WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayofikiwa nchini, hivyokuliwezesha Taifa kuendelea kupata utulivu, maelewano na kasi kubwa ya maendeleo kupitia maono, maelekezo na mipango mbalimbali.
“Sisi wana-Ruangwa tunatoa shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa Wilayani na Kitaifa. Kwa hakika Mheshimiwa Rais amekuwa kielelezo cha misingi ya uongozi na utawala bora, hivyo sisi Wana – CCM tunaendelea kutembea kifua mbele na tunamuhakikishia kuwa mazingira aliyoyaweka yatatuwezesha kushinda chaguzi zote za Serikali za Mitaa mwaka huu 2024 na zile za Uchaguzi Mkuu za mwaka 2025.”
Mheshimiwa Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi ameyasema hayo leo (Jumanne, Januari 2, 2024) kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM wa wilaya ya Ruangwa uliofanyika katika Uwanja wa Likangara, Ruangwa ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Abdulrahman Kinana.
Waziri Mkuu ametaja baadhi ya masuala makubwa ya Kitaifa yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani ni pamoja na kuendeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa wa Reli ya Kisasa na madaraja makubwa likiwemo la Kigongo – Busisi ili kukuza uchumi, kuongeza fursa za ajira na kufikia malengo yaliyokusudiwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Waziri Mkuu amesema mafanikio mengine ni kurejesha taswira ya Tanzania katika medani za kimataifa na kuimarisha diplomasia ya uchumi. “Kwa kufanya hivi Mheshimiwa Rais, amefungua fursa mbalimbali ukiwemo uwekezaji, mitaji, masoko ya bidhaa, ongezeko la watalii, kubidhaisha lugha ya Kiswahili na utatuzi wa changamoto za kibiashara na nchi jirani.”
Pia, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais, ameiwezesha nchi kuwa na mtangamano wa kisiasa unaojumuisha siasa safi, za kistaarabu na zinazoheshimu mawazo ya kila mmoja wetu, hatua ambayo imefanya hali ya siasa nchini kuwa tulivu chini ya sera ya upatanishi, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi wa nchi aliyoipa jina la 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuilding), kwa Kiswahili ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi wa Taifa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana wilayani Ruangwa tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani ni pamoja na uboreshwaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na kilimo na hivyo kuwawezesha wananchi kupata maendeleo.
Akizungumzia huduma za afya, Waziri Mkuu amesema Serikali imewezesha ujenzi wa hospitali ya wilaya; ujenzi wa vituo vya afya vipya vinne katika kata za Malolo, Nangurugai, Narungombe na Namichiga; Ujenzi wa zahanati mpya tisa za Namungo, Mbangara, Muhuru, Namkatila, Mkaranga, Mihewe, Lipande, Mkutingome na Mtakuja na hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma karibu na makazi yao na kwa wakati.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Ndugu Abdulrahman Kinana amesema kasi kubwa ya kupeleka maendeleo inayofanyika Ruangwa ni ya kupigiwa mfano hivyo amewasihi wananchi kuendeleza umoja na mshikamano katika kujiletea maendeleo ya kweli.
Ndugu Kinana amesema maendeleo makubwa yanayoendelea kufanyika wilayani Ruangwa yanatokana na kazi nzuri inayofanywa na Mbunge wa Ruangwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Majalwa ambaye amekuwa kiungo cha karibu anayewaunganisha wananchi, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa Serikali.
“Mimi nitakuwa shahidi wa kusimulia kazi nzuri ya maendeleo inayofanywa Ruangwa. Mimi natembea mara nyingi nchi nzima, nimewahi kupita Ruangwa miaka ya 1980 na 2000 lakini Ruangwa ya leo ni tofauti kabisa na Ruangwa niliyowahi kuiona huko nyuma. Nawapongezeni wana Ruangwa kwa umoja na mshikamano wenu,” amesisitiza.
Pia, Ndugu Kinana ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Sulu Hassan kwa kuendelea kufikisha maendeleo katika maeneo mbalimali na kumfanya avunje rekodi kwa kufikisha fedha nyingi za maendeleo katika halmashauri zote nchini. “Ndugu zangu sifa mnazompa Rais anastahili kwa kuwa anafanya kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo Watanzania.”