Moja ya vituo vya kuchotea maji(DPS)kinachjengwa katika kijiji cha Mchonda wilayani Nachingwea.
Na Muhidin Amri,
Nachingwea
SERIKALI imetenga Sh.milioni 331 kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji Naipingo utakowanufaisha zaidi ya wakazi 3,000 wa kijiji cha Mchonda kata ya Mchonda wilayani Nachingwea.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilayani humo Timoth Kitinga alisema,mradi huo unatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani(force akaunti) kwa lengo la kuboresho huduma ya maji kwa wakazi wa kijiji cha Mchonda ambao kwa muda mrefu hawana huduma ya maji ya uhakika.
Alitaja kazi zinazotekelezwa ni kujenga tenki la lita 150,000,kujenga vituo vya kuchotea maji vitano,kuchimba mtaro na kulaza mabomba urefu wa kilomita 5.5 na kujenga nyumba ya mashine ya kusukuma maji na kwa sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 95.
Alisema,mradi huo ni miongoni mwa miradi 8 inayotekelezwa na Ruwasa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na utakapokamilika utawezesha wananchi kuondokana na mateso ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwenye mito na mabonde.
Kitinga alisema awali wananchi wa kijiji hicho na vijiji vingine wilayani humo, wanategemea kupata huduma ya maji kupitia chanzo cha Mbwinji,hata hivyo wakati wa kiangazi kinapokauka wanaangaika kwa kukosa huduma muhimu ya maji.
Katika hatua nyingine Kitinga alisema,Ruwasa ilipoanzishwa mwaka 2019 upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika wilaya ya Nachingwea ulikuwa ni asilimia 57.5, lakini kwa muda wa miaka minne wametekeleza miradi 18 iliyoongeza upatikanaji wa maji hadi kufikia asilimia 67.5.
Aidha alisema kuwa,kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hakuna miradi mipya itakayotekelezwa, badala yake nguvu kubwa itatumika kukamilisha miradi viporo iliyoanza kujengwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yenye thamani ya Sh.bilioni 4.5.
“kwa mwaka wa fedha 2023/2024 tumetengewa Sh.bilioni 1.5 ambazo zitatumika kukamilisha miradi viporo 8 tuliyoanza kuitekeleza kwa mwaka 2022/2023,kati ya miradi hiyo 6 inatekelezwa na wakandarasi na 2 inatekelezwa na wataalam wa ndani”alisema.
Alieleza,miradi yote itakapokamilika itaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kutoka asilimia 67 ya sasa hadi asilimia 80 kwa wakazi takribani 233,000 wa wilaya hiyo.
Ahmad Hamis mkazi wa kijiji cha Mchonda,ameishukuru serikali kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji ambao utakuwa mkombozi wa huduma ya maji kwenye makazi yao.
Alisema,kwa muda mrefu wamekuwa na adha ya kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama,hali inayowalazimu kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwenye mito na visima vya asili vilivyochimbwa tangu miaka 80.
Diwani wa kata ya Mchonda Exvia Tambula,ameiomba serikali kupitia Tarura kuhakikisha wanakamilisha mradi huo haraka ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama na kufikisha mtandao wa maji ya bomba kwenye vijiji vingine vilivyobaki.