Moja ya tenki la kuhifadhia maji lililojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Kilwa mkoani Lindi kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
………………………..
Na Muhidin Amri
Kilwa
SERIKALI kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Kilwa mkoani Lindi,imetenga Sh.milioni 432,521,623.85 ili kutekeleza mradi wa maji Hotelitatu unaotarajia kuhudumia zaidi ya wakazi 2,703 wa kijiji hicho.
Kaimu meneja wa Ruwasa wilayani Kilwa Mhandisi Msomi Lunjilija alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Disemba 2022 na kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 95.
Alisema,mradi huo unahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita 75,000 kwenye mnara wa mita 9,ujenzi wa kibanda cha mashine(Pump House) kufunga umeme,kujenga vituo vya kuchotea maji 8,uchimbaji wa mitaro na kulaza mabomba urefu wa kilomita 5.45.
Kwa mujibu wa Msomi, chanzo cha mradi huo ni kisima chenye urefu wa mita 130 ambacho kina uwezo wa kuzalisha lita 6,600 kwa saa na kinatosheleza mahitaji ya maji kwa watu wote waliopo katika kijiji hicho.
Alisema,mahitaji ya maji kwa wakazi 297,676 wa wilaya ya Kilwa ni lita za ujazo 12,187,380 kwa siku na uzalishaji halisi ni lita 7,617,122.5 hivyo kuwa na upungufu wa lita 4,570,267.5 na watu wanaopata maji safi na salama ni 189,620 sawa na asilimia 63.7.
Aidha alieleza kuwa,kabla ya kuanzishwa kwa Ruwasa mwaka 2019 hali ya upatikanaji wa huduma ya maji wilayani humo ilikuw asilimia 38 tu na kulikuwa na miradi 14 ya maji ya bomba na visima vifupi.
“lakini katika kipindi cha miaka minne tumefanikiwa kujenga miradi mipya 8,kufanya upanuzi wa miradi 2 na kukarabati miradi 5 ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 38 hadi kufikia asilimia 63.7”alisema Msomi.
Mkazi wa kijiji cha Hotelitatu Salma Kinewa,ameiomba Ruwasa kukamilisha ujenzi wa mradi huo haraka ili waweze kuondokana na adha ya huduma ya maji inayowakabili kwa muda mrefu.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Seleman Ndumbo,ameipongeza serikali kutoa fedha na wataalam wa Ruwasa kwa usimamizi wa mradi huo unaotarajiwa kumaliza kero ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji cha Hotelitatu.