Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Prof. Lazaro Busagala
…………………..
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imefanya ukaguzi wa matumizi salama ya mionzi katika vituo 66 ndani ya Halmashauri ya ilala katika Jiji la Dar es salaam.
Katika ukaguzi huo vituo 54 vimekidhi matakwa ya kisheria na kuruhusiwa kuendelea kutoa huduma na vituo 12 vimebainika kukiuka sheria na taratibu za matumizi salama ya mionzi katika kutoa huduma kwa wananchi.
Vituo 12 vyenye mapungufu vimechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ili kuwalinda wananchi kutokana na madhara ya mionzi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mtaalamu wa mionzi wa TAEC Bw. Peter Mammba amesema lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha matumizi ya mionzi nchini yanakuwa salama ili kuwalinda wagonjwa, wafanyakazi, wananchi na mazingira.
Baada ya kupokea ripoti ya ukaguzi huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Rehema Madenge ameipongeza Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania kwa kuendesha zoezi la ukaguzi na akaitaka Tume kuongeza nguvu ya ukaguzi ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama dhidi ya matumizi ya mionzi.