Na Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Januari Makamba amesema kutokana na umuhimu wa Sera ya Mambo ya Nje kuna haja kwa watanzania kutoa maoni ya marekebisho ya Sera hiyo mpya ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 ili kuendana na wakati .
Hayo ameyasema leo Januari 9,2024 wakati akifungua kongamano la pili la kukusanya maoni ya wadau mahsusi kuhusu marekebisho ya sera mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 yaliyofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa sera ndio inasaidia kufikia malengo hayo kwahiyo sio jambo dogo ni lazima watanzania kushiriki katika kutoa mchango wa kufanya maboresho hayo kwamba sera inayotumika sasa hivi ni ya mwaka 2001 na dunia inapitia mabadiliko mbalimbali.
“Kutokana na umuhimu wa Sera ya Mambo ya Nje tunao wajibu wa kutoa maoni yetu sasa Sera ya Mambo ya Nje ni tamko la Nchi lenye kutoa mwongozo na mwelekeo kuhusu madhumuni,malengo kwenye kushiriki jambo kubwa,kwenye kushiriki kutengeneza tamko la nchi na misingi ya Tanzania itakavyoshirikiana na wadau wengine duniani”amesema
Aidha amesema jambo hilo ni mahsusi wa kipekee kwasababu ya historia ya nchi yetu,heshima kwenye masuala ya kimataifa Tanzania tangu harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu ambazo zilishirikisha wadau wengine duniani.
Ameongeza kuwa harakati za kutafuta uhuru wa Afrika na Ukombozi wa watu waliokuwa wanaonewa sehemu mbalimbali duniani katika harakati za kutafuta maendeleo ni ya nchi zinazoendelea Tanzania imekuwa kama bondia wa uzito wa juu kwa kuheshimika,inasikika na inaushawishi licha ya nguvu yake ndogo ya kiuchumi.
“Nchi yetu katika mahusiano ya Kimataifa ushirikiano wa kimataifa ina sifa na hadhi ya kipekee tangu uhuru na wajibu wa viongozi wa nchi kulinda haki na heshima ya sifa hii kwasababu ndio inayotoa ushawishi na kutuwezesha sisi kufanya mambo yetu nchini kwa urahisi na wepesi,kwasababu nchi ili ipige maendeleo kwa kasi lazima ijenge ushawishi duniani”amesema
Aidha Waziri Makamba amesema kama nchi lazima wapitie upya Sera ili kuona inaendana na mazingira ya sasa,mabadiliko yanayotokea kwa kasi duniani,malengo yetu ya sera ya maendeleo yataezeshwa vipi na sera mpya ili kuendana na mazingira yaliopo sasa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassoro amesema sera ya Mambo ya Nje ni misingi ya uhusiano wa Nchi na Mataifa mengine,hivyo iliunda timu ya pamoja ya wataalam na kufanya tathmini ya mapitio ya sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001 ili kufanya marekebisho yatayoendana na mahitaji ya sasa.
Amesema zoezi hilo la tathmini na mapitio limetumia mbinu mbalimbali ikiwemo mahojiano na wadau na kufanya tafiti katika vyombo vya habari mbalimbali kusambaza madodoso katika muendelezo huo wanakusanya maoni kupitia kongamano hilo.
Nao baadhi ya wadau wa kongamano hilo, akiwemo Mwanasiasa mkongwe Prof, Anna Tibaijuka, amependekeza kuwepo na timu ya wataalamu wa kidiplomasia kwamba waheshimike katika kufanya utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo maboresho ya sera hiyo.
Tibaijuka amesema wataalamu hao endapo wataheshimiwa na kuthaminiwa wataweza kusaidia kutumiwa katika maeneo mbalimbali kwani wataweza kukuza uchumi wa kidipromasia ndani na Nje ya Nchi.
Kwa upande wake Mwanasiasa mkongwe na Mbobezi wa masuala ya Uchumi Prof, Ibrahim Lipumba ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha wanafanya mchakato wa kuwaandaa vijana wa Sasa na wa baadaye kuwa wanadipromasia wapya na mahiri watakaoweza kuimarisha hali ya kisiasa na kiuchumi ndani na Nje ya Nchi.