…………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi, Hanang
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wananchi na wadau Mkoani humo imetoa raslimali fedha na michango mbalimbali vyote vikiwa vimegharimu sh. milioni 107.2 kwa wakazi waliopata maafa ya mafuriko Hanang ,Disemba 3 Mwaka 2023.
Kati ya michango hiyo ni pamoja na fedha sh.milioni 55.5 na vifaa vyenye thamani ya milioni 51.734.5 .
Akikabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang Janeth Mayanja, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Zephania Sumaye akiwa ameambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta, alieleza , michango yote ni mchango kutoka kwa wadau, viongozi wa dini, watumishi na wananchi.
Alitaja vifaa vilivyotolewa ni vyakula ikiwemo ngano kilo 125, mafuta ya kupikia lita 290 ,mchele kilo 590, unga wa mahindi kilo 1,425, sabuni ,tambi na nazi”.
“Vingine ni vifaa vya nyumbani bakuli,sahani,vikombe viroba 11, sufuria box 10 sawa na sufuria 960, viatu ,viroba vya nguo sita, taulo za kike 448, magodoro 107 na blanket 95.
Zephania alieleza pia kuna vifaa vya ujenzi, nyaya za umeme rola 71 ,mabati 250 sanjali na vifaa vya usafiri pikipiki tano.
Akipokea hundi na vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Janeth Mayanja ,alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wananchi na wadau wa Mkoa huo.
Alieleza , maafa ya mafuriko ya mvua yalitokea Disemba 3 mwaka uliopita na kusababisha maafa makubwa ikiwemo vifo , majeruhi, maporomoko,nyumba kusombwa na maji .
Alisema kwa niaba ya Serikali anashukuru kwa mchango huo mkubwa .
Janeth alibainisha kwamba ,katika kambi tatu za watu walipoteza nyumba zao Serikali inaendelea na taratibu za makazi mapya kwa ajili ya wananchi hao ambapo tayari maeneo yamepatikana na ujenzi unakaribia kuanza.