Naibu Waziri wa elimu sayansi na teknolojia Omary Kipanga akizungumza katika mahafali hayo ya 15 chuoni hapo.
Mkuu wa Chuo cha ufundi Arusha ,Dk Mussa Chacha akizungumza chuoni hapo.
Baadhi ya wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi pamoja na uongozi wa chuo hicho mkoani Arusha.
……
Julieth Laizer,Arusha
Arusha. Naibu Waziri wa elimu sayansi na teknolojia Omary Kipanga amesema kuwa ,serikali imetenga fedha zaidi ya bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA kwenye halmashauri 64 nchini ambazo hazina vyuo hivyo ili wataalam wazidi kuzalishwa zaidi kusaidia nchi kuwa na wataalam wa kutosha lakini pia kupunguza kizazi kisicho na ajira miaka ijayo.
Kipanga ameyasema hayo jijini Arusha, kwenye mahafali ya 15 ya chuo cha ufundi Arusha kilichofanikisha wahitimu 833 kutunukiwa shahada, astashaha na shahada ya juu katika fani mbali mbali za teknolojia na uhandisi hasa ujenzi, uzalishaji Mali na nishati.
Amesema lengo la serikali kujenga vyuo hivyo ni kuhakikisha tunajikita katika kuzalisha wataalam kwenye maswala ya Tehama watakaosaidia kuratibu mipango yetu ya maendeleo lakini vile vile ya kidigitali tunakoelekea kiuchumi “ameongeza.
Amesema yote hayo yanatokana na miradi mingi mikubwa ambayo serikali inatekeleza nchini kukosa wataalam wa ndani ikiwemo treni ya mwendo kasi, ndege , meli na hata vivuko.
Hata hivyo ametoa rai kwa vyuo vya kati na vya ufundi (VETA) nchini kuhuisha mitaala yao kwa mwaka wa masomo 2024.
“Kitendo cha kufanya hivyo ni kusaidia mafunzo wanayoyatoa yaendane na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya soko la ajira hasa sekta ya uzalishaji.”amesema.
Amesema viko baadhi ya vyuo vinatoa elimu ya miaka ya 90 kurudi nyuma na kushindwa kutekelezeka sera ya serikali ya kuzalisha wataalam watakaofaa kutumika kwenye sekta ya uzalishaji au kuleta ushindani kwenye soko la ajira Afrika mashariki.
Kipanga amesema kuwa iko haja ya vyuo hivyo kuendelea kuboresha mitaala ikiwemo kuhuisha ya zamani na kuleta mipya itakayozalisha wahitimu wenye sifa katika soko la ajira katika nchi za Afrika mashariki lakini pia sekta za uzalishaji nchini hasa viwanda.
“Mitaala hiyo ilenge kutoa elimu bora inayolenga wahitimu kuwapa uwezo wa kushindana kwenye soko la ajira au ubunifu wa kujiajiri ndani ya nchi za Afrika mashariki” amesisitiza
Kipanga akaongeza kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa vyuo vya kati na ufundi, Rais Samia kwenye sekta ya ufundi na ufundi stadi ametafuta fedha kwenye Benki ya dunia kwa ajili ya mafunzo ya umahiri wa wataalam mbali mbali nchini.
“Ipo miradi mingi imeanzishwa nchini lakini inakosa wataalam kama treni ya mwendo kasi hakuna wahandisi, tuna ndege ambazo zimeshanunuliwa lakini hakuna hawandisi na pia kuna meli na vivuko vingi ambayo serikali imewekeza fedha nyingi lakini hakuna wataalam, ndio maana tunataka mitaala ihuishwe”
Awali mkuu wa chuo cha ATC, Dk Musa Chacha alisema jumla ya wahitimu 833 wamefanikiwa kumaliza kozi mbali mbali za teknolojia na uhandisi ikiwemo wa umeme, mitambo, maboma ujenzi, habari, barabara, Tehama tiba na nyinginezo.
Amesema kwa mwaka huu wamefanikiwa pia kuhuisha mitaala 16 na kuongeza mipya 8 Ili kuendana na hitaji la jamii hasa katika ajira na pia utaalamu wa changamoto mbali mbali katika jamii.
Dk Chacha pia amesema kuwa Ujenzi wa jengo la hospitali kwa ajili ya mafunzo na huduma ya afya chuoni hapo umefikia asilimia 97 na unatarajiwa kukamilika, mwezi wa pili mwaka ujao 2024 kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo mambo ya afya na pia itatumika kutibu wananchi magonjwa mbalimbali.
“Tunatarajia kuanza kutoa huduma ya uchunguzi wa afya, mama na mtoto, macho, mfumo wa pua, koo na masikio, meno, magonjwa ya ndani, huduma za upasuaji, na huduma za utoaji dawa kwa wanafunzi watumishi na jamii nzima” amefafanua.