni mnambana fundi mkuu wa mradi huu ili aongeze idadi ya mafundi kama mkataba unavyosema. Mkataba unasema kila jengo liwe na mafundi nane lakini hapa tumekagua tumeona jengo moja lina fundi mmoja hadi wawili, hii haikubaliki na ilitakiwa ikamilike mapema ili Januari 8,2024 wanafunzi waingie darasani.”
” Mhe. Rais Samia ameleta fedha Sh.Bilioni nane kwa ajili ya ujenzi huu niwaagize msimamie haraka mafundi waongezwe na ujenzi ufanyike usiku na mchana nataka tuone kasi ya ujenzi huu kwa sababu hakuna chochote kinachokwamisha,” amesema Mhe. Ndejembi.