Meneja katika idara ya Kinga -Taasisi ya Saratani Ocean Road,Dk.Maguha Stephano akizungumzia kuhusiana na kampeni hiyo mkoani Tanga.
Wananchi mbalimbali wakisubiri kupatiwa huduma hiyo bure mkoani Tanga .
…………………………
Happy Lazaro,Tanga.
Tanga.Zaidi ya Wananchi 2000 kutoka wilaya mbili za Handeni na Mkata mkoani Tanga wamefikiwa na huduma ya kampeni ya uchunguzi wa saratani bure iliyofanyika kwa kipindi cha wiki moja huduma inayotolewa na Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Tanga,Meneja katika Idara ya Kinga – Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Maguha Stephano amesema kuwa ,kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani ambapo zaidi ya asilimia 75 wanaofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu wanafika wakiwa wamechelewa.
Amesema kuwa, kutokana na changamoto hiyo inapelekea wengi kupoteza maisha na pia kujenga imani potofu dhidi ya tiba za saratani.
Amefafanua kuwa,saratani ikigundulika katika hatua za awali inatibika na hii imepelekea Taasisi hiyo kuona haja ya kuwa na hizi huduma mkoba za kuwafuata wananchi katika Mikoa yote nchini huku lengo likiwa ni kutoa elimu kwa wananchi ya jinsi ya kujikinga na saratani.
“Pia mbali na kutoa vipimo tunalenga kuwaelimisha na kuwahimiza kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi mara kwa mara hata kama hawana dalili za ugonjwa huo na hii itasaidia saratani kugundulika mapema na kupata matibabu sahihi.”amesema.
Ameongeza kuwa,lengo lingine ni kuwajengea uwezo watoa huduma katika hospitali za Rufaa za Mikoa, wilaya na vituo vya afya kuwa na uwezo wa kugundua dalili za awali za saratani na kuweza kutoa rufaa mapema kwenda katika hospitali za kibingwa za saratani.
“Tunapenda wananchi wafahamu kuwa kuanzia desemba 10 hadi 11 tutatoa huduma Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Mkata ambapo kuanzia desemba
12 hadi 13 tutakuwa Kituo cha Afya Kabuku na desemba 14 tutakuwa Kituo cha Afya Kideleko huku desemba 15 hadi 16 tutakuwa Hospitali ya Wilaya Handeni Mjini.”amesema Dk Maguha.
Aidha ametoa wito kwa wananchi mbalimbali mkoani Tanga kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo ili waweze kutambua afya zao mapema na kuweza kuchukua tahadhari kwani wengi wanakabiliwa na changamoto hiyo ila hawajijui kabisa kutokana na kutokuwa na tabia ya kupima mara kwa mara.