Na. WAF – Dar es Salaam
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameitaka Taasisi ya Saratani Ocean Road hadi kufikia Fubruari Mosi, 2024 mashine ya Pet-CT Scan iwe imeanza kutoa huduma kwa Watanzania ili rufaa za kwenda nje ya nchi zipungue.
Waziri Ummy ametoa tamko hilo Disemba 21, 2023 baada ya kufanya ziara ya kujionea huduma zinazotolewa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road jijini Dar es Salaam.
“Mmeniambia tarehe 26, Disemba mtafanya majaribio ya mashine hii sasa nataka nikija tena hapa tarehe 01-02-2024 nione mashine ya Pet-CT Sacan iwe imeanza kufanya kazi Ili Watanzania waweze kupata huduma za Pet-Ct Scan hapa nchini.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali Afya za Watanzania kwa kuipa fedha Sekta ya Afya kwa ajili ya matibabu ikiwemo ya Saratani Pamoja na Vifaa Tiba.
Amesema, kwa sasa wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa udhamini wa Serikali ni wagonjwa 42 wakiwemo wa Saratani wagonjwa 15 kwa muda wa miezi Mitatu kuanzia Julai hadi September Mwaka huu.
“Tunataka kupunguza Rufaa za nje ya nchi ili kusogeza huduma kwa Watanzania lakini pia kuokoa fedha za Serikali na tutaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za Saratani nchini.” Amesema Waziri Ummy
Pia, Waziri Ummy ameitaka Taasisi ya Saratani Ocean Road kwenda kuwajengea uwezo wataalamu waliyopo katika Hospitali za Rufaa za Kanda pamoja na Hospitali za Rufaa za Mikoa hususan huduma za mkoba kwa kuwa Taasisi hiyo ni kituo cha umahiri wa Masuala ya Saratani nchini Tanzania.
Vilevile, ameitaka Taasisi hiyo kuharakisha harakati za kufungua vituo katika Mkoa wa Mbeya na Dodoma ili watu wanaotaka kupata huduma za mionzi wazipate kwa haraka.
Waziri Ummy ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma za Saratani kwa Watanzania na amewahakikishia kuwa Serikali itatimiza wajibu wake ili wafanye kazi katika mazingira rafiki.
Mwisho Ametoa wito kwa Watanzania kuwa na tabia ya kupima Afya zao mara kwa mara ili kujua hali zao za kiafya mapema na kuanza kupata huduma mapema kama umekutwa na ugonjwa ikiwemo Saratani.