Na Mwandishi Wetu
MIKOA ya Morogoro na Tanga imepewa kipaumbele cha kulima zao la karafuu katika mpango wa pamoja wa serikali na wadau wa kilimo kutoka sekta binafasi na taasisi zisizo za kiserikali.
Ongezeko la Mkoa wa Tanga katika ulimaji wa karafuu kitaifa limetangazwa katika Mkutano wa Wadau wa Kilimo na Mazingira waliokutana jijini Dar es Salaam.
Wadau hao wamesema zao la karafuu limeonesha kustawi katika mikoa hiyo miwili, hivyo waamini ikipewa kipaumbele itaongeza uzalishaji.
“Morogoro ndiyo iliyotangulia na mwaka jana tu ilizalisha tani 2,000 sawa na nusu ya uzalishaji wa Zanzibar wa jumla ya tani 4,000, hivyo ongezeko la Tanga ni wazi Tanzania itakuwa mzalishaji mkubwa wa karafuu,” walisema wadau.
Ulimaji wa karafuu Tanzania Bara umetokana utafiti na ushauri wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), taasisi inayowashirikisha wadau katika sekta binafsi katika kulima mazao na kuendeleza minyororo ya thamani ya mazao hayo.
Akitangaza uamuzi wa kuiongeza Tanga kwenye mpango huo wa zao la karafuu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga, amewambia wajumbe wa jukwaa la Wadau wa Kilimo na Mazingira kwamba utafiti umeonyesha kuwa mkoa huo unaweza kulima kwa mafanikio zao la karafuu.
Kirenga ameeleza kuwa zao la karafuu ni zao la thamani kubwa na ni sehemu ya mazao muhimu ya viungo na pia ni muhimu katika mazao ya mboga, matunda, mizizi na maua (hortculture) ambayo yana masoko yanayaotabirika duniani.
Alisema endapo Watanzania watachangamkia fursa zilizomo katika ulimaji wa zao la karafuu, basi uchumi wa mkulima mmoja mmoja na wa Taifa utaimarika na kukifanya kilimo kiwe na tija.
“Mazao ya viungo hususani karafuu yamekuwa na soko imara na la uhakika. Sasa bei elekezi ya kilo moja ya karafuu ni kati ya shilingi 14,000 hadi 18,000. Bei hizi zinaonyesha ni jinsi gani zao hili likipewa kipaumbele litakavyokuwa na maana kwa mkulima mdogo na pia likawa ni zao letu lenye tija kubwa katika soko la kimataifa”, Kirenga alilieleza jukwaa hilo.
Aliongeza kuwa karafuu ni zao la msingi Zanzibar na wao ndiyo wazalishaji wakuu wa zao hilo, wana masoko makubwa na ya uhakika.
“Hivi karibuni Tanzania Bara imeanza kuzalisha zao hili katika baadhi ya mikoa miwili. Uzalishaji umekuwa na mwelekeo mzuri kwani mikoa hii sasa inazalisha kwa wingi zaidi karafuu ikilinganishwa na Zanzibar ambao ndio waanzilishi. Mikoa hiyo kwa sasa ni Morogoro na Tanga”, alisema Kirenga.
Sasa hivi serikali inawashirikisha wadau wengine kuinua pato la Mtanzania kufikia dola za Marekani 3,000 kabla ya mwaka 2025.
Tanzania sasa inahesabiwa kuwa nchi yenye uchumi wa kati wa chini baada ya pato la Mtanzania kuvuka dola za Marekani 1,096, kigezo kinachotumiwa na Benki ya Dunia katika kupima umaskini wa watu katika taifa lao.
Ili kulifanya zao la karafuu likubalike kwa wakulima Mkoa wa Morogoro na SAGCOT wameshirikiana serikali ya mkoa kuwapeleka Zanzibar wakulima 20 wa Morogoro kujifunza ulimaji wa zao hilo.
Tayari ulimaji wa zao hilo umeimarika katika Wilaya za Morogoro Vijijini, Kilombero; katika Halimshauri ya Wilaya ya Mlimba na sasa imeongezeka Wilaya ya Mvomero.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli, ameeleza uingizaji wa kilimo cha karufuu katika mkakati wa kuinua pato la mkulima una maana kubwa kwa wilaya yao.
Alisema ulimaji wa zao hilo unawaletea wakulima fursa tele na kwani wadau wamejizatiti kuunga mkono ulimaji wa zao katika wilaya yao.
“Wilaya yetu imekuwa ikiathiriwa na kilimo kisichokuwa na tija. Uwepo wa mazao kama haya ya kimkakati utapelekea kuinua maisha ya mwananchi mmoja mmoja. Tumethibitishiwa kuwa ardhi yetu itasitawisha zao la karafuu kama tutazingatia maelekezo ya wataalamu,’’ alisema Nguli.
Meneja wa SAGCOT, Mkoa wa Morogoro, John Banga alieleza kuwa Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyopewa kipaumbele cha kuzalisha kilimo cha mazao ya viungo, na hasa karafuu, huku akianisha sababu zake ni kwamba mkoa una hali ya hewa inayofaa na afya ya udongo ni himilivu kwa zao la karafuu.
“Ndani ya miezi miwili wakulima wamegawiwa zaidi ya miche 150,000 ili waweze kuendeleza kilimo cha karafuu. Jambo kubwa na zuri wapo wadau ambao wamekuja kuunga mkono juhudi hizi za kulima karafuu katika milima ya Morogoro. Kilimo cha karafuu kwa njia hii kitasaidia katika kutunza afya ya mazingira ya misitu. Tutajiepusha na uchomaji wa maeneo na ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa,’’ alisema Banga.