Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu (SMZ) Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jingo jipya la maabara ya kisasa ya wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi (ZFDA) huko Mombasa ikiwa NI miongoni mwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
……………………..
Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu Mhe. Balozi Seif Ali Iddi amewataka wananchi kutumia vyakula na dawa zenye kiwango ili kuzilinda Afya zao.
Akifunguwa Jengo la Maabara ya Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar ZFDA huko Mombasa Wilaya ya Magharibi ‘B’.ikiwa ni miongoni mwa Shamra Shamra za Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema utumiaji wa dawa na vyakula ambavyo havina kiwango vitasababisha madhara ya kiafya kwa mtumiaji na kuipatia hasara Serikali kwa kutoa gharama kubwa ya matibabu
Aliwataka wafanyakazi wa Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi kuvitunza vifaa vya maabara walivyowekea pamoja na kutoa huduma kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Mhe.Balozi aliwafahamisha kwamba waendeleze kudumisha nidhamu wakati wa kazi ili kuwa na bidii uhakika na haki bila ya kumuonea mfanyabiashara yeyote Jambo ambalo litaongeza ufanisi wa majukumu yao.
Nae Waziri wa Afya Mhe. Nassour Ahmed Mazrui amesema maabara imejengwa kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa ambayo vitachunguza dawa na vyakula pamoja na bidhaa zinazozalishwa ndani na nje ya nchi ili kuona ubora na usalama wa bidhaa hizo
Alieleza kuwa Wawekezaji wanaokuja kuekeza bidhaa za vyakula na viwanda wataridhika kuona maabara yenye hadhi kubwa ya kimataifa .
Mapema Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) Burhan Othman amesema kukamilika Kwa maabara hiyo kutasaidia kuengeza nyanja za uchunguzi ambapo awali kulikuwa hakuna uwezo huo, pamoja na kurahisisha mzunguko kwa wafanyabiashara .
Amesema jengo la maabara ya ZFDA ni la Kwanza kwa hapa Zanzibar na lina ghorofa tatu zimejengwa kupitia pesa za mradi wa maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika awamu mbili ya kwanza mradi ulitumia Tshs Bilioni 5.4 Kwa ajili ya jengo na Bilioni 4.4 Kwa ajili ya vifaa.
Ujenzi huo ulianza Machi 2019 na kukamilika Juni 2022 na mchakato wa manunuzi ya vifaa vya maabara hiyo ulianza Julai 2022 na kukamilika Disemba 2023.