Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (kulia
mbele) akifunua kitambaa kuashiria ufunguzi wa Jengo la Mamlaka ya
Maji Zanzibar uliofanyika wilayani Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi
tarehe 8 Januari 2024. Kushoto mbele ni Waziri Maji, Nishati na Madini
Zanzibar, Mhe. Shaibu Kaduara,
………………….
*Awapongeza Rais Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi kwa maono na miongozo yao kutekeleza Miradi ya kimkakati
*Aipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini kupitia ZAWA kwa kukamilisha Jengo lenye ubora na hadhi ya juu
*Ataka ZAWA kutoa huduma bora
Zanzibar
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amefungua Jengo la Afisi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) lililoko eneo la Madema, Zanzibar na kupongeza mafanikio na ushindi wa kufanikisha miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.
Dkt Biteko amesema, kuelekea Kilele cha Mapinduzi ya Zanzibar, watu waliopewa dhamana ya kusimamia miradi hiyo ambayo Serikali imepeleka fedha nyingi, wafanye kazi kwa uaminifu kwani watatatoa hesabu si tu kwa waliowaweka madarakani, au Wananchi bali kwa Mwenyezi Mungu, hivyo wafanye kazi kwa uaminifu mkubwa.
“Nitoe wito kwenu ZAWA hakikisheni mnawahudumia vema Wazanzibari, ili waone fahari ya kuhudumiwa na ninyi, na nitoe wito kwetu Sisi tuliopo madarakani kuhakikisha tunatoa huduma kwa weledi wa hali ya juu kwa maslahi ya Wananchi wetu” Alisisitiza Dkt. Biteko
Aidha, alipongeza pia Wizara ya Maji kwa kuwajali wafanyakazi wake kwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa wafanyakazi wake ikiwa ni kuwajengea jengo lililoondoa changamoto ya nafasi kwa wafanyakazi hususani kwenye jengo la awali.
Dkt Biteko amesema, ujenzi wa Jengo Hilo la ghorofa 4 lililogharimu kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 92.18 kama mkopo toka Benki ya Exim Kutoka India kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, unahusisha Ofisi za wafanyakazi, Maabara, Ukumbi wa Mikutano, Maegesho na Ukumbi wa Mazoezi na kuipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini kwa kujenga jengo lenye hadhi na ubora wa hali ya juu.
“Niwashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maono na miongozo yao iliyopelekea kukamilika kwa miradi mikubwa na ya kimkakati yaani wanaupiga mwingi” Alisisitiza Dkt. Biteko.
Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Shaibu Kaduara, amesema ujenzi wa jengo hilo ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo Maji na tayari miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa ili kutatua kero ya Maji visiwani Zanzibar na kuongeza kuwa wataendelea na kasi hiyo bila kulala ili kuwaletea maendeleo wanachi wa Zanzibar.
Alimpongeza Mhe. Dkt. Biteko kwa ushirikiano ambao Zanzibar inapata hususani kwa miradi ya Umeme hususani uimarishaji wa miundo mbinu ya umeme, kwa kutekeleza mradi wa kuleta umeme kutoka Tanzania Bara, kilovolt 220 kutoka Rasi Kilomoni na ule wa Pemba kwa Msongo wa Kilovoti 132 na kuishukuru Serikali kwa Kufanikisha miradi hii.
“Zanzibar ndio nchi pekee Afrika Mashariki, na pengine Duniani kwa kuwajali wananchi wake kwa kuwapatia Maji ambayo wanayachagia na sio kulipia Maji” Alisisitiza Mhe. Kaduara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Mhandisi. Dkt. Salha Mohamed, amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza mwezi Machi, 2021 ikiwa ni sehemu ya uhuishaji na ustawishaji Maji Zanzibar chini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maji chini ya miradi mitatu ambapo wa kwanza ni wa Mfenesini na Dole unaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 26,167, 200, Awamu ya pili unaogharimu kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 27,740,731, ambao umejenga matanki makubwa sita, matatu chini, na matatu juu, na ya tatu ni ile inayohusiaha Masongini, Kwarara na ZAWA kwa ujenzi wa matanki matano, na unagharimu kiasi cha zaidi ya milioni 35.
Aidha, Mhandisi Dkt. Salha aliwashukuru Afisi ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Wakandarasi na wadau wote waliochangia kufanikisha ujenzi wa jengo hilo la Mamlaka ya Maji -ZAWA