Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutambua mchango wake wa kuifungua nchi kiuchumi kupitia Sekta ya Utalii wakati wa Mahafali ya 19 ya Chuo hicho yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Kampasi ya Tunguu tarehe 28 Desemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Viongozi pamoja na wageni mbalimbali mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kutambua mchango wake wa kuifungua nchi kiuchumi kupitia Sekta ya Utalii kwenye Hafla ya Mahafali ya 19 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Kampasi ya Tunguu tarehe 28 Desemba, 2023.
……………………
Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya Usimamizi wa Utalii na Masoko katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Tunguu Zanzibar.
Shahada hiyo ya Heshima ya Uzamivu ya Usimamizi wa Utalii na Masoko ametunukiwa leo desemba 28,2023 katika Mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt Shein Kampasi ya Tunguu ambapo Mgeni rasmi alikua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali mwinyi.
Akizungumza mara baada ya kutunukiwa Shahada hiyo, Rais Samia amesema alipokea barua ya pendekezo la kutunukiwa shahada hiyo ambapo alitaka kujua alichofanya Zanzibar hadi kufikiwa uamuzi huo huku akiahidi kuendelea kusaidia sekta ya elimu ili kuendana na kasi ya teknolojia.
Amesema ameimarisha mashirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi hasa ndani ya sekta ya utalii, kuvutia hoteli zenye majina ya kidunia kwa kuanzisha uwekezaji ikiwemo Kempisk, Lagema, Zuri Residence, kuitangaza Zanzibar kituo kizuri cha utalii, kuanzisha mchakato ya kuifanyia marekebisho bustani ya forodhani, kubuni mikakati ya kuifungua sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal Tour.
Amesema licha ya filamu hiyo, alifanya filamu nyingine ijulikanayo kama Kijiji cha milele ambayo itatoka hivi karibuni dhamira ikiwa kuletea maendeleo wananchi na kuimarisha ustawi wao.
“Ukiona vinaelea vimeundwa, ninapopokea heshima hii naipokea kwa ajili ya Watanzania wote wanaoendelea kunipa moyo na ushirikiano mkubwa katika kuitekeleza majukumu yangu kama Mkuu wa nchi,”amesema.
Amesema kwasasa hali ya Maisha ya nchi itategemea kutumia ujuzi na maarifa, kuendeleza afya na kuelimisha watu wake ambapo mwaka huu mapitio ya sera ya elimu na mitaala vimepitiwa upya.
Awali Rais, Dkt. Ali Hassan Mwinyi amesema katika mahafali hiyo, Chuo hicho kinajivunia mafanikio ambayo chuo hicho yanakipata kila mwaka hasa ongezeko la wahitimu katika fani zinazofundishwa chuoni hapo.
Amesema kwa mwaka wa masomo 2022/2023 wahitimu 2102 wanatunukiwa sawa na ongezeko la asilimia 9 ikilinganishwa na wahitimu 1913 kwa mwaka jana.
Ameseam Chuo hicho kitaendelea kuwa bora kwa kuandaa vijana mahiri na wenye weledi kitaaluma, uzalendo na wema watakaotoa mchango muhimu katika sekta mbalimbali za maendeleo na kuhimili ushindani katika soko la ajira.
“Serikali zetu zote mbili, tumejiandaa kuhakikisha kuwa vijana wote wenye sifa za kujiunga na vyuo vikuu wanapatiwa mikopo ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao,”amesema.
Aidha Rais Dkt Samia amezipongeza bodi za Mikopo pande zote mbili kushirikiana na kuhakikisha vijana waliodahiliwa vyuo vikuu na wanaohitaji mikopo wanapatiwa mikopo hiyo.
Amehimiza kuendelea kufanya tafiti zenye lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto zinazo ikabili jamii na kutoa ushauri wa kitaalamu.
Amesema yapo mafanikio yanayopatikana katika Chuo hicho, zipo changamoto zinazoathiri ufanisi ikiwemo uhaba wa wataalamu na rasilimali watu,uhaba wa miundombinu ya majengo ikiwemo ofisi na maabara ambapo
“Uongozi wa Chuo unafanya jitihada katika kutatua changamoto zinazoikabili chuo, ikiwemo upanuzi wa chuo utakaoondoa changamoto ya miundombinu na mahitaji mengine.
“Suala la rasilimali watu, serikali inampango wa kuongeza rasilimali watu katika taasisi za elimu ya juu ikijumuisha wahadhiri, wakutubi na wataalamu wa maabara lengo kukidhi mahitaji ya viwango vya ubora wa elimu kama iliyoelezwa katika ilani ya Uchaguzi 2020/2025,”amesema.
Amefafanua kuwa Chuo hicho kimekua miongoni mwa vyuo vya elimu ya juu, vinavyonufaika na mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya uchumi.
“Niwatake kuitumia fursa hii vizuri ili tukiongezee uwezo chuo chetu uwezo wa kuendesha program zitakazokwenda sambamba na mahitaji ya soko na jamii.
“Lazima tujipange kusomesha walimu kwa madhumuni ya kwenda na mabadiliko ya mitaala ya kitaaluma,”amesema.
Amesema mradi huo unakwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu, ambapo amewataka kusimamia vema fedha zilizotolewa ili ipatikane thamani halisi ya majengo na kuondokana na uhaba wa majengo katika chuo hicho.
Viongozi pamoja na wageni mbalimbali wakiwa kwenye Hafla ya Mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Kampasi ya Tunguu tarehe 28 Desemba, 2023.
Wahitimu katika ngazi mbalimbali wakiwa kwenye Hafla ya Mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Kampasi ya Tunguu tarehe 28 Desemba, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Dkt. Aman Abeid Karume katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Kampasi ya Tunguu walipohudhuria Hafla ya Mahafali ya 19 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) tarehe 28 Desemba, 2023.