Na Mwandishi wetu, Hanang’
CHAMA cha Makatibu wa Afya Tanzania (AHSATA) wametoa msaada wa sare za shule, nguo za ndani na vifaa vya kusomea kwa wanafunzi walioathirika na maafa yaliyotokea Desemba 3 mwaka 2023 Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara.
AHSATA wametoa msaada huo Januari 6 mwaka 2024 ambao ni pamoja na Madaftari elfu moja (1,000), Kaptula 100, Mashati 100,, sketi 100 pamoja na nguo za ndani.
Katibu wa Afya wa Mkoa wa Manyara, Thomas Malle akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Chama amesema msaada huo umetolewa na Makatibu wa Afya Nchini Tanzania.
“Wanachama wa AHSATA ambao ni watumishi wa umma baada ya kusikia maafa yaliyotokea Hanang’ waliamua kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa michango yao ili kuwasaidia wanafunzi waliopatwa na maafa hayo,” amesema Malle.
“Wapo wanafunzi wa shule za msingi watakaofanya mtihani wa kitaifa kwa mwaka huu wa 2024 ikiwemo wa darasa la saba, la nne hivyo wanapaswa kusaidiwa,” amesema Malle.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Janeth Mayanja, akipokea msaada huo, amewashukuru Makatibu wa Afya kwa kuwasaidia wanafunzi walioathirika na maafa hayo kwa wakati sahihi.
Mayanja amewapongeza Makatibu wa Afya nchini kwa kuwasaidia wanafunzi hao kwani umefika kwa wakati muafaka kutokana na shule za Msingi kufunguliwa Januari 8 mwaka 2024.