Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM taifa Mhe Dkt Angeline Mabula amekabidhi jumla ya mifuko mia mbili kwaajili ya ujenzi wa Zahanati ya Luhanga na ujenzi wa barabara ya mlima wa Rada mtaa wa Kabambo kila mradi mmoja ukipata mifuko mia moja ya saruji.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa shule mpya ya sekondari Kisenga iliyopo kata ya Kiseke Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi wa kata hiyo kuishukuru Serikali ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwani imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 68 kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa shule hiyo mpya iliyogharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 584 kupitia mradi wa SEQUIP
‘.. Jumla ya mifuko yote itakuwa mifuko mia sita, Kwa maana mifuko mia mbili naitoa kata hii kwaajili ya ujenzi wa Zahanati mifuko mia moja na barabara mifuko mia moja, Lakini tutapeleka mifuko mia mbili mingine kata ya Mecco na mia mbili nyengine kata ya Nyamanoro ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amepiga marufuku vikwazo vya aina yeyote vitakavyosababisha wanafunzi wanaotarajia kuanza kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2024 kushindwa kuripoti shule ikiwemo michango isiyokuwa ya msingi na lazima kama kuchangia madawati kwa kuwa Serikali imeshachukua jitihada mbalimbali kumaliza kero hizo
Kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Ilemela Wakili Mariam Abubakar Msengi amesema kuwa Rais Dkt Samia amewatatulia wananchi mzigo mkubwa hasa katika kipindi kama hichi cha kuanzia mwaka wa masomo kwani wananchi wangekuwa wanakimbizana kujichanga kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na madawati hivyo kuwaomba kutunza miundombinu ya shule hiyo pamoja na kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na shule wanaripoti pindi shule zinapofunguliwa
Nae diwani wa kata ya Kiseke Mhe Mwevi Ramadhan mbali na kuishukuru Serikali na Mbunge wa Jimbo hilo Kwa namna anavyoshirikiana nae katika kumaliza kero za wananchi wake amewataka wananchi hao kuwachagua tena Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan na Mbunge Dkt Angeline Mabula kama ishara ya Shukran Kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya kata yake
Dkt Angeline Mabula pia ametoa tofali kwaajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ndani ya Jimbo hilo hivyo kuwataka wananchi kuendelea kutekeleza sera ya Jimbo hilo ya utatu Kwa wananchi kuanzisha miradi, Mbunge kutoa tofali za utekelezaji wake na kisha manispaa kumalizia