Na. Philipo Hassan, Arusha
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Friends of Serengeti yenye Makao Makuu yake nchini Switzerland imetoa ndege moja isiyo na rubani (Drone) pamoja na majaketi 170 ya askari kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori katika Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire leo tarehe 29.12.2023 makao makuu ya TANAPA yaliyopo mtaa wa Majengo jijini Arusha.
Akikabidhi vifaa hivyo mwakilishi wa Taasisi ya Friends of Serengeti Ndugu Suzy Shiyo alieleza kuwa taasisi yake itaendelea kuunga mkono shughuli za Uhifadhi na Utalii kwa kutoa vifaa mbalimbali vya kisasa na rafiki kwa mazingira ili kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii katika Hifadhi za Taifa nchini.
Aidha, Ndugu Suzy aliongeza kuwa “Tunatoa Ndege isiyo na Rubani (Drone) ambayo itasaidia kuimalisha ulinzi (doria) kwa kufichua majangili na kuokoa muda mwingi, kwani itakuwa na uwezo wa kuchunguza eneo kubwa na kwa gharama nafuu kuliko kutumia magari ambayo yangetumia mafuta mengi na nguvu kazi kubwa”.
Vile vile, Suzy aliongeza kuwa licha ya Drone hiyo, pia tumetoa majaketi 70 kwa Hifadhi ya Taifa Serengeti na mengine 100 kwa Hifadhi ya Taifa Tarangire, majeketi hayo yatasaidia kuwakinga askari na baridi nyakati za usiku na kipindi cha masika.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara – TANAPA Herman Batiho, akipokea vifaa hivyo aliishukuru Taasisi ya Friends of Serengeti na kusema, “TANAPA katika Mpango Mkakati wetu tumebainisha kulinda rasilimali kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo hii ya ndege zisizo na rubani, hivyo tuwashukuru sana kwa msaada huu.”
“Aidha, nikuhaidi Ndugu Suzy, Drone hii pia itatusaidia katika maeneo yenye migogoro baina ya wanyamapori na binadamu. Pindi itakaporushwa na kupiga picha maeneo hayo na kugundua kuna makundi ya tembo tutatuma kikosi cha askari wetu kwenda kuwarudisha mara moja wanyamapori hao,” aliongeza Kamishna Batiho.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Beatrice Kessy, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire aliishukuru taasisi hiyo kuendelea kusaidia katika Uhifadhi na kusema “Marafiki wa Serengeti leo wametukabidhi majaketi 100 kwa ajili ya askari wanaofanya doria katika hifadhi za Serengeti na Tarangire. Mwezi huu pia wametufungia huduma ya WiFi katika vituo viwili vya askari (Lobosireti na Kimotorok). Kwa kweli mmetuletea mapinduzi katika Uhifadhi, kwa kutuletea Drone tutafanya doria maeneo korofi ambayo yalikuwa hayafikiki kwa magari, hivyo tukuahidi wewe na taasisi yako kifaa hiki tutakilinda na kitafanya kazi kwa muda mrefu ili kikidhi matamanio yenu”.
“Vifaa hivi tunavyovipokea leo vitaleta hamasa na chachu katika kulinda rasilimali mali hizi muda wote, pawe na jua ama mvua, usiku au mchana tutapambana kuhakikisha kuwa vizazi kizazi cha sasa na kijacho kinafurahia uwepo wa TANAPA katika kutunza wanyamapori hao aliongeza Kamishna Kessy”.
Taasisi ya Friends of Serengeti imekuwa na mchango mkubwa ndani ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) tangu mwaka 1984. Taasisi hii imekita mizizi yake kwa kusaidia jitihada za Uhifadhi wa Maliasili nchini ambapo kwa sasa wanufaika wakuu ni Hifadhi za Taifa Serengeti na Tarangire, huku misaada mingi ikijikita katika masuala ya doria.