Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Disemba 28
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge, ametoa agizo kwa wakuu wa shule na bodi za shule wasiwe kikwazo , kuwazuia wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2024 wasipokelewe shule ,kwa sababu yeyote ile.
Aidha ametoa agizo jingine kwa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za chini, wahakikishe wanafuatilia wanafunzi hao ,wanaripoti shule kwa wakati ,na ambae atashindwa kusimamia maagizo hayo atawajibishwa .
Akizungumza katika Kikao cha wadau wa elimu mkoa kilichofanyika Disemba 28,mwaka 2023 ,Kunenge alisisitiza endapo atasikia ama akifika na kukuta mtoto hasomi basi kiongozi wa eneo husika atawekwa pembeni.
“Haiwezekani mshindwe kusimamia suala la elimu hadi mkuu wa Mkoa ama mkuu wa wilaya afike kushughulikia tatizo hilo, haiwezekani kuona watoto hawaendi shule,wanakaa chini,wanasoma chini ya miti na kukuta changamoto hizi kwenye mitandao, na viongozi mpo,tutaanza na wewe!!!”
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan anapambana kuinua sekta ya elimu ,kuona watoto wanasoma na kutoa kipaombele kwa watoto wa kike bila kuwabagua ,anajitahidi kuongeza miundombinu ya madarasa, majengo na kuweka fedha katika sekta hii,Tusimwangushe” anaeleza Kunenge.
Kunenge pia aliwaasa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule, na wanaripoti shule kwa wakati.
Vilevile ,mkuu huyo wa mkoa alisema, elimu ni sehemu ya mkakati katika mkoa ,ni sehemu ya uwekezaji na viwanda kwani watoto wanaweza kutumia fursa ya Viwanda kujisomea kwa vitendo.
Kadhalika, mkoa umejiwekea mkakati, shule ya Sekondari ya wasichana wenye vipaji ya Bibi Titi Mohammed iliyopo Utete, Rufiji iwe shule inayofanya vizuri katika masomo ya sayansi
Akijinasibu kuhusiana na ufaulu na mafanikio ya sekta ya elimu mkoa ,kwa mwaka 2023, alieleza mkoa huo, umefanya vizuri katika ufaulu wa darasa la 7 kwa asilimia 83.72 ,daraja A ,mkoa ukiwa juu kwa wastani wa kitaifa 3.4.
Pamoja na hilo ,darasa la kwanza na la pili Mkoani humo wamefanya vizuri katika KKK ,kati ya mikoa 26.
Awali ofisa elimu mkoa wa Pwani,Sara Mlaki , alieleza kwa mwaka 2023 wanafunzi wa darasa la saba 41,028 wamefaulu kujiunga na kidato cha kwanza January 2024.
Alieleza, idadi hiyo inajumuisha wanafunzi 189 wenye mahitaji maalum.
Sara alieleza, wanafunzi 238 wamepangiwa shule za Sekondari za bweni na wengine 40,458 wamepangiwa shule za Sekondari za kutwa.