Akizungumza wakati wa kikao baina ya menejimenti ya Chuo hicho Kikuu Mzumbe na Kampuni hiyo ya Y & P Architect kupokea na kupitisha rasimu ya michoro ya ujenzi wa miundombinu ya majengo unaotekelezwa na serikali kupitia mradi wa HEET Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. William Mwegoha amesema pamoja na kuzingatia ubora mradi huo unapaswa kukamilika kwa wakati.
“Hii ni kazi muhimu katika chuo chetu kwa sababu itakapo kamilika itatuongezea huduma kwenye chuo chetu ambayo mwisho wa siku ni mkakati wa kuongeza masuala ya Udahiri , mifumo ya TEHAMA, masuala ya kuendeleza bunifu na matumizi ya Mtandao kuwezesha mafunzo ya masafa” . Alisema Prof. William Mwegoha makamu mkuu wa chuo kikuu Mzumbe
Katika kikao hicho kampuni ya Y & P Architect imewasilisha rasimu ya michoro ya majengo matatu ya.Academic Complex, TEHAMA na Uvumbuzi pamoja na jengo la Mgahawa (Cafteria) yanayotarajiwa kujengwa eneo la Maekani Kampasi kuu Morogoro.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Y & P Architect, Yasin Mringo, ameishukuru Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa ushirikiano uliosaidia kuwa na ufanisi hadi hatua iliyofikiwa ambapo pamoja na kupokea mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya maboresho ameahidi kuongeza kasi kwenye utekelezaji wa shughuli zilizobaki kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika mapema hata kabla ya muda wa mkataba.
“Tumekwisha kamilisha hatua ya kwanza tunashukuru mungu leo kwa kushirikiana na Uongozi wa chuo kikuu Mzumbe baada ya sikukuu hizi za mwisho wa mwaka kupita nimategemeo yetu kwamba katika kipindi cha miezi miwili na nusu ya kufanya kazi tutakamilisha mategemeo yetu ili kufikia mwezi wa Nne au watano mkandarasi kwa ajili ya ujenzi awe amepatikana”. Alisema Msanifu Majengo Yasin Mringo.
Mkataba wa huduma ya Ushauri Elekezi, Usanifu na usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho uliosainiwa Oktoba 9,2023 baina ya Chuo kikuu Mzumbe na kampuni ya Y & P Architect, sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa HEET kuboresha miundombinu ujenzi wa majengo eneo la chuo kikuu Mzumbe, pia kuanza mchakato wa ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo hicho katika mkoa wa Tanga.