Waziri wa Nchi (OR) Kazi,uchumi na uwekezaji akitoa taarifa kuhusina na maonesho ya kazi zinazofanywa na taasisi za umma na binafsi kupitia magari. (PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO )
………….
Na Imani Mtumwa, Maelezo Zanzibar
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika barabara kuyapokea na kuyasherehekea maonesho ya kazi zinazofanywa na Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na maonesho hayo huko Ofisini kwake Mwanakwerekwe amesema kwa mara ya kwanza Wizara hiyo imeandaa maonesho hayo yanayotarajiwa kufanyika januari 4 mwaka huu ili kutatoa fursa kwa taasisi hizo kutangaza kazi zao pamoja na wananchi kuona kazi zinazofanywa na taasisi hizo.
Mhe. Mudrik ameeleza kuwa maonesho hayo yanatarajiwa kupokelewa na Makamo wa Pili wa Rais Mstaafu wa awamu ya saba Mhe. Balozi Seif Ali Iddi katika Viwanja vya Mnara wa Kisonge ambapo magari hayo yatatoa huduma mbalimbali kwa wananchi viwanjani hapo.
Alifahamisha kuwa magari hayo yatapita barabarani kuanzia Amani kupitia Mikunguni kwa Pweza, Saateni, Pinda Mgongo, Malindi, Darajani, Kisiwandui, Michenzani, Kisonge, Kariakoo na kurudia Michenzani na baadae kupitia Madema na kumalizia katika viwanja vya Maisara kuanzia saa 7:30 za mchana hadi saa 12:00 za jioni.
Maonesho hayo yameandaliwa na Wizara ya nchi (OR), Kazi, Uchumi na Uwekezaji kwa kushirikiana na Mkoa wa Mjini Magharibi kuelekea maadhimsho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yanayotarajiwa kufikia kilele chake Januari 12.
MAELEZO YA PICHA
Waziri wa Nchi (OR) Kazi,uchumi na uwekezaji akitoa taarifa kuhusina na maonesho ya kazi zinazofanywa na taasisi za umma na binafsi kupitia magari.
PICHA NA FAUZIA MUSSA – MAELEZO