Vyoo vipya vya wavulana katika shule ya sekondari Frank Weston wilayani Tunduru baada ya kujengwa upya na Halmashauri ya wilaya Tunduru.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Chiza Marando,akitoa taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya elimu katika Halmashauri hiyo. ……….
Na Muhidin Amri, Tunduru
KILIO cha wanafunzi wa shule ya sekondari Frank Weston wilayani Tunduru kuhusu ubovu wa vyoo ,kimepata ufumbuzi baada ya Halmashauri ya wilaya na wadau mbalimbali kujitokeza kwa kujenga vyoo vya kisasa.
Awali wanafunzi wa shule hiyo, walilazimika kurudi nyumbani na wengine kwenda vichakani na kuacha vipindi darasani kila wanapotaka kujisaidia kwa kuhofia usalama wao.
Wameishukuru serikali,kwa kujenga vyoo vipya ambavyo vimewaondolea kero iliyokuwepo kwa takribani mwaka mmoja na kusababisha kukosa vipindi madarasani.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao Salum Mtipwa alisema,changamoto ya vyoo hasa kwa upande wa wavulana ilikuwa mbaya hali iliyopelekea wakati mwingine kurudi nyumbani au kuomba kujisaidia nyumba za majirani.
“vyoo hivi sasa ni vizuri na vina usalama wa mkubwa pamoja na maji,tunaishukuru sana Halmashauri yetu ya wilaya kwa kutujengea vyoo vipya”alisema.
Mwanafunzi mwingine Divia Sa d wa kidato cha tatu alisema,kabla ya vyoo vipya walipata shida kubwa kila wanapohitaji kwenda chooni kutokana na ubovu wa vyoo vya zamani ambavyo licha ya ubovu wake pia hakukuwa na huduma ya maji.
Alieleza kuwa,walishindwa hata kujisafisha wanapotoka kujisaidia jambo lililopelekea baadhi ya wanafunzi wenzao kukumbwa na magonjwa ya mara kwa mara.
Kwa upande wake makamu mkuu wa shule hiyo Michael Chuwa,ameishukuru serikali kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru kuwapatia fedha zilizowezesha kujenga vyoo vipya kwa ajili ya wanafunzi.
Alisema,hapo awali mahudhurio ya wanafunzi wa shule hiyo hayakuwa mazuri kwa kuwa baadhi ya wanafunzi walihofia usalama wao kutokana na ubovu wa vyoo na wengine kupata magonjwa ya mara kwa mara.
Alisema,kwa sasa katika shule hiyo kuna mahudhurio mazuri kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi waliovutiwa na kujengwa kwa vyoo vipya vilivyosaidia kupunguza kero ya kurudi nyumbani wakati wa masomo kila wanapotaka kujisaidia.
Aidha,amemshukuru Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka kwa kuchangia mifuko 70 ya saruji na waandishi wa Habari walioibua changamoto ya vyoo katika shule hiyo.
Kaimu afisa elimu sekondari wilaya ya Tunduru Mwanahamis Mwango alisema,Halmashauri ya wilaya imetoa Sh.milioni 15 ili kujenga vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa kiume,hivyo kuwaondolea usumbufu wanafunzi shule hao kurudi nyumbani na wengine kwenda vichakani wanapotaka kujisaidia.
Mwango,amewashukuru wadau na wazazi waliojitokeza na kushiriki katika ujenzi wa vyoo hivyo ambavyo vimesaidia kupunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi.Pia alisema, Halmashauri ya wilaya Tunduru imeanza kutekeleza mpango wa kuboresha miundombinu katika shule mbalimbali za sekondari ikiwemo matundu ya vyoo kwa shule zote za sekondari.