*Akabidhi Pikipiki na kofia ngumu Jumuiya ya Wazazi (CCM) Zanzibar
*Awataka kutumia pikipiki hizo kuieneza CCM
*Azuru Kaburi la Hayati Abeid Amani Karume
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameitaka Jumuiya ya Wazazi ya CCM kutumia rasilimali walizonazo katika kukijenga na kukieneza Chama cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuzungumza na wananchi kuhusu kazi kubwa za maendeleo zinazofanywa chini ya Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Biteko ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Kundi la Wazazi), amesema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dogo Mabrouk. Kikao kilifanyika katika Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Kama wewe ni Mwenyekiti wa Mkoa, Katibu wa Mkoa au kiongozi yoyote yule, kwa kutumia rasilimali ulizonazo tembelea maeneo ya mkoa wako, Wilaya na Vijiji hata mara moja, zungumza na makundi mbalimbali ikiwemo Wajumbe wa Kamati za utekelezaji za Jumuiya yetu na waeleze kuhusu masuala ya kujenga na kueneza Chama. Hii inawezekana, tujipange, tufanye ziara hata kama ni kidogo, polepole tutafanya makubwa kadri tutakavyoendelea, tuwe mstari wa mbele kueleza mafanikio ambayo CCM na Serikali yake wameyafanya.” Amesisitiza Dkt. Biteko
Amesema kuwa, Jumuiya ya Wazazi ya CCM ni Jumuiya kubwa ndani ya Chama hivyo inapaswa kufanya kazi za kukijenga Chama kwa ukubwa huo kwa kuwa inabeba makundi yote ndani ya CCM na haina mipaka au ukomo wa mtu kuwa sehemu ya Jumuiya.
“Nikitolea mfano Jumuiya yetu ya Wanawake, inahusu Wanawake katika Chama, Jumuiya ya Vijana umri fulani ukifika unakuwa hauna vigezo, lakini Jumuiya hii haina mipaka hivyo inapaswa kuwa na nguvu kubwa, tutumie ukubwa wa Jumuiya hii kuwasaidia Mwenyekiti wetu na Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar katika kujenga Chama na kuzungumza kwa ukubwa yale yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika.” Ameeleza Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi wanataka kuona viongozi wa Chama katika ngazi mbalimbali wanawasaidia kazi ikiwemo ya kueleza mafanikio makubwa ya kimaendeleo yanayoendelea kufanyika na kazi kubwa inayofanywa na viongozi hao katika kuwaunganisha Watanzania, kuwa na maridhiano na kujenga uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Dogo Mabrouk amemshukuru Dkt.Biteko kwa kuithamini Jumuiya hiyo na kwa kuiwezesha kwa vitendea kazi ambavyo vitaboresha utendaji wa Jumuiya kwenye mikoa sita ya Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, Dkt. Biteko alizuru katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume lililopo Kisiwandui Zanzibar.
Aidha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mhe. Dkt. Biteko amekabidhi PikiPiki Sita kwa ajili ya Jumuiya ya Wazazi (CCM), Zanzibar pamoja kofia ngumu kwa ajili ya Jumuiya hiyo kwenye Mikoa Sita ya Zanzibar.
Amesema kuwa, pikipiki hizo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi (CCM) ambapo ameelekeza kuwa, pikipiki hizo zikafanye kazi ya siasa kama ilivyokusudiwa.