Na Issa Mwadangala
Wakazi wa Mkoa wa Songwe wametakiwa kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalum katika jamii kwa lengo la kuwafariji na kuwaweka karibu na jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya Jinai Mkoa wa Songwe Mrakibu wa Polisi SP William Nyamakomago Januari 03, 2023 katika hafla iliyoandaliwa na kikundi cha kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu kiitwacho African Genius Foundation tawi la Songwe.
Naibu Mkuu wa Upelelezi SP Nyamakomago amesisitiza suala la utoaji wa malezi bora kwa wajukuu wanaoishi na wazee na kuwataka wazee hao kuwafundisha mila na desturi za kitanzania ili kuzuia mmomonyoko wa maadili kwa watoto kwa lengo la kujenga taifa imara linalokemea na kupinga vitendo vya ukatili na uhalifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Aidha, Sp Nyamakomago amewaomba wananchi wa Mkoa wa Songwe kutoa msaada kwa watu wenye mahitaji maalum kama kilivyofanya kikundi cha African Genius Foundation kwani kufanya hivyo ni neema kwa mwenyezi Mungu.
Naye Mhamasishaji na Mratibu wa kikundi hicho Mkoa wa Songwe Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Sadam Kitembe amesema kuwa katika kikundi hicho wamejiwekea utaratibu wa kuwasaidia watu wenye uhitaji maalumu kama yatima, wajane, wazee na watu wanaoishi katika mazingira magumu kwa lengo la kuwaweka karibu na jamii.
Kwa upande wa wazee hao wamelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa elimu walioipata na wameahidi kutoa ushirikiano katika kila jambo linalohusu uhalifu na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto ili kuwa na jamii bora iliyo na kizazi imara katika jamii.
Katika halfa hiyo wazee hao walipata nafasi ya kushiriki chakula cha mchana na viongozi wa kikundi hicho na kupatiwa mahitaji mbalimbali kama sabuni, mchele, mafuta ya kupikia, mafuta ya kupakaa,sukari, chumvi na nguo.