Na Mwandishi Wetu, Lindi
MWENYEKITI wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi, Isihaka Mchinjita amesema anatarajia kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Tanzania Bara.
Kwa sasa nafasi hiyo kwa upande wa Tanzania Bara inashikiliwa na Doroth Semi ambaye ameweza kuitumikia kwa kiwango cha kuridhisha.
Mchinjita, ametangaza nia hiyo leo mkoani Lindi ambapo ameweka wazi baada ya kuwa Mwenyekiti wa mkoa wa Lindi kwa miaka mitano anaona kwa sasa anafaa kugombea ngazi ya taifa.
“Nimekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2019 mpaka sasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo. Nimetoa mchango wangu wa ujenzi wa chama chetu katika nafasi hizi mbili kwa uaminifu na moyo wa dhati kwa chama changu.
Ninawashukuru wanachama wenzangu wa Mkoa wa Lindi ambao waliniamini na wajumbe wa Halmashauri Kuu ambao walinichagua kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama.
Katika uchaguzi unaoendelea ndani ya chama changu ambapo kwa sasa tupo katika hatua za chaguzi za mikoa, sitogombea nafasi ya mwenyekiti. Ninaamini chama chetu Mkoa wa Lindi kimeimarika ambapo kwa sasa ni imara kimuundo kuanzia kwenye matawi yaani vijiji au mitaa mpaka ngazi ya jimbo,” alisema.
Alisema majimbo yote nane ya Mkoa wa Lindi yameshakamilisha uchaguzi kwa ngome zote pamoja na kamati ya uongozi wa jimbo, hivyo ni matarajio yake kuwa viongozi wa majimbo ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu watafanya kazi bora ya kutuchagulia safu imara ya uongozi wa mkoa kwa ngome zote na Kamati ya Uongozi Mkoa.
“Ninawatakia kila la kheri wagombea wote wanaoendelea kujitokeza kugombea uongozi katika nafasi zote ngazi ya mkoa,” alisema.
Mchinjita alisema baaada ya kushiriki katika uongozi wa chama kwa nafasi ya mwenyekiti Mkoa na Mjumbe wa Kamati Kuu, anayo nia ya kuomba ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama kunipa nafasi ya kukitumikia ngazi ya taifa.
“Katika uchaguzi mkuu ujao unaofanyika kuanzia Machi 2 hadi 3 ,2024, ninatangaza nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara. Wakati utakapofika nitaeleza kwa undani dhamira na aina ya mchango nitakaoutoa endapo wajumbe wa Mkutano Mkuu wataona nipewe nafasi kukiongoza na kukitumikia chama chetu katika nafasi hii. Ninawashukuru, ” alisema.